Saturday, 21 April 2012

MAWAZIRI NANE KUACHIA NGAZI

Friday, 20 April 2012 22:32
0digg
Pinda awaambia waandike barua za kujiuzulu mara moja, ni baada ya wabunge 73 kusaini kumng'oa madarakani
Waandishi Wetu, Dodoma
MAWAZIRI nane wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wanatarajiwa kujiuzulu baada ya wabunge kumkalia kooni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu ripoti chafu ya ubadhirifu wa fedha za umma zilizowasilishwa na wenyeviti wa kamati za tatu za Bunge.

Taarifa za ndani zilizopatikana baada ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika jana usiku, zilieza kuwa wabunge wa chama hicho wameagiza mawaziri nane wajiuzulu kutokana na kushindwa kufanya kazi zao kikamilifu.

Mawaziri waliotajwa ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali  za Mitaa(Tamisemi), George Mkuchika, Waziri wa Maliasili na Utalii,Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda.

Wengine waliotajwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu.

Baada ya kikao hicho Katibu wa wabunge wa CCM, Jenista Mhagama aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kwamba maamuzi yaliyofikiwa katika kikao cha wabunge wa CCM juzi na jana yatatolewa na Mwenyekiti wa wabunge wa CCM ambaye ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Hata hivyo, Mhagama  hakutaja uamuzi huo huku akisisitiza kuwa anayestahili kusema ni Waziri Mkuu.

"Wabunge wa CCM wamefanya kazi yao na waliyoyasema wameyafanyia kazi na Pinda atatangaza kuhusu hayo maamuzi magumu yaliyofikiwa," alisema Mhagama.

Vyanzo vya ndani ya kikao hicho vilimnukuu Pinda akiwataarifu wabunge kwamba mawaziri nane wametakiwa kuandika barua za kuachia nafasi zao ifikapo leo asubuhi.
Kama mawaziri hao watajiuzulu itakuwa mara pili kwa Serikali ya Awamu ya Nne mawaziri kuachia ngazi kwa shinikizo la Bunge.

Daniel Mjema, Dodoma, Geofrey Nyang'oro Dar
MKAKATI wa kukusanya majina 70 ya wabunge kama sehemu ya kukamilisha utaratibu wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, umepamba moto na hadi kufikia jana jioni, wabunge 75 walikuwa wameunga mkono hatua hiyo, watano kati yao, wakitokea chama tawala CCM.


Endapo mchakato huo utakamilika, Pinda atakuwa ameingia katika historia ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Bunge, tangu Tanzania ipate uhuru wake Desemba 9, 1961


Hata hivyo wakati mchakato huo ukiendelea, Spika wa Bunge, Anne Makinda jana jioni aliibuka bungeni na kueleza kuwa mchakato huo ni batili.


Akinukuu vifungu vya Kanuni za Bunge na Katiba, Spika Makinda alisema mkakati huo ni batili kwa kuwa kanuni zinaeleza bayana kuwa ulipaswa kufanyika siku 14 kabla ya kuwasilisha hoja hiyo kwa Spika.

"Bunge letu linaisha Jumatatu ambayo ni siku nne tu tangu leo (jana) na kwa mujibu wa kanuni, taarifa ya maandishi iliyotiwa saini na kuungwa na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote, itatolewa kwa Spika siku angalau 14 kabla ya siku inapokusudiwa kuwasilishwa bungeni."

Spika Makinda alisema pamoja na hayo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliyeongoza mchakato wa kukusanya saini hizo za wabunge, alikuwa sahihi kuendesha mpango huo kwa mujibu wa Kanuni ya 133 ya Bunge na Ibara ya 53 (3)ya Katiba.

Akizungumza na gazeti hili, Zitto alipingana na maelezo hayo ya Spika akidai kuwa aliyatoa kwa lengo la kutetea Serikali ya chama chake kwa kupindisha sheria.

"Spika hajasema kitu, wamejipanga tu hawa (CCM). Sisi hatujampelekea hoja yetu. Tunampelekea Jumatatu kisha ataamua. Ili mradi iwe siku 14 kabla ya siku ya kutoa hoja. Wanaweweseka tu," alidai Zitto.

Alifafanua; "Kanuni inasema siku 14 kabla, sisi tunakusanya saini ili tutimize sharti la kanuni. Spika anajaribu kulindaa Serikali ya chama chake kwa kupindisha kanuni."

Kanuni zinasemaje

Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, kipengele cha 133 (4) na (5) kuhusu hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kinaeleza:

"Hoja inayotolewa chini ya kanuni hii na iliyotimiza masharti ya katiba itawasilishwa bungeni mapema iwezekanavyo na itaamuliwa kwa kura za siri."

Kifungu cha tano kinasema kuwa hoja hiyo itapitishwa tu pale itakapoungwa na wabunge wengi.

kanuni hizo za Bunge zinafafanua katika kifungu cha sita kuwa kama wabunge watapitisha hoja, itambidi Spika kuwasilisha azimio hilo kwa rais mapema iwezekanavyo.

