Tuesday 20 November 2012

WALIOMUUA SWETU FUNDIKIRA WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA.



Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam imetoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa wanajeshi watatu waliokuwa wakishitakiwa na kesi ya  kumuua mtoto wa Chifu Abdallah Fundikira, Swetu Fundikira kwa kukusudia. Adhabu hiyo imetolewa mapema leo baada ya kuwakuta na hatia washitakiwa wote watatu kwa mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Wanajeshi hao ni Sajenti Rhoda Robert (42) wa  Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha Mbweni,Koplo Ally Ngumbe (37) wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kikosi cha Kunduchi na Koplo Mohamed Rashid. Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Zainabu Mruke ambaye alisikiliza kesi hiyo.

Katika hukumu yake Jaji Mruke alisema kuwa imethibitika kuwa washitakiwa waliua kwa kukusudia.

"Midhahir hakukuwa na shahidi wa moja kwa moja washitakiwa waliua lakini mazingira yanaonesha Swetu aliuawa na washitakiwa hao" alisema Jaji Mruke. Aliongezea kuwa ni wazi upande wa mashitaka umeweza kuithibitishia mahakama pasi na shaka yoyote kuwa washitakiwa walitenda kosa la mauaji ya kukusudia.

Marehemu Swetu aliuawa kutokana na majeraha yaliyotokana na kupigwa kitu kichwani, jambo ambalo  lilithibitishwa na Daktari  wa Hospitali ya Taifa Muhimbili aliyetoa ushahidi kuwa alifanyia uchunguzi mwili wa marehemu.

Kwa mujibu wa ushahidi, Januari 23 mwaka huu, Marehemu Swetu alikutana na washitakiwa katika makutano ya barabara ya Kawawa na Mwinjuma Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es salaam,  ambapo baadaye wanajeshi hao walimchukua wakidai kuwa wanampeleka kituo cha polisi cha Oysterbay lakini hawakumpeleka huko. Badala yake  alikutwa usiku wa manane eneo la msikiti wa Jamatini, Upanga, jijini humo, akiwa na washitakiwa katika hali mbaya mpaka mauti yalipomkuta katika hospital ya Taifa ya Muhimbili walikodaiwa kuwa walikuwa wanampeleka.

Hata hivyo hawakufanya hivyo na baadaye walikutwa katika eneo la msikiti wa Jamatini huku mwili wa marehemu ukiwa umelala kifudifudi ukiwa hauna nguo yeyote zaidi ya soksi ya mguu wa kulia ambapo katika utetezi wao walidai kuwa  Swetu alivua nguo mwenyewe na kwamba alijirusha kutoka kwenye gari wakimpeleka kituo cha Polisi Kikuu.

Washitakiwa walishindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu kifo cha Swetu kwa sababu ni wao ndio waliondoka nae akiwa katika hali ya uzima na ni wao walikutwa nae akiwa hoi hajitambui, na baadaye kufa.

Kama ambavyo inafahamika adhabu ya kunyongwa ni adhabu kubwa, ndugu wa washitakiwa hao walilia mahakamani baada ya kusomwa hukumu hiyo huku wengine wakizimia. 

Hata hivyo wakili wa washitakiwa hao Mhe Ruge Kalori hakuridhishwa na hukumu hiyo  hivyo alisema kuwa atakata  rufaa.
 
ISAACKIN SAY
 
I HOPE HII HUKUMU ITATIMIA ILI HAKI IENDE SAWA,ANAYEMJUA SWETU ATAJUA KWAMBA NDUGU YETU YULE KAULIWA KWA MAKUSUDI TU KIBABE.
ILA KIZUNGUMKUTI CHA SHERIA BONGO HAKIELEWEKI,USISHANGAE JAMAA WAKAKATA RUFAA NA BAADA YA HAPO WAKASHINDA KESI KISHA BAADA YA SIKU MBILI TATU UNAWAKUTA WANADUNDA MTAANI,HAPO NDIO MAUMIVU YA KICHWA HUANZA POOOOLE POLE.

No comments:

Post a Comment