SALMA Hamidu, mkazi wa Igogo, jijini Mwanza ameibuka na kudai amezaa
na marehemu Steven Kanumba mtoto wa kike aitwaye Treasure Steven Charles
Kanumba (2), Ijumaa linashuka na maneno ya kinywa chake.
Akizungumza na mwandishi wetu, Salma anayefanya kazi kwenye Ofisi ya
Uwakili ya Law Consultancy jijini Mwanza, alidai alianza kufahamiana na
marehemu mwaka 2006 wakati yeye akiwa kwenye Kundi la Nyakato Arts chini
ya Mwalimu Joseph.
CHANZO CHA UHUSIANO
Salma akasema kuwa, uhusiano
wao uliunganishwa na Mwalimu Joseph ambaye alimpa marehemu namba zake
za simu wakati alipopeleka filamu za Machozi Yangu na Siri Yangu
kuifanyia uhariri (editing) jijini Dar es Salaam katika studio alizokuwa
akifanyia kazi marehemu.
“Marehemu alipoona picha zangu kwenye
filamu hizo alivutiwa na mimi katika kuigiza, akaomba namba zangu za
simu kwa Mwalimu Joseph,” alisema Salma.
Mrembo huyo aliendelea
kuweka wazi kuwa, baadaye Mwalimu Joseph alirejea Mwanza na kumtaka
radhi kwa kumwambia alimpa Kanumba namba zake za simu.
SIMU YA KWANZA YA KANUMBA KWA SALMA
“Baada ya wiki mbili nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha ni Kanumba. Aliuliza kama huwa nasafirisafiri.
“Nilimjibu si sana kwa sababu nasoma. Wakati huo nilikuwa nasomea
kompyuta kwenye Chuo cha English Kingdom Nyakato,” alisema Salma.
Akaongeza: Marehemu alinielewa, lakini akaniomba niwe mwenyeji wake
punde atakapokuja Mwanza, nikaridhia ombi lake, alikata simu, lakini
tukaendelea kuwasiliana kwa simu kila mara.
Salma alisema mawasiliano yake na Kanumba yalidumu kwa mwaka mmoja bila kuonana ‘laivu’.
Aidha, alidai kuwa siku moja marehemu alimpigia simu akimtaka kujiunga
na kundi lake lililopo Dar, akamkubalia lakini tatizo likawa umbali.
“Lakini marehemu akaniambia nisiwe na wasiwasi kuhusu hilo,” alisema
Salma.
Akizidi kumwaga data za uhusiano wao ulivyoanza, Salma alisema:
LAIVU KWA MARA YA KWANZA
“Mwaka 2007, Kanumba
aliniita Dar, alinitumia tiketi ya ndege ya Precision Air, kwetu niliaga
nakwenda kumsalimia mama mkubwa anayeishi Tabata.
“Nilipofika Dar,
nilimpigia simu Kanumba kumtaarifu nimefika, akanitaka tukutane Ubungo
Plaza Hotel (Blue Pearl),” alisema Salma.
Pale Ubungo Plaza,
marehemu kwa mara ya kwanza alimtamkia lililo moyoni mwake kwamba
ametokea kumpenda na akamuomba wawe wapenzi.
“Sikuwa na uamuzi wa haraka, lakini kutokana na ushawishi wake nilikubali, baadaye nilirudi Tabata kwa mama mkubwa.
“Usiku alinipigia simu, akaniomba kesho yake tusafiri kwenda Zanzibar,
nilikubali, asubuhi niliaga kwa shangaza tukaenda Zanzibar.
“Tulifikia Bwawani Hoteli. Tulikaa kwa siku tatu na kwa mara ya kwanza
nilikutana na marehemu kimwili. Tuliporudi Dar mimi nikarejea Mwanza,”
alisema Salma.
KANUMBA PENZI LAKOLEA, ATUA MWANZA
“Baada ya
kama miezi minne na siku kadhaa hivi, marehemu alinipigia simu akasema
yuko Mwanza, anataka kuja chuoni kuniona. Alikuja akiwa ameongozana na
marafiki zake wawili, Credo na Theonist Rutashoborwa.