Kifungu hicho kinafafanua kwamba kwa namna yoyote ile ndani ya siku mbili, Waziri Mkuu atakuwa amejiuzulu na Rais kumteua mbunge mwingine kushika nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Katiba, mpango wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inafafanuliwa na Ibara ya 53.

Kwenye ibara hiyo kifungu kidogo cha tatu kinatoa masharti ambayo wabunge wanapaswa kuyakamilisha ili kutekeleza azma yao ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Ibara ya 53(3)a, kinasema taarifa ya maandishi iliyotiliwa saini na wabunge wasiopungua asilimia 20 itawasilishwa kwa Spika wa Bunge siku angalau 14 kabla ya siku inapokusudiwa kuwasilishwa bungeni.

Zitto akusanya maoni

Jana Zitto alianza kutekeleza azma yake ya kuwasilisha hoja binafsi bungeni ya kutokuwa na imani na Pinda kwa kukusanya saini za wabunge hadi kufikia jioni tayari alikuwa na wabunge 75 wakiwamo watano kutoka CCM.

Wabunge wa CCM waliotia saini hoja hiyo na kufanya idadi hiyo kufikia 62 ni Deo Philikunjombe wa Ludewa, Ally Keissy Mohamed wa Nkasi Kaskazini, Alphaxard Kange Lugola wa Jimbo la Bunda, Murtaza Ally Mangungu na mbunge mmoja wa Viti Maalumu kutoka Kanda ya Ziwa ambaye hakutaka atajwe kwa sasa.

Zitto alisema akikamilisha idadi inayotakiwa, atawasilisha hoja binafsi ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Pinda bungeni Jumatatu kutokana na kiongozi huyo wa shughuli za Serikali kushindwa kuwawajibisha mawaziri wazembe na mafisadi.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema zoezi hilo si la chama chochote cha siasa bali wabunge wote wanaoitakia mema Tanzania na watu wake.

Zitto, alisema amearifiwa na Katibu wa Wabunge wa CUF, Magdalena Sakaya kwamba makao makuu ya chama hicho yameelekeza wabunge wake wote watie saini kuunga mkono hoja hiyo.

“Hili suala limekuwa sasa ni la karibu  Bunge zima kwa sababu vyama vyote wabunge wake au wawakilishi wao wametia saini isipokuwa UDP tu,” alisema Zitto.

Aliwataka Watanzania na wabunge wasichukulie kuwa hoja hiyo ni ya kambi ya upinzani au ya Zitto kwani wabunge wengi waliopaza sauti walikuwa ni wa CCM.

“Hii ni hatua ambayo tunaifanya ili tuondoke kwenye Bunge la kulalamika kwenda kwenye Bunge la kutenda ndio nia hasa na si vinginevyo,” alisisitiza Zitto.

Aliongeza, "Kuna wengine wamesema;  ooh! Waziri Mkuu hana makosa! Tunamuonea lakini tunataka tuwaambie ujumbe mmoja kuwa tunamheshimu sana Waziri Mkuu, tunampenda sana Waziri Mkuu lakini tunaiheshimu zaidi nchi yetu.”

Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema kama mawaziri waliotajwa hawatawajibika, ‘watalia’ na Waziri Mkuu Pinda.

Alisema wamempa Waziri Mkuu muda wa hadi Jumatatu ili mawaziri wake wajipime na kujiuzulu vinginevyo watawasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye.

Mawaziri wanatakiwa kujiuzulu ni Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika na  Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na naibu wake, Lazaro Nyalandu.

“Tunataka kupiga kura hii ili mawaziri waliotajwa ama wizara zao, mashirika yaliyo chini yao au Halmashauri ziwajibike… Tunataka Bunge lionyeshe makali yake halisi,” alisema.

Zitto alisema kama watamaliza Bunge hilo bila kuwawajibisha mawaziri waliotajwa, wananchi watalidharau. Alisema wanachofanya sasa ni kulinda heshima yao kwani bila watendaji kuwajibika, madudu yataendelea.

Zoezi la kukusanya saini hizo lilianza jana saa 3:00 asubuhi nje ya lango kuu la kuingia ukumbi wa Bunge na ilipotimu saa 8:24 mchana, wabunge 62 walikuwa wametia saini.

Mbunge Deo Filikunjombe, alisema kuna  mawaziri wanaodai kuwa anashinikiza waondolewe kwa sababu anataka uwaziri lakini alisema anamuomba Rais atakapofikia kulivunja Baraza lake la Mawaziri, asimteue kamwe kuwa waziri.

“Waziri Mkuu ndiye mshauri mkuu wa Rais, namuomba amshauri Rais asiniteue kuwa waziri kwa sababu sikuomba uwaziri mimi nimeomba ubunge,” alisema.

Alisema jana asubuhi alipata ujumbe kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi kuwa alikuwa anatakiwa kuonana na Waziri Mkuu.

Hata hivyo alisema kwa kuwa alijua anachoitiwa, aliona ni vyema atie saini yake kwanza kwenye hoja hiyo ili kuepuka ushawishi ambao ungemfanya abadili mawazo yake.

Habari zaidi zilidai kuwa Serikali kupitia kwa baadhi ya wabunge, maswahiba na mawaziri, jana walikuwa na kazi ya ziada kuwashawishi wabunge wa CCM wasisaini.

Nje ya viwanja vya Bunge, mawaziri na baadhi ya wabunge watiifu kwa Waziri Mkuu, walionekana wakihaha kila kona kujaribu kushawishi wabunge wasiikubali kusaini.

Mbali na wabunge wa Chadema, wengine wa kambi ya upinzani waliotia saini hoja hiyo ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya TLP, Augustino Mrema.

Baadhi ya wabunge wengine waliotia saini hoja hiyo ni Moses Machali (NCCR-Mageuzi) na wabunge 11 wa CUF wakiongozwa Mbunge wa Morogoro, Magdalena Sakaya.

Waunga mkono

Watu kadhaa jana walisema kuwa wanaunga mkono uamuzi wa wabunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Pinda, huku wakihimiza wawakilishi hao wa wananchi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono mchakato huo.

Askofu Msaidizi Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba Methodius Kilani alisema ni wakati mwafaka kwa viongozi na watendaji wanaotuhumiwa kuwajibika wenyewe bila kusubiri shinikizo.

Askofu Kilaini, alisema kitendo cha viongozi na watendaji serikalini wanaotuhumiwa kusubiri shinikizo la  kutakiwa kujiuzulu siyo jambo jema hasa katika nchi inayoongozwa kwa utawala wa sheria na misingi ya kidemokrasia.

"Bunge linatekeleza wajibu wake kwa niaba ya wananchi. Hii ni sehemu muhimu ya kazi zake. Pia kuna njia mbalimbali za Bunge kutumia katika kuiwajibisha Serikali. Hii ni moja wapo lakini siyo njia bora zaidi katika kuleta mabadiliko," alisema Kilaini.

Alifafanua kuwa njia sahihi ni ile ya wahusika wenyewe kulazimika kujiuzulu pasipo kulazimishwa.

Askofu Kilaini ambaye katika maelezo yake alionyesha hofu kama njia hiyo inayotumiwa na wabunge kushinikiza mawaziri walioshindwa kuwajibika kujiuzulu kama itafanikiwa. Alipongeza Bunge kufikia hatua hiyo akisema ni moja ya hatua muhimu zenye lengo la kuleta mabadiliko.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Deus Kibamba, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhimiza uwajibikaji ikiwa inafuata taratibu walizojiwekea.

"Zipo kanuni zinazotoa mamlaka kwa Bunge kuchukua hatua dhidi ya viongozi serikalini ambao uwajibikaji wao unazidi kushuka. Hii ni hatua muhimu katika kuhimiza utendaji serikalini na itachochea uwajibikaji," alisema Kibamba.

Kwa upanda wake, Profesa Idris Kikula wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alisema ni vema Watanzania wakasubiri kwanza na kuona kitakachofanyika, ili waweze kujadili.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Rodrick Kabangila aliunga mkono hatua hiyo akisema itaamsha ari ya uwajibikaji serikalini, hususani kwa mawaziri watakaoteuliwa kushika nyadhifa hizo baada ya Baraza la sasa kuvunjwa.

Moto wa kutaka kuwajibishwa kwa mawaziri watano ulitokana na ripoti ya CAG kuainisha ulaji wa kutisha serikalini.

Baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo, wenyeviti wa kamati tatu; Hesabu za Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, nao waliwasha moto ambapo moja ya mapendekezo ya yao ni kuwajibishwa kwa mawaziri hao.

Moto ulikolezwa zaidi na wabunge waliochangia taarifa hizo huku  wabunge wengi wa CCM wakiwasulubu mawaziri hao na baadaye Waziri Mkuu kuguswa kutokana na kwamba ndiye  Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali bungeni.

Katika kujaribu kupunguza makali ya wabunge hao, wabunge wa CCM walikutana kwa faragha Ukumbi wa Pius Msekwa lakini mambo yalizidi kuharibika na kutaka mawaziri hao wajiuzulu.

Wabunge hao walishikilia msimamo kuwa kama mawaziri hao hawatajiuzulu, wangepiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa vile kikatiba, hawana mamlaka ya kuwawajibisha mawaziri hao isipokuwa Waziri Mkuu.

Akifanya majumuisho ya kamati yake Zitto aliyepigilia msumari wa mwisho alipowataka wabunge kukusanya saini za wabunge 70 ili kupata uhalali wa kikanuni wa kumpigia Waziri Mkuu kura ya kutokuwa na imani .

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment