WAKATI kumbukumbu ya milipuko ya mabomu katika kambi ya JWTZ ya Gongo la Mboto ikiwa bado hazijafutika katika fikra za wakazi wa jiji la Dar es Salaam, mabomu mengine ya jeshi yamelipuka katika kambi ya Kizumbi mkoani Shinyanga.Lakini tofauti na milipuko ya GongolaMboto, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 20, na wengine 400 kujeruhiwa, milipuko ya Kizumbi, hayakuleta madhara yoyote.
Milipuko ya Gongo la Mboto iliyotokea usiku wa Februari 16 mwaka huu, pia imesababisha mamia ya wananchi, kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao, kuharibiwa.
Habari za awali zilisema mabomu ya Kizumbi, yalilipuliwa kwa makusudi kwa lengo la kuyateketeza baada ya kuthibitika kuwa muda wake, umepita.
Ingawa mabomu hayo hayakuleta athari, yamesababisha taharuki kubwa, kama iliyowakuta wananchi wa Gongo la Mboto ambao wengi wao walikimbia na kwenda katika maeneo wasiyoyajua, ili kusalimisha maisha yao.
Habari zilisema kulipuliwa kwa mabomu katika kambi ya Kizumbi, kulianza Ijumaa iliyopita na kwamba milipuko hiyo, imesababisha hofu kubwa miongoni mwa wananchi.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema hofu hiyo imewakumba zaidi wakazi wa mji wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa habari hizo, ulipuaji wa mabomu katika kambi hiyo iliyoko nje kidogo ya mji huo, jana uliingia katika siku yake ya tatu.
Mmoja wa wananchi mwenye makazi yake karibu na kambi hiyo, Masumbuko Masunga (36), alisema milipuko hiyo imesababisha watu wengi kukimbia makazi yao.
Alisema hatua hiyo imetokana na hofu ya kupoteza maisha kama ilivyowahi kutokea kwa wakazi wa Mbagala na Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani, alithibitisha kutokea kwa milipuko hiyo, lakini aliwataka wananchi, wasiwe na wasiwasi kwa sababu mabomu hayo yanalipuliwa wanajeshi wenyewe.
Kamanda Diwani alisema kabla ya kuanza kwa kazi ya kulipua mabomu hayo, JWTZ ilitoa taarifa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga na wa watu wa vijiji vyote vinavyozunguka kambi.
Kwa mujibu wa kamanda huyu, kazi ya kuteketeza mabomu hayo, inatarajiwa kukamilika leo.
Hata hivyo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha JWTZ, Luteni Kanali Kapambala Mgawe, aliliambia gazeti hili jana kuwa hana taarifa kuhusu ulipuaji wa mabomu hayo.
Alisema "nilisikia taarifa hiyo tangu jana (juzi) lakini, hazikuwa rasmi na baadaye nikajua kuwa hazikuwa na ukweli wowote," alisema Mgawe.
"Sisi tunafanya kazi saa 24, taarifa hizo nimezisikia tangu jana sidhani kama zina ukweli wowote. Mabomu ya Gongo la Mboto nilipata taarifa baada ya dakika 10 tu tangu mabomu yaanze kulipuka, lakini hayo unayonieleza sijapata taarifa yoyote. Labda mabomu hayo yawe yanalipuka sasa hivi," alisisitiza.
Ofisa huyo wa JWTZ alisema hajapata taarifa zozote kuhusu kulipuka kwa mabomu.
"Sidhani kama kuna kitu kama hicho, ngoja tuangalie, haiwezekani tukio kama hilo litokee msemaji wa jeshi nisiwe na taarifa," alisisitiza.
Kamanda Diwani alisema tangu kuanza kwa kazi ya kuyateketeza mabomu hayo, hakuna taarifa yoyote inayohusu athari au madhara kwa wananchi na mali zao.
Tathmini Gongo laMboto vurugu tupu
DOSARI zimeanza kujitokeza katika tathmini ya mali iliyoharibiwa kwa milipuko ya mabomu iliyotokea kambi ya JWTZ Gongo la Mboto, baada ya wathamini kukataa kutambua mali zilizoteketea kabisa.
Habari zilisema wathamini hao wanataka waonyeshwe mabaki ya mali zilizosalia na si kuelezwa kuhusu mali zilizotekea kabisa, jambo ambalo limezua mtafaruku baina yao na waathirika.
Msimamo huo, juzi ulisababisha kuzuka kwa vurugu zilizoambatana na kutupiana maneno kati ya wananchi na kikundi wathamini wanaoendesha shughuli hiyo.
Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea Gongo la Mbobo juzi, aliwakuta wasimamizi hao wakizozana na waamiliki wa nyumba waliotaka mali zao zitambuliwe na kufanyiwa tathmini, lakini wathimini wakagoma.
"Msituonyeshe mali ambazo hazipo,tunataka kuandika mali zinazoonekana tu, zile ambazo hazionekani hatuhusiki nazo kabisa ndivyo tulivyoogizwa,"alisema mmoja wa wathamini hao, kutoka Ofisi ya Waziri (Mkuu Kitengo cha Maafa).
Ofisa huyo ametambuliwa kwa jina moja la Christopher.
Kauli hiyo iliibua hasira za wakazi ambao walianza kurushiana naye maneno huku wakisema huo ni usanii waliokuwa wakiutegemea kutoka katika serikalini.
Mkazi wa Gongo la Mboto aliyejitambulisha kwa jina moja la Agnes alisema hawana imani kabisa kuhusu mpango wa kuthamini mali kwa sababu haki haitendeki."Tulijua watatusaidia lakini kumbe wanatumia lugha chafu kwetu kama vile wanaongea na maadui zao,"alisema.
Violet Sambiwa alisema lugha ya matusi inayotumiwa na wathamini hao si nzuri na kwamba wanapaswa kuwasikiliza waathirika na kutekeleza haja zao.
Gazeti hili lilipotaka kuzungumza na mmoja wa wathamani hao, aligoma na kusisitiza kuwa asingependa kupigwa picha."Nyie mnaojiita waandishi hebu nipatieni vitambulisho vyenu ndio muanze kupiga picha hapa la sivyo mwondoke,"alisema.
Pamoja na kumpa vitambulisho, ofisa huyo aliendelea kugoma kuzungumza na waandishi na badala yake, aliwafukuza akisema kwa mujibu wa taratibu zao, hawatakiwi kupigwa picha wakiwa kazini.
Serikali yashauriwa kurejesha mafunzo ya JKT
SERIKALI imeshauriwa kurejesha sheria ya lazima ya mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuwasaidia wananchi kupata mbinu za kujihami na majanga.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Radio Sauti ya Qurani, Shamim Khan.
Khan ambaye aliwahi kuwa mbunge na waziri, alitoa ushauri huo wakati kamati hiyo ilipotembelea waathirika wa mabomu Gongo la Mboto na kutoa misaada mbalimbali kwao.
Alisema maafa yanakuwa makubwa kwa sababu wananchi wengi hawajui namna ya kujihami na majanga na badala yake wanakimbia hovyo.
Khan alishauri JWTZ kutoa mafunzo ya namna ya kujihami na majanga ya namna hiyo kupitia vituo vya televisheni na radio ili wananchi waelewe.
source:mwananchi
No comments:
Post a Comment