Friday, 17 June 2011

Waziri Pinda ajitosa mjadala wa posho


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ametetea malipo ya posho kwa wabunge na watumishi wengine wa umma na kusema kwamba ni jambo dogo ambalo halipaswi kupewa uzito mkubwa kama linavyojadiliwa hivi sasa.
Kadhalika, Pinda alisema suala la malipo ya posho kwa wabunge na watumishi wengine wa umma lipo kisheria, hivyo posho hizo zitaendelea kutolewa hadi hapo sheria itakapoangaliwa upya.

Pinda alijikuta akiingia katika mjadala kuhusu mapendekezo ya kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na watumishi wengine wa umma, ambapo aliwalaumu wabunge wa Chadema kwamba wanakuza jambo hilo tofauti na ukubwa wake."Ni kwa bahati mbaya kwamba jambo hili limekuwa likikuzwa sana, mimi naamini kuwa ni jambo dogo, lakini kwa jinsi linavyokuzwa linaleta sura tofauti kabisa," alisema Pinda na kuongeza:
"Hata Chadema, wabunge wake watakuwa wanamezea mezea mate, lakini sasa wafanyeje".

Alisema suala hilo limekuzwa katika misingi ya kutaka kuifanya Serikali ionekane kwamba inawaibia wananchi, jambo ambalo si kweli na kwamba sehemu kubwa ya posho wanazopewa wabunge huzitumia katika kuwasaidia wananchi kwenye majimbo yao au nje ya majimbo.
Pinda alikuwa akijibu swali la papo kwa papo lililoulizwa na Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa ambaye alitaka kauli ya Serikali kuhusu hoja ya kufutwa kwa posho ambayo alisema imekuwa ikiwajengea chuki wabunge dhidi ya umma.Katika swali lake hilo, Mnyaa alianza kwa kunukuu Katiba ya Nchi, akibainisha kuwa malipo ya mishahara, posho na stahili nyingine kwa wabunge ni ya kikatiba.

Baadaye akataka kujua endapo Serikali itawachukulia hatua zozote wabunge wanaopinga posho hizo kwa kuwa "Wanavunja Katiba". Akijibu swali hilo, Waziri Pinda alisema posho hizo zipo katika makundi mawili. "Kundi la kwanza ni stahili zilizopo kwa mujibu wa sheria kufuatana na katiba ya Jamhuri Muungano wa Tanzania, ambazo pia wabunge wanaangukia katika kundi hilo la kwanza kwa hiyo ni vigumu kuzifuta."

“Hizi (posho) ukitaka kuzirekebisha lazima kukaa na kuangalia upya sheria, lakini tu niseme hili ni suala linalozungumzika.Hakuna haja ya kukwaruzana. Mimi najua wapo wabunge wa Chadema wengi wanamezea mate posho hizi, lakini  wafanye nini!”alisema Pinda.

Alisema watu wanaposema posho hizi zifutwe wana maana hata zile wanazopewa wanajeshi ziondoshwe, jambo ambalo ni gumu, vivyo hivyo kwa madiwani ambao kimsingi hawana mishahara.

Waziri Mkuu alisema, posho za watumishi, hasa wabunge zinaweza kupitiwa upya na kufanya marekebisho, ikiwamo kuziingiza katika mishahara yao, lakini jambo la muhimu ni kutowapotosha wananchi wakaona kuwa wanaibiwa na Serikali yao.“Sehemu kubwa ya posho za wabunge hawazitumii. Hili ni suala linalozungumzika.Tuketi tuziangalie posho hizi, ikiwezekana ziingizwe katika mishahara,”alisema Pinda.

