Sunday, 26 February 2012

TAIFA LIMEKOSA VIONGOZI-WARIOBA

na Irene Mark
WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema taifa linakabiliwa na upungufu wa wataalamu na viongozi wenye maadili.

Kwa sababu hiyo amelitaka Kanisa Katoliki lisiogope wala kuyumbishwa na vitisho, lakini akasihi liepuke hisia mbaya kutoka kwa watu zinazoweza kuwaingiza kwenye migogoro isiyo na tija.

Jaji Warioba alisema hayo wakati wa mahafali ya kwanza ya Sekondari ya Mtakatifu Joseph Dar es Salaam jana na kuwataka wahitimu hao kuwa mfano wa kuigwa kwenye jamii.

Akizungumza kwa kutumia mfano wa Musa kutoka kwenye Biblia Takatifu, alizitaja sifa za viongozi bora kuwa ni uaminifu, ucha Mungu, mwenye uwezo kiutendaji, mpinga rushwa na ufisadi.

“Mussa aliambiwa ateue watu wenye uwezo, wacha Mungu, waaminifu na wanaochukia rushwa, wewe kuwa kiungo kati yao na Mungu… Musa akafanya hivyo na ndio mfumo tulionao hadi sasa kwenye ngazi ya kijiji, kitongoji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa,” alisema.

Hata hivyo, alisema viongozi wengi ambao walitegemewa kuongoza kama wale walioteuliwa na Musa wameacha wajibu huo na wanatenda kinyume kabisa, na kila ngazi sasa hakuna uwajibikaji wa pamoja, badala yake kuna kile alichokiita ‘sumu ya uongozi’.

Aliongeza kuwa taifa linaelemewa na ukosefu wa uongozi bora, hivyo akawataka wahitimu hao kuishi kulingana na yale waliyofundishwa wakiwa shuleni.

“Haya mliyofundishwa hapa muyazingatie kwa sababu mnaingia katika jamii ambayo ina upungufu wa maadili,” alisema.

Alilitaka Kanisa Katoliki nchini na madhehebu mbalimbali ya dini kutoogopa vitisho wanapokemea maovu.

“Endeleeni kukemea maovu na kutupa mwongozo… msije mkaogopa vitisho visivyo na msingi, msiogope kabisa mkatishwa mkarudi nyuma.

“Muepuke hisia zozote mbaya kwenu zinazolenga kuwaingiza kwenye migogoro isiyo na tija, kazi hiyo mmeifanya vizuri naomba muendelee,” alisema jaji huyo aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, ambapo wanafunzi 163 walihitimu kidato cha sita.

Aidha, alilipongeza kanisa hilo kwa kazi linazofanya upande wa elimu na kusema shule zilizopo chini ya kanisa hilo zinaingia kwenye kundi la shule bora kila mwaka, kwa sababu linawalea watoto kwa nidhamu na maadili bora.

Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa, aliwataka wahitimu hao wawe na hofu ya Mungu katika maisha na uongozi wao kwenye jamii.

Askofu huyo alisema wahitimu hao ni viongozi bora wa baadaye katika jamii, hivyo kuwataka watumie elimu yao kupinga rushwa na ufisadi.

“Viongozi wanaweza kuiangusha au kuiongoza vema nchi, ninyi mkawe viongozi bora, mshirikisheni Mungu katika uongozi wenu na maisha yenu ya kila siku,” alisema na kuliomba taifa kuendeleza amani na utulivu uliopo.

Naye Mkuu wa shule hiyo, Sista Theodora Faustine aliishukuru serikali kwa kuirejesha shule kwenye umiliki wa kanisa huku akieleza changamoto inayowakabili kuwa ni bweni la wanafunzi.

Katika hilo alibainisha kwamba kiwanja cha ujenzi wa bweni hilo kipo nyuma ya Kanisa la Mtakatifu Peter Oysterbay, ambapo gharama za ujenzi hadi kukamilika kwake ni sh bilioni 3.9 huku akieleza kwamba hivi sasa wanafunzi 337 waliopo shuleni hapo wanaishi kwenye hosteli.
 

No comments:

Post a Comment