Thursday, 18 August 2011

Pinda atetea kugawa ardhi kwa wawekezaji

*Akiri kushiriki mazungumzo, akana kuuza hekta 400
*Tibaijuka atangaza kibano wasioendeleza mashamba



WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda amekiri kuwapo makubaliano kati ya Kampuni ya Agri-sol Energy Tanzania na Halmashauri ya Mpanda kuhusu matumizi ya
ardhi, huku akisema kuwa hakuna mkatana wowote kuhusiana na suala hilo

Akitoa ufafanuzi kuhusu swali la Mbunge wa Kawe (CHADEMA), Bi Halima Mdee aliyemtaka Waziri Mkuu kuangalia kwa makini suala la mwekezaji ambaye amepewa miliki ya ardhi kwa miaka 99 katika maeneo ya Lugufu na Mishamo, Bw. Pinda alisema kilichofikiwa ni MOU.

"Hakuna mkataba wowote tulioingia, hiyo ardhi mnayosema tumeuza iko wapi, tupeni nafasi, watu wa Rukwa na Kigoma tunawaambieni hatukosei ng'o," alisema Waziri Mkuu Pinda.

Alisema eneo linalozungumziwa lipo katika jimbo lake na amewahi kushiriki katika mazungumzo hayo akiwa mwenyekiti wa mazungumzo hayo, lakini hakuna mkataba wa uuzaji huo.

Awali, akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kwa Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Mdee alisema kuwa Waziri Mkuu anapaswa kuliangalia suala hilo kwa makini zaidi kwa kuwa suala hilo linagusa hata ofisi yake.

Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu alisimama na kutoa taarifa kuhusu suala hilo, kuwa hadi sasa hakuna mwekezaji aliyepewa hatimiliki mkoani Rukwa, lakini kilichopo hivi sasa ni mazungumzo kati ya mwekezaji huyo na halmashauri.

Kutokana na hali hiyo, Bi. Mdee alisimama tena na kusema kuwa kwanza haihitaji taarifa hiyo na kuongeza kuwa, ukweli wa jambo hilo upo na tayari kuna kitabu kuonesha makubaliano kati ya Agrisoil na halmashauri.

Hata hivyo, alisema kuwa yeye kama Mbunge wa Kawe hivi sasa hatafuti umaarufu wa kisiasa, kwani tayari umaarufu huo anao na anacho kifanya hivi sasa ni kutetea wananchi wanyonge ambao wanaporwa haki zao.

Wakati mbunge huyo akiwasilisha maoni hayo, alisema kuwa hivi karibuni kampuni ya Agrisol Energy LLC na kampuni ya Serengeti Advisor inayoongozwa na Bw. Iddi Simba aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Bishara katika Awamu ya Tatu na Bw. Betram Eyakuze kwa pamoja wameunda kampuni ya Agrisol Energy Tanzania.

Alisema kuwa tayari watu hao wameingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda na kusema kuwa mkataba huo unatarajia kuipa kampuni husika miliki ya ardhi ya miaka 99 ya maeneo ya Lugufu hekta 80,317 na Mishamo hekta 219,800.

Alibainisha kuwa masharti ya msingi katika makubaiano hayo baina ya halmashauri husika na mwekezaji ni kulipa kodi ya ardhi ambayo ni sh. 200 kwa hekta, ushuru wa kisheria wa halmashauri na ada itakayolipwa halamshauri ni sh 500 kwa hekta.

Alisema kama mgogoro utatokea baina ya pande zote mbili, busara itatumika kutatua mgogoro husika na ikishindikana chemba ya biashara ya kimataifa ICC ndio atakuwa msuluhishi.

Akizungumzia suala la migogoro mbalimbali ya ardhi katika Jimbo la Kawe, mbunge huyo alisema kuwa serikali inapaswa kufuatilia kwa makini na kuwabaini wale wote waliohodhi maeneo kinyume na utaratibu na kuwarudishia wananchi.

Alisema kuwa viwanja vya wazi katika Mkoa wa Dar es Saalam serikali ilifikia kuunda tume kuchunguza maeneo hayo na kuhoji taarifa ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam, Bw. Wiliam Lukuvi inatekelezwa kwa muda gani tangu ilipomaliza kazi yake na kuwasilishwa kunakohusika.

Kwa upande mwingine naye Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) Bw. Ezekia Wenje alisema kuwa mkoa wa Mwanza umekuwa ukikabiliwa na matatizo ya watu kuporwa ardhi yao kutokana na baadhi ya maofisa ardhi ambao wameota mapembe kutokana na serikali kutowachukulia hatua kali za kinidhamu.

Alisema kuwa miongoni mwa watu hao ambao wamekuwa kero katika Jiji la Mwanza ni pamoja na mmoja wa watumishi ambaye yupo idara ya ardhi, aliyemtaja kwa jina moja la Otieno na Frank Joseph ambaye ni Ofisa Mipango Miji katika jiji hilo na kusema kuwa maofisa hao ni kero.

Serikali inapaswa kusafisha watu kama hao katika wizara yake kwani wamekuwa kama majinamizi, huku serikali ikilea uovu huo bila kuwachukulia hatua kali na pindi inapochukua hatua huwahamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine badala ya kuwawajibisha.

Alisema kuwa hivi sasa jiji la Mwanza lina migogoro mingi ya ardhi hasa katika maeneo ya Luchelele, Kapri Point, Isamilo na Bugalika, hali ambayo aliitaka serikali kutafuta ufumbuzi wa kero mbalimbali za wananchi katika maeneo hayo ili wananchi waweze kupata haki zao kama fidia au ardhi yao.

Tibaijuka ajibu hoja za wabunge

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema atakutana na pande mbili zizazogombana katika mgogoro wa Ardhi eneo la Chasimba, Kata ya Makongo Juu katika Jimbo la Kawe Dar es Salaam.

Akitoa ufafanuzi kwa hoja mbalimbali za wabunge jana, Profesa Tibaijuka alisema pia kuwa serikali itachukua ardhi kwa wale walioshindwa kuendeleza maeneo waliyomilikishwa na badala ya kukodisha wengine.

Alisema atavalia njuga migogoro ya ardhi kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Kawe, Bi. Halima Mdee ili haki itendeke na wenye haki wapate haki yao kufuata sheria za ardhi ya Mipango Miji ya mwaka 2007.

Alisema ardhi ni mali ya serikali na mwisho wa kumiliki ni miaka 99 lakini mtu anaweza kumnyang'anywa kwa kushindwa kutekeleza masharti.

Alisema makazi bora hayawezi kuja kwa digrii bali yatakuja kwa kukamilisha kazi ya kuifanya ardhi ipendeze kufanana na madhari nzuri ya Tanzania, hivyo ni lazima wengine wadhurike ili kufikia lengo hilo.

Alisema mradi wa New Kigamboni ni lulu na italeta ajira kwa vijana wengi wa Tanzania na kujengwa nyumba za kisasa, mahoteli na kubadilisha kabisa madhari ya eneo hilo
CHANZO:MAJIRA
 

No comments:

Post a Comment