Friday, 9 March 2012

MAHAKAMA KUU YASITISHA MGOMO WA MADAKTARI NCHINI

 

Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, leo (Alhamisi Machi 8, 2012) imetoa uamuzi wa kusitishwa mara moja kwa mgomo wa Madaktari ulioitishwa nchi nzima tangu jana (Jumatano Machi 7, 2012).
Katika amri yake ya pili, Mahakama Kuu pia imekitaka Chama cha Madaktari Tanzania na Jumuiya ya Madaktari kuwatangazia wanachama wao mara moja kupitia Vyombo vya Habari kusitishwa kwa mgomo huo nchi nzima kama walivyowatangazia wakati wanauitisha mgomo wenyewe.
Mahakama Kuu pia imeamuru pande zote mbili, yaani Serikali kwa upande mmoja na Chama cha Madaktari na Jumuiya ya Madaktari, kwa upande mwingine, kutumia fursa zilizopo katika kutatua mgogoro wa kikazi uliopo kati yao kwa haraka.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu imetolewa na Jaji R.M. Rweyemamu, baada ya kusikiliza ombi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Chama cha Madaktari na Jumuiya ya Madaktari kuitaka itoe zuio kwa mgomo huo.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Rweyemamu alisema anazingatia madhara ambayo mgomo huo ungeleta kwa jamii kwa vile huduma za tiba ambazo madaktari walitaka kugoma kuzitoa ni miongoni mwa huduma muhimu zilizotajwa kwenye Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba 6 ya Mwaka 2004.
Uamuzi huo, ni kama ifuatavyo:
Leo, tarehe 8, Machi 2012, Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, mbele ya Jaji R.M. Rweyemamu, baada ya kusikiliza Ombi No. 24 la 2012 lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Mwombaji) dhidi ya Chama cha Madaktari Tanzania na Jumuiya ya Madaktari (Walalamikiwa), imetoa uamuzi ufuatao:
i) Chama cha Madaktari Tanzania na Jumuiya ya Madaktari pamoja na Wanachama wao, kusitisha Mgomo waliouanzisha rasmi tarehe 7 Machi 2012 nchi nzima na kurejea kazini mara moja kwa kuendelea na kazi zao kama kawaida, mara tu Amri hii itakapowafikia. Aidha, waombaji watatakiwa kutoa Kiapo cha kuthibitisha kwamba wamewasilisha Amri hiyo kwa Walalamikiwa na kuwasilisha Kiapo hicho Mahakama Kuu – Divisheni ya Kazi kesho tarehe 9, Mach 2012.
ii) Mara baada ya Amri hii kuwasilishwa kwa Walalamikiwa (Chama cha Madaktari Tanzania na Jumuiya ya Madaktari) watatakiwa kuwatangazia Wanachama wao kupitia Vyombo vya Habari kusitishwa kwa Mgomo huo Nchi nzima kama walivyowatangazia wakati wa kuitisha Mgomo huo;
iii) Mahakama inaamuru pande zote mbili (Serikali na Chama cha Madaktari Tanzania pamoja na Jumuiya ya Madaktari) kutumia fursa za Kisheria zilizopo katika kutatua Mgogoro wa Kikazi uliopo kati yao kwa haraka.
Imetolewa na:
Ofisi ya Waziri Mkuu,
S.L.P. 3021
DAR ES SALAAM.
Alhamisi Machi 8, 2012

No comments:

Post a Comment