Monday, 30 July 2012

SAKATA LA GPL NA CHAMELEON LINAENDELEA,SOMA HAPA


Joseph Mayanja ‘Chameleone’.
Na Saleh Ally
KUMEKUWA na maswali mengi sana kuhusiana na mgogoro ulioibuka kati ya Kampuni ya Global Publishers (GPL) na msanii Joseph Mayanja ‘Chameleone’ wa Uganda ambaye anadaiwa dola 3,500 (zaidi ya Sh milioni 5) alizochukua halafu hakuzifanyia kazi.
Global iliingia mkataba na Chameleone kupitia wakala wake aitwaye George kwa ruhusa ya Chameleone mwenyewe. Mganda huyo alikubali GPL iingie mkataba na wakala huyo kwa niaba yake ili aje nchini Julai 7, kutumbuiza katika Tamasha la Usiku wa Matumaini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Msanii Kidumu raia wa Burundi, ndiye aliiwakilisha GPL na baada ya kuwasiliana na Chameleone, walikutana naye akamtambulisha George. Baada ya kuingia mkataba huo, dola 3,500 ambazo zilikuwa za utangulizi zikatolewa maana msanii huyo alitaka dola 5,000 katika malipo yote. Baada ya hapo maandalizi yakiwemo matangazo ya tamasha hilo yakaendelea.
Alipoanza kuulizwa kuhusiana na kuja, Chameleone akagoma kwa madai kwamba George hakumpa fedha! Alipoulizwa kwamba yeye ndiye alimtambulisha wakala huyo, sasa vipi liwe tatizo la GPL? Akasisitiza haelewi lolote na hatakuja.
GPL ilishaanza matangazo, hivyo ikaona ni vizuri kuzungumza naye upya ili imlipe tena dola 5,000. Ajabu, safari hii akageuza bei, akasisitiza kama wanamhitaji, wamlipe dola 8,000 (zaidi ya Shilingi milioni 12) na si kwa advance, alitaka alipwe yote.
Kwa ajili ya kulinda heshima kwa kuwa GPL ilishatangaza kuwa atakuwepo katika tamasha, meneja wake Abdallah Mrisho, akafunga safari hadi Kampala na kumlipa Chameleone kitita cha dola 8,000. Mkataba mpya ukatengenezwa, ule wa mwanzo ukaendelea kuwepo.
Chameleone alitua nchini kwa ajili ya shoo, safari hii GPL ikiwa imelazimika kulipa tiketi za ndege za watu watatu badala ya wawili kama yalivyokuwa makubaliano ya mwanzo. Alipewa Range Rover Vogue ambalo alilitumia kwa safari zake zote akiwa hapa nchini.
Alifikia katika hoteli inayomilikiwa na GPL. Baada ya shoo, uongozi wa GPL ulitaka kujua kuhusiana na fedha za mkataba wa kwanza ambazo Chameleone alitoa maagizo wakala wake asaini mkataba huo halafu baadaye akaruka. Yakatokea mabishano, naye akaondoka hotelini hata bila ya kuaga.
Kawaida katika hoteli hiyo kumekuwa na utaratibu wa kuhifadhi pasi za kusafiria za wageni, baada ya kutokea matatizo kadhaa na wateja kutoka nje ya nchi. Baada ya kuondoka, siku iliyofuata Chameleone alituma mtu arudie pasi zake akidai yeye alikuwa Zanzibar katika tamasha.
Uongozi wa hoteli uligoma kuzitoa hadi afike mwenyewe, naye akagoma kwa madai hana shida kwa kuwa anajua zitapelekwa. Baada ya hapo, ndiyo akarejea kwao kufuatia kupata pasi za kusafiria kutoka ubalozi wa Uganda nchini. Mbaya zaidi akavamia ubalozi wa Tanzania nchini Uganda na kufanya vurugu akidai pasi zake.
Kwa kuwa uongozi wa hoteli ulikabidhi pasi ya kusafiria ya Chameleone kwa uongozi mkuu, nao siku chache baadaye ukazikabidhi kwa serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Baada ya hapo, jambo hilo limezidi kupasua anga huku baadhi ya watu wakionekana kulikuza bila ya kujua lolote linaloendelea. Ili mradi wamerukia tu huku wakitangaza eti, pasi ya kusafiria ya Chameleone ni ya kidiplomasia kwa kuwa alipewa na Rais Yoel Museven, kitu ambacho ni uzushi mtupu tena usiokuwa na maana.
Wapo wanaotangaza eti GPL imemtapeli Chameleone, kivipi? Wakati yeye ndiye amefanya utapeli kupitia wakala wake George, utaratibu ambao amekuwa akiutumia kwa watu wengine ambao amewahi kuwatapeli. Chameleone maana yake ni kinyonga, mnyama ambaye ngozi yake inaweza kubadilika rangi kutokana na mazingira aliyopo, ndicho anachokifanya.
Kwa nini yeye?
Jiulize mara mbili au tatu kwamba kwani ni mara ngapi GPL imewahi kufanya kazi na wasanii wa nje bila ya kuzuka mgogoro wowote? Hata Chameleone mwenyewe hajalalamikia malipo kutoka GPL, badala yake kampuni ndiyo inamlalamikia yeye kwa utapeli.
Kumjua George:
GPL ingeweza vipi kufika kwa George bila ya kutambulishwa na Chameleone mwenyewe? Yeye ndiye alimtambulisha George kwa Kidumu aliyekuwa mwakilishi wa GPL, kwamba aingie naye mkataba kwa kuwa ndiyo utaratibu wake anaoutumia kwa mawakala. Kama kweli George hakumpa Chameleone fedha, vipi tatizo liwe la GPL?
Kenya v Uganda:
Rekodi zinaonyesha Chameleone hafanyi shoo Kenya na hasa Nairobi, ikitokea akaenda huko, basi atalazimika kuwa chini ya ulinzi mkali. Yote ni kutokana na utapeli mkubwa ambao ameufanya huko kwa zaidi ya mara moja. Wakenya aliowatapeli, wote alitumia mfumo huohuo wa wakala.
Angalia Wakenya namna walivyokuwa wakali na kushikilia msimamo wa kutaka haki zao zilipwe, hapa nyumbani Watanzania wanadai haki yao kwa Mganda huyo lakini wanaopiga vita tena kwa juhudi kubwa ni Watanzania wenzao! Yote hiyo ni chuki, ndiyo maana wapo wanaothubutu kunyoosha mkono kwa GPL bila hata kujua chanzo cha tatizo, yote hiyo kwa kuwa Watanzania wengi chuki ndiyo msingi unaotuongoza!
DJ JD:
Ameibuka na kusema aliwahi kutapeliwa na Chameleone dola 3,000 (zaidi ya Sh milioni 4.5), hiyo ilikuwa mwaka 2004. Hadi leo amekuwa akipiga chenga kumlipa na kuna wakati alimwambia aandae onyesho aje atumbuize ili wawe wamemalizana, akafanya hivyo na kwa mara ya pili hakutokea tena!
Wapo ambao wanaamini Chameleone hawezi kufanya utapeli, wanaona ni mtu ‘smati’ sana. Huenda amefanya upuuzi huo sehemu nyingi lakini hakuwahi kukutana na watu wanaojua kudai haki yao na wasiokubali kukaa kimya kwa kuhofia kelele za watu wengi ambazo unaweza kuzilinganisha na za chura.
JD aliwahi kumkimbiza Chameleone kama mwizi alipokuja hapa nchini, alitaka kumtia nguvuni katika mikono ya Jeshi la Polisi. Lakini DJ huyo anasema Merrey Balhabou na Rita Poulsen walimuombea msamaha wakidai atamlipa, naye akaahidi hivyo, hadi leo changa la macho. Kula fedha za bure kuna utamu wake, lakini mwisho wake utakuwa mbaya kwake.
Biashara:
Kuna mpango, kampuni moja ambayo hufanya masuala ya burudani, imeonyesha kufurahia sana kutokea kwa utapeli huo wa Chameleone. Inachofanya sasa ni kulikuza suala hilo kwa nguvu zote, kwanza ni kama faraja kwao kusikia GPL inaingia katika mgogoro kwa kuwa wamekuwa na mafanikio makubwa katika matamasha yao ukilinganisha na wao ambao hufanya kwa msimu maalum.
Kuna taarifa wanataka kulikuza zaidi suala hilo ili baada ya muda Chameleone awe gumzo halafu wamlete wao nchini kutumbuiza. Hivyo, kwa kutumia vyombo vyao na watu wa kutengeneza katika mitandao, wamekuwa wakilikuza na kusukuma kashfa nyingi, taarifa tunazo na nguvu ya kupambana nao hadharani na ikiwezekana mafichoni, tunayo.
Kawaida ya Watanzania huona kila kilicho nje ya nchi ni bora zaidi, ndiyo maana hadi leo wengi hawaamini kwamba Uwanja wa Taifa ni mzuri na bora kuliko viwanja vingine ndani ya Afrika Mashariki na Kati. Huenda kingekuwa Uganda au Kenya, basi wangeambiwa ni bora wangekubali.
Huo ni utumwa wa mawazo na kuwapa nafasi wale wanaoamini wao ni bora kwa hisia na kwa kuwa wanakuzidi kuzungumza Kingereza tu, basi unaamini kweli wao ni bora. Tuache uwoga, hapa GPL tunaheshimu lakini hatuhofii yeyote yule hata chembe, tena hasa unapofikia wakati wa kudai haki yetu ambayo tunaamini tunastahili kuipata, sisi ni Watanzania.

GPL

No comments:

Post a Comment