Wednesday, 18 April 2012
DAWASCO YAWATOA WANANCHI WASIWASI JUU YA UBORA MAJI
KAMPUNI ya Maji safi na Maji Taka Dar es salaam(DAWASCO), imewataka wananchi kutokuwa na shaka ya aina yoyote juu ya ubora wa maji yake kwa madai kuwa yana usalama wa kiwango cha kimataifa.
Hatua hiyo ya Dawasco inakuja siku chache baada ya Naibu Waziri wa Maji Greyson Lwenge, kutoa kauli ya aina hiyo wakati akiliambia Bunge kufuatia swali lililoulizwa na Mbunge wa Ubungo John Mnyika, aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali juu ya maji ya Dawasco.
Aidha akizungumza jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco John Midala, alisema kimsingi kazi inayofanywa na kampuni hiyo ni kuhakikisha wanatoa huduma ya maji safi na salama kwa kila mtumiaji ili kulinda afya zao na kwamba taarifa zinazodai kuwa maji hayo ni salama ni uzushi.
Kwa mujibu wa midala, Dawasco imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyanzo vyake vya maji sambamba na kuyatia dawa iliyothibitishwa kuwa ubora wake unastahili kwa matumizi ya binadamu aliyodai kuwa imekuwa ikitumika tangu kipindi kirefu kilichopita.
Alisema kwa kawaida kabla maji hayo hayajasambazwa kwa watumiaji, mbali na kutiwa dawa hiyo, pia hupitia hatua mbalimbali ya kuyasafisha kwa lengo la kuondoa taka zote zinazokuwepo pindi yanapotoka katika vyanzo vya awali vya uzalishaji.
“Hivyo napenda niendee kuungana na Serikali kuwajulisha wananchi wote kuwa maji yetu ni salama, tena kwa ubora wa kimataifa, wasiogopeshwe na taarifa za kizushi zilizowahi kutolewa kuwa maji siyo salama” aliongeza Midala.
Katika hatua nyingine Midala alisema kampuni hiyo inaendelea na uboreshaji wa miundombinu yake ya mabomba katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam kwa lengo la kuhakikisha wanawaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa maji.
Alisema mbali na uboreshaji huo pia wameanzisha idara maalumu inayoshughulikia upotevu wa maji kwa kuunda vikosi kazi vinavyofanya ukaguzi mara kwa mara kwenye mtandao wa mabomba na kufanya matengenezo yanayostahili ili kupunguza kiwango cha maji kinachopotea.
source:fullshangwe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment