Wednesday, 10 August 2011

Wauza mafuta wapigwa kitanzi



MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetoa amri kwa kampuni nne kubwa zinazosambaza mafuta kurejesha huduma hiyo mara moja huku ikizitaka kujieleza, kwa nini zisichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa leseni zao za biashara.

Kampuni hizo ni pamoja na BP ambayo Serikali inamiliki nusu ya hisa pamoja na Engen, Oil Com na Camel. Mbali ya maagizo hayo mawili, Ewura pia imezitaka kampuni hizo kuhakikisha kwamba zinaendelea kutoa huduma hiyo bila kubughudhi mfumo wa usambazaji mafuta nchini.
Aidha, Ewura pia imetoa leseni kwa Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuingiza mafuta kuanzia jana ikisema ombi lake la kupatiwa leseni ya kuuza ndani ya nchi litashughulikiwa baada ya kubainisha miundombinu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alisema kisheria, amri hiyo (Compliance Order) ni sawa na agizo la Mahakama Kuu na kwamba wahusika hawana budi kutii. Mbali na kampuni hizo, Masebu alisema pia kwamba kampuni nyingine ndogo za mafuta zinachunguzwa na zitakazothibitika kuhusika katika mgomo wa kutoa huduma hiyo muhimu ya nishati, zitachukuliwa hatua.
Agizo la Ewura limekuja sambamba na hatua ya Bunge kusitisha shughuli yake kawaida jana ambayo ilikuwa ni mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara na kujadili mgomo wa wafanyabiashara ya mafuta ambao mpaka jana, walikuwa wamesitisha uuzaji wa bidhaa hiyo katika vituo mbalimbali nchini na kusababisha kusimama kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Ombi la kujadili suala hilo liliwasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya bunge ya Nishati na Madini, January Makamba.
Baada ya mjadala uliochukua sehemu kubwa ya shughuli zake za jana, Bunge liliazimia kwa kauli moja kwamba Serikali ihakikishe amri hiyo ya Ewura kama ilivyowasilishwa kwake na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja inatekelezwa.
Akihitimisha hoja yake, Makamba alitoa hoja kwamba sheria ifuate mkondo wake na kuitaka Serikali kuchukua hatua kwa kampuni zitakayokaidi agizo hilo mara baada ya muda uliotolewa kumalizika. Pia alisema: “Kwa sababu tatizo hili ni la nchi nzima na watakaoanza kunufaika ni wakazi wa Dar es Salaam, Serikali ihakikishe kuwa na mikoani mafuta yanapatikana kama kawaida.”

Michango ya wabunge
Awali, akichangia hoja hiyo, Makamba alisema tangu Ewura ilipotangaza kushuka kwa bei ya mafuta, hali imekuwa mbaya lakini kabla ya hapo mafuta yalikuwa yanatosha. Alisema hatua ya kushuka bei ya mafuta ililenga kuwapunguzia wananchi mzigo na ni suala lililopitishwa na wabunge na kuelezea kushangazwa kwake na jinsi usimamizi wa sheria ulivyochelewa kutekelezwa.

Makamba alisema nchi imekuwa kwenye mgawo wa umeme kwa muda mrefu lakini nishati ya mafuta ni muhimu zaidi kuliko umeme: “Hili ni tatizo kubwa, lazima Serikali ionyeshe ipo na ina uwezo wa kusimamia, watu sasa wananunua kwa mfano, Korogwe lita moja ya mafuta ni Sh3,000, Handeni Sh4, 000 naambiwa Tabora hakuna kabisa mafuta... hili ni jambo la hatari kwa usalama wa nchi,” alisema Makamba na kuongeza:

“Tunataka kuiona hali ya mafuta inarejea kama ilivyokuwa awali, kama tutashindwa kufanya uamuzi, nchi itasimama, wananchi hawatuelewi. Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndicho kimeunda Serikali, lakini suala hili la mafuta linavyofanyika sivyo wananchi walivyotegemea. Mheshimiwa Waziri sema kitu, Mheshimiwa Waziri Mkuu sema kitu, kwa sababu ipo Ewura lakini Serikali ipo, haiwezekani siku saba nzima hatujasikia Waziri Mkuu amesema kitu, wala Waziri amesema kitu kwa nini? Hili jambo baya, tunaomba muonyeshe mpo na mnafanya kazi.”

Akichangia hoja hiyo ya mafuta, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe alitaka wafanyabiashara hao waagizwe kufungua vituo vya mafuta na kuendelea kutoa huduma mara moja na kwamba kama hawatafanya hivyo hadi jana saa 12:00 jioni, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), livifungue na kuyauza kwa nguvu.

Alisema katika hali ya kawaida imezoeleka kuona wanaogoma ni wafanyakazi na hajawahi kutokea wafanyabiashara wakagoma: “Hatujasikia wafanyabiashara wamekata rufani tangu kushushwa bei au wamekwenda Tume ya Ushindani (FCC) kukata rufani. Wanataka kutuonyesha ubabe wao, wanataka kutumia jeuri ya fedha, Watanzania siku zote ni maskini jeuri, leo mafuta yatoke, Ewura waagize yatoke ikifika saa 12 jioni wamegoma basi wanyang’anywe leseni mara moja  na JWTZ liingie na wafungue vituo mafuta yatoke.”

Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alisema bado Serikali ina haki ya kulinda maslahi ya raia wake akisema wafanyabiashara kwa kutumia umoja wao, wameamua kukiuka maagizo la Ewura.

Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa alisema tatizo hilo linatokana na makosa yaliyoanzia bungeni akisema chombo hicho kimeshindwa kuisimamia Serikali ipasavyo: “Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika Bunge la Tisa, iliwahi kupendekeza kuwa Serikali  kupitia TPDC, ianze kusimamia biashara ya mafuta, lakini haijatekeleza.”

Alisema umefika wakati Serikali ijue kwamba siyo kila wakati maagizo ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), yana manufaa kwa nchi kama Tanzania, kwani Serikali kujitoa kwa asilimia 100 katika biashara ni makosa.

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ambaye alijinasibu kuwa ni mtaalam katika sekta ya mafuta, alisema tatizo kubwa lililopo ni kanuni inayopanga bei. “Serikali imepotoshwa, siku ambayo tulipandisha bei ya mafuta ya taa niliwaambia Ewura wapime akiba ya mafuta ya taa iliyopo na watu ambao walipandisha siku ya pili tu walikuwa ni watu wa kukamatwa.”

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema ana ushahidi vigogo wa Serikali kuhongwa katika sakata la mafuta na kwamba hilo pia limefikia hapo kutokana na udhaifu wa Serikali: “Tusiiadhibu Ewura, kwani walitekeleza wajibu wao, lakini pia katika hili Takukuru wanapaswa kuchukua hatua ya kuchunguza kwani nina ushahidi viongozi na maofisa wa Serikali kuhongwa katika jambo hili.”

Alisema inashangaza kuona kwamba, Serikali ina hisa asilimia 50 katika Shirika la BP lakini pia shirika hilo linagoma kuuza mafuta wakati ni mali ya Serikali: “Tunamiliki asilimia 50 BP, tunamiliki asilimia 50 katika Tipper halafu tunaambiwa mafuta hakuna, Serikali yetu ipo wapi, nashauri Serikali kuchukuwa hatua.”

Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene aliitaka Serikali kuwafungulia mashtaka wauzaji hao kwa kuwa wamekiuka Sheria ya Ushindani wa Kibiashara (FCC). Alisema kuwa wametishia usalama wa nchi hivyo ni muhimu Watanzania wakasimama pamoja na kuonyesha uzalendo kwenye suala hilo.

"Tuchukue hatua zozote kwa kuwa tuko tayari kwa lolote. Lazima tuonyeshe ukakamavu kwenye hili kwani usalama wa nchi si kulinda tu, bali hata kumiliki nishati," alisema Simbachawene.

Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa alisema kuwa uhuru waliopewa wauzaji wa mafuta wanautumia vibaya na hiyo ni changamoto kwa Serikali na kwamba inapaswa kulishughulikia suala hilo bila kuyumba kwa kuwa wananchi wana shida na ndiyo inayoweza kuwasaidia.

Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani alisema wafanyabiashara hao wanaiyumbisha Serikali na ndiyo maana wiki nzima wananchi wameteseka. Alisema vyombo vya dola vilipaswa kuhakikisha vina taarifa za kutosha kuhusu kiasi cha mafuta kilichopo ikiwepo kwenye maghala ili kutoa taarifa kamili ya hali ilivyo:  “Hata mawasiliano yao vyombo vya dola vilipaswa kuyajua katika kipindi hiki.”

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema kampuni za mafuta zimepewa fursa ya kufanya biashara hiyo lakini si haki yao... “Ndiyo maana wanaweza kunyang'anywa leseni wakati wowote ule." Alitaka zinyang'anywe fursa hiyo kwa kuwa zinataka kuathiri uchumi wa nchi.

Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile alisema ni muhimu Serikali ikachukua hatua ndani ya saa 24 na kuhakikisha wananchi wanapata mafuta: “Tuwakague na tukikuta mafuta tuyachukue na tuwafutie leseni.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan alisema kama si Makamba kuomba suala hilo lijadiliwe, Serikali ilikuwa imelala: “Serikali ichukue hatua na mpaka kesho tatizo liwe limekwisha na kama itashindikana mawaziri waondoke kwa kuwa hawana kazi ni waoga.”

Mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi alisema kilichofanywa na kampuni hizo ni usaliti kwa taifa na kitawaharibia biashara yao: “Serikali ichukue hatua na kuwanyang'anya leseni kisha ichukue mafuta na kuyauza.”

Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere alisema katika suala hilo ndiyo sehemu Serikali inapotakiwa kujisafisha: “Tunahitaji hatua zichukuliwe. Tunahitaji kuona makali ya Serikali ili kuondoa dhana ya kuonekana kuwa ni legelege”.

Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage alitaka sheria ya kuweka watu kizuizini irudishwe ili watu waache kuichezea Serikali kama mpira.

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment