Wednesday, 10 August 2011

Polisi Uingereza walaumiwa kutozima ghasia

 

Polisi wa kukabiliana ghasia

Machafuko zaidi yameendelea maeneo kadhaa nchini Uingereza baada ya kushuhudia ghasia na uporaji usiku kucha kuamkia Jumatatu.
Mkuu wa polisi katika mji wa Manchester amesema maafisa wake wamekuwa na wakati mgumu kukabiliana na magenge ya vijana aliowataja kufanya vitendo vya jinai.
Katika mji wa pili mkubwa Birmingham, vijana waliwalenga polisi kwa mawe pamoja na kupora maduka. Zaidi ya washukiwa mia moja wamekamatwa katika maeneo ya Manchester na Midlands. Matukio haya yameacha idara ya Polisi kulaumiwa na raia kwamba haijawajibika ipasavyo katika kuthibiti hali.
Idara ya ujasusi imejipata tena matatani, hata kabla ya kuuguza sakata ya udukuzi wa simu, idara hii imeanza kutiliwa shaka utendakazi wake na umma.Ni wakati mgumu sana kwa idara ya polisi katika miaka mingi.
Mwezi jana polisi walijipata matatani kufuatia sakata iliyokumba gazeti ya News Of the world.Mkuu wa polisi Paul Stephenson aliye na ujuzi wa miaka mingi alilazimika kujiulu pamoja na afisa wake wa juu Jon Yates.
Kuondoka kwa wawili hao kulipelekea kuwepo na mageuzi katika idara ya polisi hali ambayo imepelekea kulegea katika kufanya maamuzi ya haraka kufuatia ghasia zilizozuka wikendi iliyopia katika eneo la Totten ham..Machafuko yalichacha kiasi cha polisi kushindwa kuthibiti hali.
Waliachwa kuwalinda wazima moto badala ya kuwakamata waporaji.Hata hivyo mkuu wa polisi Simon Foy amewatetea maafisa wake akisema walifanya kila wawezalo kuthibiti hali japo wamekabiliwa na wakati mgumu.
Aidha suala lingine limeathiri idara ya polisi ni mpango wa serikali kupunguza matumizi yake ambapo bajeti ya polisi imepunguzwa, hivyo kupunguza maafisa wa usalama. Inakadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2015 takriban polisi 34,000 watakuwa wameachishwa kazi Uingereza na Wales.
Hakuna ishara ya wizara ya ndani kubatilisha mpango wa kupunguza makadirio ya polisi, lakini ikiwa ghasia hizi zitaendelea huenda mawaziri wakashurutishwa kuachana na mpango huo unaotaka kupunguza marupurupu ya polisi wakati wa masaa ya ziada na malipo mengine.
Huku haya yakiarifiwa Marekani nayo imetoa onyo kwa raia wake dhidi ya kuzuru Uingereza. Aidha raia wake wanaoishi Uingereza wameonywa dhidi ya kushiriki kwenye ghasia hizo au kuwa karibu na matukio ya ghasia. Hatua kama hii imekuwa ikilenga maeneo ya vita duniani. Lakini matukio yanayoendelea Uingereza bila shaka imewaacha wengi vinnywa wazi kote duniani

BBCSWAHILI

No comments:

Post a Comment