Thursday, 2 February 2012

POSHO ZA WABUNGE TAYARI ZINALIWA

 
Spika wa Bunge Anne Makinda.
-Yasema wabunge waliachiwa wapime
-Spika Makinda asema zilipata baraka
WAKATI Spika wa Bunge Anne Makinda, akithibitisha kuanza kulipwa posho mpya za Sh. 200,000 kwa kila kikao cha Bunge baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa kibali; Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imekana kuidhinisha viwango hivyo.
Taarifa fupi ya Kurugenzi hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kwamba “Rais Kikwete anakubali haja ya kuangalia upya posho kwa wabunge, lakini amewataka wabunge kutumia hekima na busara katika kulitafakari suala hili.”
Taarifa hiyo iliyolenga kueleza maelekezo ya Rais kuhusu posho za wabunge ilisema aliwataka wabunge kutumia Mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma hivi sasa “kulizungumza upya suala hilo.”
Ikiwa huo ndio msimamo wa Ikulu, Makinda aliwahakikishia waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu kwamba wabunge wamekwishaanza kulipwa posho mpya.
“Sio kwamba tutaanza kutoa, tulishaanza kutoa na Rais (Jakaya Kikwete), ameshatoa kibali chake na mbunge atalipwa katika vikao tu, si kila siku na tena baada ya kukaa kwenye vikao na kusaini,” alisema.

Alisema posho hiyo iko katika waraka wa serikali kuhusu posho uliotolewa Julai mwaka jana. Kutokana na waraka huo, wenyeviti wanapata Sh. 200,000, wajumbe ni Sh 150,000 na wengine Sh. 100,000.

Alisema mtu mwingine akipata mshahara unakuwa wake na familia yake, lakini kwa mbunge si hivyo kwa kuwa kuna watu wengi ambao wamekuwa wakihitaji misaada yao
.

“Wabunge wengine wanaondoka na mshahara wa Sh. 45,000 kwa mwezi wengine Sh. 100,000, wanachopata ni kidogo sana kwa kwa sababu utendaji wake wa kazi ni mgumu,” alisema.

Makinda aliyekuwa ameongozana na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah pamoja na maofisa wengine wa Bunge, alisema wabunge wengine wamekuwa wanakopa hadi mafuta ya kwenda bungeni na kwamba si matajiri kama wengine wanavyosema.

Alisema wapo wabunge wengine ambao hufariki dunia muda mfupi mara baada ya kumaliza kipindi chao cha ubunge, “Anamaliza ubunge Februari anakufa, kiinua mkongo chake (gratuity) ameshakopa leo ikifika mwaka 2015 hana kitu.”

Alisema hali hiyo inatia uchungu sana na kwamba hawana la kufanya kuhusiana na jambo hilo na badala yake wanafanya kazi.

Mbali ya posho, kwa mwezi mbunge analipwa mshahara wa Sh. milioni 2.3 na akikatwa kodi anabakiwa na Sh. milioni 1.7 ambazo pia hukatwa mkopo anaokuwa amekopa benki ukiwemo ule wa gari.

Vyanzo vya habari kutoka kwa wabunge vinasema kuwa wabunge wana mlolongo wa madeni ambayo hutokana na maamuzi yao ya kukopa fedha nyingi kutoka taasisi za fedha.

“Wapo waliokopa hadi Sh. milioni 200 mzee, si unajua tena mkutano wa kwanza wa Bunge ukianza tu mabenki nayo hayalazi damu, wanashawishi wabunge wanakopa. Sasa ukikopa halafu hukuwekeza si unajua fedha inavyoteketea, ununue gari la kifahari na mbwembwe nyingine, mara ulipe madeni ya kampeni, yaani baada ya miezi minne huna kitu,” alisema mbunge mmoja aliyeomba jina lake lisitajwe kwa kile alichosema suala la posho kwa sasa ni nyeti mno katika korido za Bunge.

Naye mbunge machachari wa Kigoma Kusini (NCCR), David Kafulila, ambaye yuko kwenye mzozo na chama chake kilichomfukuza uanachama, alisema kinachosumbua kwa sasa ni kukosekana kwa mfumo wenye usawa wa ulipaji mishahara na posho ndani ya serikali.

Kafulila alisema ni aibu kuona daktari akilipwa mshahara wa Sh. 900,000, lakini wapo maofisa wadogo tu katika mashirika ya umma kama Benki Kuu (BoT) au Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanachota hadi milioni saba kwa mwezi.

“Angalia Gavana wa Benki Kuu analipwa mshahara wa Sh. milioni 20, Mkurugenzi wa NSSF Sh. milioni 18, mbunge Sh. milioni 1.8, daktari Sh. 900,000,” alisema na kuhoji hapa haki iko wapi.

Aliongeza kwamba waziri akisafiri nje ya nchi posho yake kwa siku ni Dola za Marekani 420 (sawa na Sh. 672,000) lakini Mkurugenzi wa Mkuu wa Shirika lililo chini yake anachota Dola za Marekani 800 (Sh. 1,280,000) kwa siku.

Kuna watumishi wa umma wako hoi sana, walimu, mahakimu na hata ndani ya serikali wapo wasiojua kesho watakula nini: “Tatizo ni la kimfumo zaidi, tunahitaji kuufumua na kuusuka upya. Hii ndiyo njia pekee ya kutibu matatizo haya.”

chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment