Wednesday, 18 April 2012

UTATA ZAIDI KIFO CHA KANUMBA NA MALI ALIZOACHA


JANA Kamati ya Mazishi ya Steven Charles Kanumba ilisema kuwa, mwigizaji huyo ameacha viwanja viwili na magari matatu, zaidi ya hapo hakuwa na lolote.
Sababu za Kamati hiyo kutoa maelezo hayo ni kufuatia taarifa za vyombo vya habari kwamba wamechakachua fedha za michango ya mazishi.
Mapema jana, vyombo vya habari viliripoti kutokana na vyanzo vya familia ya marehemu, kwamba Kamati hiyo imechakachua fedha za michango.
Lakini pamoja na kutoa taarifa isiyojitosheleza kuhusu taarifa za michango na matumizi yake, ajabu Kamati hiyo iliingilia wajibu ambao si wao kuzungumzia mali za marehemu.
Wajibu wao ulikuwa kuzungumzia tuhuma zao za uchakachuaji michango na mambo mengine, wakiiachia familia ya marehemu kama ingeona umuhimu wa kufanya hivyo.
Lakini kwa kuwa wamekwishasema- hatuna budi kufungua mjadala katika hili.
Wanasema Kanumba ameacha viwanja viwili na magari matatu, maana yake amekufa masikini, je, hizo ndizo mali pekee za marehemu?
Umauti unamkuta Kanumba akiwa ana filamu mbili zilizokamilika, moja ikiwa mbioni kuingia sokoni na nyingine ikiwa inafanyiwa uhariri.
Kanumba alikuwa na kampuni yake - Kanumba The Great - ambayo ilikuwa inasimamia kazi zake na alikuwa ameajiri watu wasipungua sita, akiwemo Mayasa Mrisho na Sethi Bosco.
Je, kampuni hii si sehemu ya mali za marehemu na kampuni hii ina thamani gani, akaunti zake zina fedha kiasi gani.
Kampuni inadai na kudaiwa kiasi gani cha fedha?
Kanumba pia alikuwa ana akaunti binafsi mbali za kampuni yake, je, ameziacha na shilingi ngapi?
Kampuni ya Steps Entertainment Limited ndiyo ilikuwa na itaendelea kuuza filamu za Kanumba, je, haikuwa na deni la marehemu, moja.
Pili, utaratibu wa muda mrefu wa Steps Entertainment ni kulipa kwa awamu – je, kweli Kanumba alikuwa amekwishalipwa fedha zake zote na kampuni na kama alikuwa anadai nini kinafuata?
Bado watu wangependa kujua mikataba mingine ya Kanumba, kama matangazo ya biashara aliyokuwa akifanya, Zantel, Oxfam na Star Times, hana anachodai huko?
Ukimtazama mama yake Kanumba, Florence Mtegoa, mwenye umri wa miaka 55, unaweza kupata jibu kwamba asiposhikwa mkono na kuelekezwa kuhusu thamani ya marehemu mwanawe, atapoteza sana.
Mama Afeni Shakur, mama wa Tupac hadi kesho anakula jasho la mwanawe huyo aliyekuwa nyota wa muziki wa Hip hop, kwa sababu tu alisimama kidete na alikuwa anajua.
Nani atamsaidia mama Kanumba kusimamia haki za mwanae- mali zilizoachwa na mwanae na kadhalika?
Tutarajie baada ya kifo chake, Kanumba filamu zake zitakuwa zinanunuliwa sana na kama hivyo watu wamekwishaanza kutoa vitabu, DVD, za historia yake na kadhalika – je, mama huyo akiwa mrithi halali wa mali za marehemu atasaidiwa na nani katika hilo?
Ikiwa katika Sh. Milioni 53. 2 zilizopatikana kutokana na michango ya msiba, yeye aliambulia Sh. Milioni 4 tu?
Kamati ya Mazishi ya Kanumba ilikuwa inaundwa na Mwenyekiti Gabriel Mtitu, Makamu Mwenyekiti, Jacob Steven ‘JB’, Katibu, William Mtitu na Wajumbe Issa Mussa ‘Cloud’ (Mweka Hazina), Kimosa na Vincent Kigosi ‘Ray’.
Wengine ni Single Mtambalike ‘Richie’, Dilesh Solanki, Millenne Happiness Magesse, Adele Kanumba (dada wa marehemu), Hartman Mblinyi, Ruge Mutahaba, Ally Choky, Simon Mwakifamba, Eric Shigongo, Steve Nyerere, Mahsein Awadh ‘Dk Cheni’ na Mama Nassor, mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi Kanumba

chanzo:bongostarsblog

No comments:

Post a Comment