Friday, 5 August 2011

WAMAREKANI KUMILIKISHWA ARDHI MPANDA RUKWA

KAMPUNI ya AgriSol Energy LLC ya Marekani, inakamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi ya hifadhi katika Wilaya ya Mpanda, mkoani Rukwa, uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini.

Eneo linalotarajiwa kumilikishwa kwa kampuni hiyo, linahusisha ardhi iliyopo katika kambi za wakimbizi za Katumba yenye ukubwa wa ekari 80,317 na Mishamo yenye ukubwa wa ekari 219,800.

Eneo lingine ni la  kambi ya Lugufu iliyoko mkoani Kigoma yenye ekari 25,000.

Kwa mujibu wa tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitembelea Marekani ambako pamoja na mambo mengine. aliitembelea Kampuni ya AgriSol Energy LLC yenye makao yake katika Jimbo la Iowa
Katika ujumbe wake, Pinda alifuatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Sazi Salula, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dk Servacius Likwelile na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ya Uchumi wa Zanzibar,  Amina Shaaban.

Habari zaidi zilisema katika kongamano la uwekezaji lililofanyika Januari mwaka huu mkoani Rukwa, Pinda alieleza haja ya kuipokea AgriSol akisema kuwa serikali imefikia maamuzi hayo baada ya wakimbizi kuondolewa kwenye makambi hayo na wengi wao kurejea makwao.

Pinda alifafanua kuwa kuna zaidi ya hekta 29 milioni zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hapa nchini, lakini ni asilimia moja tu ya ardhi ndiyo inayotumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na hii inatokana na uwezo mdogo wa mtaji na teknolojia kwa wakulima hapa nchini.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili hivi karibuni, wilayani Mpanda, Ofisa Programu wa Taasisi ya Haki Ardhi, Bernard Baha, alisema mpango huo unafanywa kwa ushirikiano wa washirika wa kampuni hiyo na viongozi wa serikali kwa kile kinachoelezwa kuwa ni uwekezaji wa mkakati wa kilimo kwanza.


"Mmoja kati ya washirika wa karibu wa kampuni hiyo nchini ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Idd Simba, ambaye ndiyo kiongozi wa Agrisol Tanzania yenye ofisi zake Mikocheni A, jijini  Dar es Salaam.

"Mshirika mwingine nchini ni Kampuni ya Serenge Advisers Limited," alisema Baha.

Katika waraka ambao Mwananchi Jumapili imefanikiwa kuuona,Simba ameitetea kampuni hiyo ya Marekani kuwa, taarifa zake zimekuwa zikipotoshwa na watu wengine.

"Habari za hivi karibuni zimekuwa zikipotosha nia yetu. Nikiwa kama mhusika wa Agrisol Tanzania tangu mwanzo najua watu, mipango, siasa na faida za mradi huu kwa Tanzania. Mradi wetu umelenga kuwashirikisha wakulima wa ngazi ya juu wa dunia na kuifanya ardhi ya Tanzania kuwa katika viwango vya juu na matumizi stahiki," anasema Simba katika waraka huo.


Kwa mujibu wa Simba, AgriSol inatarajia kutumia zaidi ya Dola za Marekani 7000 kwa ajili ya miradi ya kilimo katika maeneo hayo matatu.

Baha amewataja washirika wengine wa Agrisol kuwa ni pamoja na Taasisi ya Pharos Global Agricultural Fund, iliyo chini ya Pharos Financial Group ya Dubai, inayoongozwa na Peter Halloran


Nyingine ni Summit Group yenye makao makuu, Iowa Marekani ikijishughulisha na kilimo na ufugaji na Chuo Kikuu cha Iowa kinachoheshimika  kwa masuala ya ardhi nchini humo.

Chuo hicho kimepewa kazi ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu  udongo, hali ya hewa, mvua na hali ya eneo zima.
Kwa mujibu wa Baha, tayari serikali imeshafanya makubaliano ya awali na kampuni hiyo.

"Kuna mambo kadhaa yenye utata katika makubaliano hayo, kwa mfano muda wa miaka 99 katika mkataba huo ni mrefu mno. Vilevile, kampuni hiyo kutumia wafanyakazi kutoka nje ya nchi na hivyo kuwakosesha ajira wazawa. Kuna matumizi ya mbegu za mazao zilizoboreshwa (GMO) kinyume na sheria za nchi. Halafu kama kutatokea mgogoro, mkataba huo unaelekeza usuluhishi kufanywa nchini Uingereza kwa sheria zao," alisema Baha.

Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Mhandisi Emmanuel Kalobero, amekiri kuwepo kwa makubaliano hayo na kwamba kampuni hiyo ilifika wilayani hapo na kuliona eneo lenyewe.

Alisema baadaye iliwachukua baadhi ya maofisa wa wilaya na kuwapeleka Iowa, Marekani katika makao makuu ya kampuni.

 Aliwataja maofisa hao kuwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Rajab Rutenge, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Salum Chima, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda, Philip Kalyalya na makamu wake, , Sylvestre Swima.

Wengine waliopelekwa Iowa, Marekani ni  Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emmanuel Kalobero, Diwani na Mjumbe wa Kamati ya Fedha, Rose Malyalya, Diwani na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Teddy Nyambo, Mwanasheria wa halmashauri, Patrick Mwakyusa, Ofisa Kilimo, Fabian Kashindye na Haruna Mwalutanile.

Kwa mujibu wa Mwanasheria wa halmashauri ya  Mpanda, Patrick Mwakyusa, halmashauri ilipata agizo kutoka serikalini ya kuandaa maeneo kwa ajili ya uwekezaji,

"Februari mwaka 2010 tuliandikiwa kutoka mkoani tukiambiwa kuwa kuna mwekezaji (Agrisol) atakuja kuchukua maeneo ya makambi ya wakimbizi, maeneo hayo yalianza kukaliwa na wakimbizi mwaka 1972 . Sisi kama Halmashauri hatuma maamuzi na maeneo hayo, tunapokea maelekezo tu." alisema Mwakyusa.


Alisema mwaka 2010 kampuni hiyo ilikuja wilayani humo kuangalia ubora wa udongo na kufuatiwa na mazungumzo yaliylenga katika kufanya utafiti.

Alisema  mkataba rasmi utaingiwa Agosti mwaka huu na kwamba halmashauri itafaidika kwa kutumia sheria za ushuru wa ndani.
"Watakuwa wakilipa ushuru mara mbili kwa kila ekari ambapo ekari moja itakuwa kati ya  Sh500 na Sh700. Jamii zinazozunguka zitapata ajira, ujuzi na masoko ya bidhaa zao," alisema.

Kuhusu muda wa mkataba, Mwakyusa anakiri kuwa hiyo ni changamoto watakayoizungumza wakati wa kusaini mkataba.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Lauteri Kanoni, anakiri kuhusishwa kwenye mkataba huo na kwamba  kampuni hiyo inajitosheleza kufanya uwekezaji mkubwa katika kilimo na anapinga wafugaji kutoka mikoa mingine kuingiza mifugo wilayani humo kwa kuwa hawana utaratibu mzuri.

"Hatutaki kupokea mifugo kutoka nje ya mkoa huu, tumeshafanya sensa ya mifugo, iliyopo inatosha, eneo hilo tutawapa Agrisol kwa sababu wana uwezo wa kuliendeleza, siyo wafugaji wasio na utaratibu mzuri," alisema.

Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Rajab  Rutenge, alisema hana wasiwasi na wawekezaji hao kwa kuwa wataleta faida kubwa.
"Hatuna wasiwasi nao kwa sababu wataleta faida kubwa, mimi mtaalamu wa usalama wa chakula, Tanzania bado tuna uhaba wa chakula, tukiwaakila watu kama hao watakuja, watazalisha chakula cha kutosha kumaliza tatizo la njaa," alisema.

Akizungumzia mbegu zilizoboreshwa (GMO), Dk Rutenge alisema hilo pia si tatizo kwani tayari mazao hayo yalishaingizwa nchini tangu zamani
Wananchi hawakushirikishwa, wanapinga

Licha ya serikali kuupigia debe uwekezaji huo, wananchi wengi katika wilaya hiyo hawaelewi kinachoendelea, hata wale waliopata taarifa yake wanaupinga.

Mkuu wa kambi za wakimbizi za Katumba na Mishamo, Athuman Igwe, anautilia shaka uwekezaji huo kwa sababu mbili.

"Kwanza muda wa miaka 99 wanaopewa kumiliki ardhi yenyewe ni mrefu mno ni mkataba wa kikoloni, mambo yakiharibika itakuwa vigumu kujinasua, Pili, ardhi yenyewe imechoka sana. Labda watumie mbolea nyingi kuirutubisha au pengine kuna kitu wanakitafuta zaidi ya kilimo," alisema Igwe.

Diwani wa Litapunga yenye vijiji vya Kambuzi Holt, Litapunga na Ndui, Godfrey Lusambwa, alisema ataupinga mkataba huo kwa kuwa hakushirikishwa kama diwani.
Ofisa Kilimo wa kata hiyo, Righton Myombe alisema hawakuwahi kutangaziwa kuhusu uwekezaji katika eneo hilo.

mwananchi

No comments:

Post a Comment