Chadema na Serikali
Kauli ya Pinda inaweza kuchochea upya mvutano baina ya Chadema na Serikali kuhusu posho za vikao, mvutano ambao ulikuwa umeanza kupungua baada ya kuwapo kwa mtazamo kwamba, pande zote zilikuwa zikikubaliana umuhimu wa suala hilo kufanyiwa kazi.
 Juzi Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe alisisitiza katika bajeti mbadala ya upinzani kuwa kufutwa kwa posho ni suala la lazima na kwamba kwa kufanya hivyo, Serikali inaweza kuokoa Sh987 bilioni ambazo zinaweza kuelekezwa katika maeneo mengine kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akihojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), alisema suala hilo linajadilika na kwamba ni ajenda ya Serikali kupunguza matumizi kwa kupitia upya malipo ya posho hizo.

 Katika kipindi hicho, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliweka bayana kuwa mapendekezo ya wapinzani ni kupitiwa upya kwa posho zote za watumishi wa umma kwa kuwa mwanya huo unatumiwa vibaya na watendaji wa sekta mbalimbali kufuja fedha za umma.
 Mbowe alisema uwapo wa 'ruhusa' ya malipo ya posho za vikao, unasababisha kutungwa kwa vikao vingi visivyo na tija katika halmashauri, mashirika na taasisi nyingine za umma nchini.

Kimsingi Lukuvi alikubaliana na hoja ya Mbowe na kuweka wazi kwamba kwa muktadha huo, suala hilo inabidi lifanyiwe kazi kwa kuwapo kwa mashauriano baina ya pande husika bila kuwaweka kando wafanyakazi wa sekta zote, kupitia vyama vyao vya wafanyakazi.

 CCM kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kilishasema kuwa hakipingi wala kuunga mkono kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na watumishi wengine wa umma, lakini kikabainisha kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa na kufikia mwafaka.
 Kwa upande wake,  Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema viongozi wa Chadema wamekuwa wakitafuta umaarufu wao binafsi kwani nao wamekuwa wakipokea posho hizo.

Chadema watishia kurudi kwa wananchi
Katika hatua nyingine, Chadema kimesema kuwa kama Serikali haitasikiliza hoja yao kuhusu posho watarudi kwa wananchi na kuandamana.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe mara baada ya kutoka kwenye Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma alikokwenda kuhojiwa kuhusiana na kutojaza fomu za kuorodhesha mali anazomiliki.
Alisema hata Mpango wa Maendeleo wa Serikali wa miaka mitano umezungumzia suala la kupunguzwa kwa posho za safari na kusema kuwa hoja yao ni ya msingi na inazungumzika.

“Ni bahati mbaya sana kusikia Waziri Mkuu anasema wasiochukua posho zitarudi Hazina, wakati Serikali anayoiongoza imeleta hoja hiyo hapa bungeni kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano,”alisema Mbowe na kuongeza:
“Mbunge kwa mwezi anapata zaidi ya Sh7 milioni, je ni watumishi wangapi katika nchi hii wanapata mshahara wa zaidi ya Sh1 milioni?”Alihoji.

Alisema Waziri Mkuu anazungumzia suala hilo kama ni la wabunge pekee wakati wao wanazungumzia wananchi wote, kwani pesa hizo zitapelekwa kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Kama wasipobadilisha hizi posho tutakutana na wananchi kwenye maandamano,”alisema.
Alisema posho wanayoilalamikia ni (sitting allowance) na kwamba kila mtu anahitaji mishahara mizuri na si mbunge pekee.

Alisema kuzungumza bungeni na kukaa kwenye kamati ni kazi ya mbunge na kuhoji kwanini mbunge huyo alipwe kwa ajili ya kukaa tu.Mbowe alisema hivi sasa mapato mengi yanayokusanywa na Serikali yanaishia kwenye kulipana posho.

MWANANCHI.


NENO LANGU:
si ndio huyu bwana alijiita mtoto wa mkulima hapo nyuma?sidhani kama anapenda kuitwa hivyo tena maana na yeye atakuwa ni mmojawapo ya wafanyabiashara wakubwa wa si hasa.haya bana hongera yako muhishimiwa

No comments:

Post a Comment