Tuesday, 10 July 2012

Profesa Mahalu Kusuka Au Kunyoa Leo




Tausi Ally
MAHAKAMA ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Euro 2 milioni, sawa na Sh3.1bilion  inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania, nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.

Hukumu ya kesi hiyo iliyokuwa ikinguruma mahakamani hapo kwa miaka kadhaa sasa, itasomwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ilvin Mgeta.

Profesa Mahalu  na Grace wanakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara hiyo.

Mei 8 mwaka huu Grace ambaye alikuwa Ofisa wa Utawala aliieleza mahakama hiyo ya  Kisutu kuwa Balozi  Mahalu hakuisababishia serikali hasara  ya kiasi hicho cha fedha, bali alileta faida kwa taifa kwa   kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.

Akiongozwa na Wakili Mabere Marando  kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili, Grace alidai kuwa kwa ufahamu wake Balozi Mahalu hakuisababishia serikali hasara kwa kuwa manunuzi yalileta faida na nchi kupata jengo zuri na hakuna fedha zilizopotea.

“Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, Balozi Mahalu mashtaka yote sita yanayomkabili hakuyatenda, aliwasilisha  mikataba miwili kama taarifa iliyofanyika kihalali,”alidai Grace.

Aliendelea kuiomba mahakama itupilie mbali tuhuma hizo  na kwamba madai ya kuwa Balozi Mahalu alitumia risiti ya ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia kuidanganya serikali kuwa mwenye nyumba amelipwa fedha siyo ya kweli.

Hata hivyo, akiongozwa na Wakili Marando, Grace  alihoji ni kwanini upande wa Jamhuri haukumleta mmiliki wa jengo hilo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia  kukana risiti hiyo  au Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru), Edward Hossea  na Fungo  kuulizwa juu ya ununuzi wa jengo hilo kwa sababu walikwenda nchini humo kufanya uchunguzi. 

No comments:

Post a Comment