“Walikuja hadi
chuoni, mimi nilitoka tukaenda kukaa kwenye baa ya Shentemba. Ilipofika
saa 2 usiku, tukahamia Isamo Hotel,” alisema Salma.
Salma
aliendelea kusema kuwa, pale Isamo walipata chakula kabla ya kujitupa
kitandani lakini siku hiyo muda mwingi alikuwa akijisikia vibaya,
marehemu akamtaka asubuhi akapime.
“Asubuhi nilikwenda kwenye
Kliniki ya Dokta Ng’walida, daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na
watoto. Vipimo vilionesha nilikuwa na ujauzito wa miezi minne.
“Nilimwonesha marehemu majibu yale, hakuonekana kukubali wala kukataa,
lakini baadaye akasema kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia
hadi atakaponiambia.
“Baada ya siku mbili, aliaga kurejea Dar
pamoja na marafiki zake. Siku chache baadaye huku nyuma kwa bahati mbaya
ujauzito ulitoka, nilikwenda kwa daktari mmoja Nyakato National ambaye
alithibitisha hilo. Huo ulikuwa mwaka 2008.
UJAUZITO WA PILI
Salma alisema kuwa mawasiliano na marehemu yaliendelea. Kuna siku alimpigia simu akimtaka wakutane jijini Arusha.
Alipofika alipokelewa na Kanumba mwenyewe kabla ya kwenda kupiga kambi kwa rafiki yake mmoja aliyekuwa akiishi peke yake.
Akasema kukutana kwao kimwili kwa safari hii, ndiko kulimpa ujauzito na hatimaye kujifungua binti anayeitwa Treasure au Tunu.
Arusha waliondoka na ndege hadi Mwanza ambapo walifikia Ladson Hotel,
ipo Bwiru na kukaa kwa siku mbili kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani
kwao Igoma.
Akiwa na ujauzito huo, Kanumba alimtumia nauli akimtaka wakutane mjini Morogoro.
“Nikiwa na tumbo langu, aliniita Morogoro, nilisafiri kwa basi hadi
kule, nilifikia kwa shangazi yangu yeye alipanga kwenye hoteli ipo
jirani na Kituo cha Mabasi cha Msamvu.
KANUMBA ATOA ONYO
“Kulitokea kutokuelewana
kidogo na marehemu kwa sababu ya ujauzito ule, akirejea mazungumzo yake
ya awali kuwa, kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia, lakini
nilimwambia sina namna ya kufanya kuhusu ujauzito ule.
“Hata hivyo,
marehemu alinionya nisimwambie mtu kuhusu ujauzito kuwa ni wa kwake, iwe
siri yangu na yake kwa sababu hakutaka habari hiyo ifike kwenye
magazeti,”alisema Salma.
Akaongeza: Baada ya hapo, alinipa shilingi 150,000 nikarudi nyumbani Mwanza.
“Nikiwa Mwanza alikuwa akinipigia simu akitaka kujua naendeleaje na
tumbo langu na kunitaka nijiandae kwa safari ya Dar, atanitumia tiketi
ya ndege.
“Nilisafiri, nilipofika Dar nilimjulisha, akasema tusikae
Dar, twende Zanzibar. Kule tulifikia tena Bwawani Hotel. Tulikaa kwa
siku nne, kisha tukarejea Dar.
Lakini tukiwa Zanzibar kuna mtu
alinipigia simu na yeye akiwepo, alikasirika sana na kuninyang’anya
simu, akachukua namba kisha akampigia mtu huyo, waligombana kwenye simu.
Aliipasua simu yangu, akaenda kuninunulia nyingine.
“Alikuwa mtu
mwenye hasira, hakutaka kusikia unazungumza na simu hasa ikiwa ni sauti
ya kiume. Ugomvi huo ulisababisha aikane mimba, akasema namsingizia ni
ya mwanaume aliyenipigia simu. Ilifika mahali akasema kila mtu aishi
kivyake.
“Hata hivyo, alikuja kuniomba msamaha huku akizidi kunionya kuwa ole wangu nitangaze nina mimba yake.”
Alisema ugomvi wake na Kanumba ulitokana na ujauzito na ilifika mahali
Salma alimweleza mama yake ambaye alimlaumu kwa kujiingiza kwenye
uhusiano na mwanaume huyo.
MISAADA KUTOKA KWA KANUMBA
Kwa upande wa
misaada, Salma alisema akiwa mjamzito, marehemu alimtumia shilingi
Milioni mbili na laki mbili kwa ajili ya kununua kiwanja.
Baadaye
alimtumia shilingi Milioni moja za kupanga nyumba. Fedha hizo alizituma
kupitia Benki ya Standard Chartered Tawi la Mwanza.
Baada ya kutuma
fedha hizo, marehemu aliwahi kwenda Mwanza na kufikia kwenye Hoteli ya
Ryans Bay. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba.
HAKUTAKA KUPIGA NAYE PICHA
Salma anasema:
Nilimtaka tupige picha ya ukumbusho akakataa, lakini nilipojifungua
alikuja na kumpiga picha mtoto kwa kutumia simu yake akisema, ‘mtoto
mama yangu mtupu kwani amefanana naye sana.’
Aliongeza kuwa
alipojifungua Kanumba alimtumia shilingi 500,000 za matumizi ya mtoto
kupitia simu ya mama yake mzazi na Salma (hakumtaja jina).
Aliendelea kusema kulijitokeza sakata wakati wa kumpa jina mtoto,
Kanumba akitaka amwite jina la mama yake, huku Salma naye akitaka
kumwita la mama yake, ndipo wakakubaliana mtoto aitwe Treasure au Tunu
ili kumaliza mzozo wa kugombea kumwita mtoto jina la upande mmoja.
“Treasure alipofikisha miezi saba alisema nimpige picha nimtumie ili
amwone alivyofikia, nilifanya hivyo. Siku moja akaniambia angetunga
filamu kuhusu maisha yetu ambayo alipendekeza iitwe My Gift.
“Siku
chache kabla ya kifo chake alinipigia simu pamoja na mtoto akisema
alitaka kusafiri na asingekuwepo kwa mwezi wote wa Machi mwaka huu,
alimsamilia mwanaye. Lakini cha kushangaza siku chache nikapewa taarifa
za kifo chake,” alisema Salma.
KWA NINI USIRI?
Salma alisema mpaka sasa
anashindwa kuelewa ni kwa nini marehemu alitaka uhusiano wao uwe wa
siri. Lakini baadhi ya marafiki zake walikuwa wakifahamu uhusiano huo.
NENO LA MWISHO LA SALMA
“Kanumba kaniacha njia
panda, sijui la kufanya, lakini ni vyema kama angemtambulisha mwanaye
kwa ndugu zake kuliko hivi sasa ambapo mengi yatazuka kuwa pengine
natafuta fedha za marehemu.
“Sijaweka wazi ili nipate chochote, bali nahisi dhambi kuficha kwa sababu huyu mtoto si damu yangu peke yangu.
“Nitakuwa mbaya kwa Mungu kama nisiposema ukweli. Angekuwepo mwenyewe
nisingesema kwa sababu yeye ndiye alikuwa kiongozi wa maisha ya mtoto.
“Narudia tena, nina uwezo wa kumlea na wala sihitaji mtoto achukuliwe
na kwenda kuishi kwa baba, ila familia ijue kuna damu yao kwangu.
“Kama hawataamini, niko tayari kufika Dar na kupima DNA ili familia ya marehemu ijiridhishe,” alisema Salma.
Hata hivyo, Salma alikiri kufanya kosa la kutowahusisha marafiki wa
Kanumba kumtegulia kitendawili hicho na kudai pengine umri mdogo
ulichangia. Salma alizaliwa mwaka 1987.
Alisema mtu pekee ambaye
watu wanamfahamu na ndiye shahidi wa uhusiano wake na marehemu ni msanii
wa maigizo, Ramadhan Malele ‘Swebe’ ambaye alikuwa akiwasiliana naye
mara kwa mara.
Salma alisema kabla Kanumba hajafikwa na mauti, yeye
aliwahi kukutana na Swebe jijini Mwanza ambapo alimsimulia hali ilivyo
na akamshauri kusikiliza matakwa ya marehemu ya kutotoa siri ya kuwepo
kwa mtoto huyo.
Chanzo:http://www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment