Tuesday, 6 March 2012

CHADEMA;JK VUNJA BARAZA LA MAWAZIRI

  Send to a friend
Monday, 05 March 2012 21:02
0diggsdigg
Baraza la Mawaziri
Boniface Meena
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kulivunja Baraza la Mawaziri kwa maelezo kwamba limeshindwa kumshauri hivyo kusababisha hali ngumu ya maisha na kuyumba kwa uchumi wa nchi huku, migogoro ikiendelea kushamiri.Tamko hilo la Chadema linakuja kipindi ambacho tayari madaktari wametoa siku tatu kwa Serikali wakitaka kung'olewa kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya kutokana na kushindwa kusimamia sekta ya afya nchini.

Akisoma maazimio ya kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliyoketi juzi jijini Arusha, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, alisema Chadema pia kinamtaka Rais Kikwete kufumua maeneo mengine ya Serikali yake kwa kuwa mfumo wake ni mbovu usiokidhi haja ya kutekelezwa kwa majukumu yake.

Mnyika akisoma maazimio hayo jijini Dar es Salaam jana alisema, "Kamati Kuu haijaridhishwa na jinsi Serikali inavyoshughulikia suala la uchumi na hali tete ya kisiasa ikiwa ni pamoja na migogoro mbalimbali na hiyo inatokana na uwezo mdogo wa mawaziri wa JK."

Alisema CC ya Chadema haijaridhishwa na jinsi Serikali ya Rais Kikwete inavyoshughulikia mambo mbalimbali nchini na hilo linatokana na mkuu huyo wa nchi kukosa washauri wazuri katika baraza lake la mawaziri.

Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo alisisitiza, "Rais aanze na baraza lake la mawaziri kwa kulivunja kisha aende kwenye ngazi mbalimbali ambazo ameteua viongozi wabovu, awaondoe."

Alisisitiza, "Na hii inatokana na katiba tuliyonayo kumpa nafasi ya kuchagua watu kadri anavyotaka."

Mnyika alifafanua kwamba ili kupunguza makali na machungu kwa wananchi yanayosababishwa na uongozi huo mbovu, ni lazima Rais aanzie kwenye chombo chake kinachomshauri ili aweze kurekebisha mfumo mbovu uliopo.

"CC imezungumzia suala la migogoro inayotokea nchini na kuona kuwa Serikali inashindwa kushughulikia vyanzo vya migogoro hiyo. Hivyo ni lazima ishughulikie vyanzo vya migogoro na kuacha masihara kwenye hilo,"alisema Mnyika.

Mnyika alisema kutokana na hali ya uchumi na siasa kuwa tete CC imeamua kuwa Baraza Kuu la Chadema litakalokaa Aprili mwaka huu lijadili hali hiyo na kutoa mapendekezo kwa Serikali jinsi ya kurekebisha mambo kama Rais hatalivunja baraza hilo ambalo limekuwa mzigo kwa nchi.

Kuhusu Katiba
Akizungumzia msimamo wa CC kuhusu utoaji wa maoni ya marekebisho ya Katiba, Mnyika alisema wametambua kuwa marekebisho yaliyofanyika kwenye mkutano wa Bunge wa ulioisha Februari 10 mwaka huu kama ni ya awali hivyo CC inataka Serikali kuendelea na awamu ya pili ya mchakato huo.

"Taarifa kuhusu suala la katiba CC inatambua kuwa marekebisho yaliyofanyika kwenye mkutano wa Bunge ni ya awali hivyo inataka Serikali kuendelea na awamu ya pili na marekebisho yake kufanyika Bunge lijalo la Aprili mwaka huu,"alisema Mnyika.

Alisema CC imeamua kuwa Chadema itaendelea kutoa elimu ya marekebisho ya katiba kwenye mikutano yake, ili kuwafungua wananchi waweze kutoa maoni kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba mpya.

Mnyika alisema kutokana na wito wa Rais Kikwete kutaka majina kutoka kwa vyama ya watu watakaoingia katika tume ya mchakato wa katiba, Chadema imekaribisha maombi na mapendekezo ya watakaotaka kuingia kwenye tume hiyo.

"Kama Serikali ilivyotamgaza kuanza kwa tume hiyo kila chama kimetakiwa kuwa na wawakilishi watatu, Chadema inakaribisha maombi na mapendekezo na mwisho wa kupokea maombi hayo ni Machi 11 mwaka huu ili tuweze kufanya utaratibu,"alisema Mnyika.

Uchaguzi wa chama, Arumeru
Mnyika alisema Baraza Kuu la Chadema litakaa Aprili 29 mwaka huu na kutangaza tarehe za kufanyika kwa uchaguzi wa ndani wa chama kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.

Alisema pia Baraza Kuu litapitisha bajeti ya mpango mkakati wa muda mrefu wa chama hivyo viongozi wote wa chama walioko katika ngazi mbalimbali wajiandae kuwasilisha maoni yao.

"Kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama CC imeamua Baraza Kuu lifanyike Aprili 29 mwaka huu na kwamba nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kitongoji, kata kwenda juu zitawaniwa,"alisema Mnyika.

Kuhusu bajeti ya uchanguzi mdogo wa ubunge jimbo la Arumeru Mashariki, Mnyika alisema chama kimeamua kuwa kampeni za uchaguzi huo ziendeshwe kwa nguvu ya umma bila kutegemea ruzuku za chama.

Alisema chama kimejipanga kupata misaada kutoka kwa wananchi wa Arumeru na wananchi wengine nchini katika kuhakikisha hakitumii ruzuku ya chama kwenye uchaguzi huo.

"Kampeni za Arumeru zitaendeshwa kwa nguvu ya umma ikiwa ni pamoja na kupata fedha za wananchi kote nchini na si kutegemea ruzuku za chama bali za wananchi kwa ujumla na hasa Arumeru,"alisema Mnyika.

Alisema chama kimeteua watu kadhaa wa kuangalia jinsi gani ya kupata fedha hizo za nguvu ya umma na kile kiasi ambacho kitahitajika kuongezeka chama kitatangaza kiasi gani kitatumika.
a

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment