Monday, 21 March 2011

HATIMA YA KIKOMBE CHA LOLIONDO WIKI IJAYO

WAKATI watu kutoka sehemu mbalimbali nchini wakiendelea kuimimini katika kijiji cha Sumange, wilayani Loliondo kupata tiba kwa Mchungaji wa KKKT, Ambilikile Mwasapile, Serikali imesema itatoa matokeo ya uchunguzi wa ubora wa dawa inayodaiwa kutibu magonjwa sugu, inayotolewa na wiki ijayo.

Hata hivyo, Serikali imesema hadi sasa hakuna madhara yoyote yaliyoripotiwa kutokana na dawa hiyo hivyo, wananchi wanaweza kuendelea kuitumia, akidokeza kuwa matokeo ya uchunguzi huo hayawezi kuleta tofauti yoyote katika imani za watu ambao wametumia dawa hiyo.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa wakati matokeo ya uchunguzi huo uliofanywa na Mkemia Mkuu yakisubiriwa kwa hamu, huku mamia ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wakiendelea kumiminika kupata tiba ya dawa hiyo inayodaiwa kutibu magonjwa sugu kama kisukari, moyo, saratani na ukimwi kwa gharama ya Sh500 tu.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu Alhamisi wiki hii, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya alisema uchunguzi huo umeshakamilika na taarifa ya mwisho itatolewa wiki ijayo.
Alisema wataalamu wameshafanyia uchunguzi dawa hiyo, lakini alikataa kutoa matokeo ya uchunguzi huo hadi hapo yatakapotangazwa rasmi.

“Nafikiri taarifa kamili itatoka wiki ijayo, … tusubiri tu na watu watajulishwa,” alisema Dk Nkya.
Hivi karibuni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilitoa tamko la kusitisha kwa muda shughuli za matibabu zinazofanywa na mchungaji Ambilikile, maarufu kwa jina la Babu hadi hapo itakapojiridhisha na ubora wa dawa hiyo, lakini siku moja baadaye Serikali iliruhusu huduma hiyo iendelee kutolewa.

Akitoa agizo la kusitisha kutolewa kwa matibabu hayo hivi karibuni, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, alisema kutokana na hali halisi ya usalama wa kiafya katika eneo hilo, kulikuwa na hatari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Dk Mponda aliongeza kuwa Serikali ilishaanza kuchukua hatua za awali ikiwamo ya kupeleka wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ambao alidai kuwa waliwasili eneo hilo wiki moja iliyopita na kuanza kufanya uchunguzi.

Kwa mujibu wa Dk Mponda, utaratibu wa kisheria wa utoaji wa dawa unamtaka atakayegundua dawa ya aina yoyote kufuata taratibu zilizopo ikiwamo kuthibitishwa na TDFA ili kuangalia ubora na madhara yake kwa watumiaji.
Hata hivyo, uchunguzi huo utakabiliwa na changamoto mbalimbali kwani kwa mujibu wa Mchungaji Ambilikile, dawa hiyo alionyeshwa na Mungu na inahitaji imani ili ifanye kazi, jambo ambalo siyo rahisi kuthibitishwa kitaalamu kwa njia ya maabara.

Akizungumzia utata huo, Dk Nkya alisema kwa sababu hakuna madhara yoyote yaliyoripotiwa kutoka kwa watu waliotumia dawa hiyo, matokeo ya uchunguzi huo hayawezi kuleta tofauti yoyote katika imani za watu ambao wametumia dawa hiyo.

“Hadi sasa hakuna taarifa yeyote ya ‘side effects’ (madhara ya dawa hiyo), watu wanaweza kuendelea kutumia dawa hiyo, lakini tusubiri taarifa kamili ya uchunguzi uliokuwa ukifanywa,” alisistiza Dk Nkya.

Kuhusu hali ya usalama wa mazingira katika kijiji hicho ambacho kila siku kinazidi kufurika watu wanaoenda kupata dawa hiyo, Dk Nkya alisema maafisa Afya waliopo wilayani wanahakikisha taratibu za afya kwa watu waliopo eneo hilo zinazingatiwa na kuimarishwa.

“Baraza la Afya la mji wa Loliondo ndio wenye jukumu la kuhakikisha hali ya afya inadhibitiwa, hadi sasa hawajatupa taarifa yoyote kuwa wamezidiwa na wanahitaji msaada kutoka wizarani,” alisema Dk Nkya.

mwananchi

No comments:

Post a Comment