Friday, 24 February 2012

UPENDO KILAHIRO KUFANYA MAKUBWA KWENYE TAAMASHA LA PASAKA


* Sasa anatamba na albamu mpya ya Ficho Langu

Na Mwandishi Wetu

TAMASHA la Pasaka linalotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8 na 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, limepangwa kusheheni waimbaji kochokocho wa nyimbo za injili.
Miongoni mwa wasanii hao ni mwimbaji galacha wa nyimbo za injili, Upendo Kilahiro ambaye anasema amepania kukonga nyoyo za mashabiki atakapopanda jukwaani katika tamasha hilo lililoliandaliwa kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama anasema tamasha hilo la Sikukuu ya Pasaka litasindikizwa na wasanii kochokocho wa muziki wa injili.
"Kilahiro tutakuwa naye kwenye tamasha, na naamini kwamba mwaka huu tamasha hili litakuwa bora zaidi kutokana na kushirikisha waimbaji wengi wakali," anasema Msama.
Katika mahojiano maalumu Dar es Salaam, Kilahiro anasema amepania kufanya mambo makubwa katika tamasha la mwaka huu, na atapanda jukwaani kuimba 'live' na bendi yake ya Upendo Kilahiro.
"Natoa mwito kwa mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi, watarajie kupata vitu vizuri na tofauti zaidi... watapata vitu vinono kwa vile tamasha hili linazidi kuwa bora zaidi.
"Sikukuu ya Pasaka ni upatanisho kutokana na kifo cha Yesu Kristo aliyefia msalabani na kufufuka siku ya tatu... tutaienzi sikukuu hiyo kwa nderemo," alisema Upendo.
Kilahiro anasema amepania kufanya mambo makubwa kuliko yale aliyofanya katika matamasha yaliyopita ya Sikukuu kama hiyo ambayo ni upatanisho kutokana na kifo cha Yesu Kristo aliyefia msalabani na kufufuka siku ya tatu.
Mwanamuziki huyo anayeabudu katika Kanisa la BCIC lililoko Mbezi Beach, Dar es Salaam (Kwa Askofu Gamanywa), anasema amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na mbali na kufanya mazoezi, pia atafunga na kusali ili Mungu amfanyie miujiza.
Anawaomba mashabiki wamiminike kwa wingi uwanjani Aprili 8 na 9 kuona mambo mazuri aliyowaandalia na kuongeza kuwa kwa vile anamtukuza Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya Shetani, anaamini atawapa kile wanachotaka kutoka kwakwe.
Anasema anatarajia kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo zilizotamba za Zindonga (alioimba kwa Kizulu), Unajibu Maombi na Ni Salama Rohoni. Kilahiro hivi sasa anatamba na albamu yake mpya ya Ficho Langu aliyoirekodi nchini Canada.
Msama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, anasema wamewaandalia mashabiki wa muziki wa injili mambo mazuri yatakayowaburudisha na kuridhika.
Msama anajinaki (jinasibu) kuwa tamasha hilo litafana kwa vile kutakuwa na waimbaji wengi wa muziki wa injili watakaowapa mashabiki vionjo mbalimbali. Anasema pia watakuwepo wageni waalikwa.
Wasanii wengine wa nyimbo za Injili watakaopamba tamasha hilo wanatarajiwa kutangazwa wakati wowote wakiwamo waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi kadhaa za Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.
"Kuna orodha ya waimbaji wa nyimbo za injili wapatao wanane ambao tunafanya nao mazungumzo na wengine bado tunaendelea, lakini tutatangaza mmoja baada ya mwingine tunapokamilisha mazungumzo," anasema Msama.
Mkurugenzi huyo anasema Kilahiro amekuwa wa kwanza kuthibitisha kushiriki katika tamasha la Pasaka litakalofanyika Dar es Salaam, na pia kurindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma Aprili 9.

No comments:

Post a Comment