|
Neville Meena AHADI
iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete ya kupatikana kwa megawati 3,000 za
umeme huenda isitekelezwe katika muda uliopangwa kutokana na kutofanyika
kwa maandalizi ya kutosha.Akilihutubia Taifa kuukaribisha mwaka 2012,
Rais Kikwete alisema tatizo la umeme nchini litakuwa historia katika
muda wa miezi 18 ijayo kutokana na mpango wa Serikali wa kusafirisha
gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
“Maombi yetu kwa Serikali
ya China ya kupata mkopo wa kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka
Mtwara na mtambo wa kuchakata gesi inayotoka Songosongo yamekubaliwa,”
alisema Kikwete katika hotuba yake ya Desemba 31, mwaka jana na
kuongeza:“Utekelezaji wake unatarajiwa kuchukua miezi 18 na gesi
itakayoletwa inaweza kuzalisha mpaka Megawati 3,000 za umeme. Baada ya
hapo kasi ya kuongeza umeme itakuwa kubwa zaidi na tatizo la upungufu wa
umeme linaweza kuwa historia.
”Hata hivyo, imebainika kuwa hadi
sasa Serikali ya Tanzania na China hazijasaini mkataba wa kifedha ili
kupata mkopo wa Dola bilioni moja za Marekani (karibu Sh1.6 trilioni)
ambazo zitatumika kugharamia ujenzi wa bomba hilo, hivyo kuzua wasiwasi
iwapo ujenzi wa bomba hilo utakamilika katika muda
uliopangwa.Makubaliano ya awali ya ujenzi wa bomba hilo yalisainiwa
China Septemba 26, 2011 na Tanzania ikiwakilishwa na Waziri wa Nishati
na Madini, William Ngeleja.
Baadaye ilisainiwa mikataba mingine
midogomidogo lakini, kikwazo hadi sasa ni mkataba wa fedha.Waziri wa
Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema hadi mwishoni mwa wiki jana,
mkataba wa kifedha ulikuwa bado haujasainiwa lakini akasema taarifa
alizonazo ni kwamba utasainiwa hivi karibuni.“Kweli bado hatujasaini
mkataba huo ila niko informed (nina taarifa) kwamba majadiliano yako
kwenye hatua nzuri na yakikamilika tutasaini,” alisema Mkulo.
Mkulo
alisema majadiliano yanayoendelea yanawahusisha Makatibu Wakuu wa
Wizara za Fedha na Uchumi, Nishati na Madini, maofisa wa Serikali ya
China na wakala wa utekelezaji wa mradi huo kutoka nchi hizo
mbili.“Ninachoweza kusema ni kwamba bado tuko kwenye ratiba, tunafahamu
umuhimu wa kukamilika kwa hatua hii, lakini lazima tujiridhishe.”Mapema
wiki iliyopita, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Servacius
Likwelile alisema bado kuna maeneo machache ya majadiliano baina ya
wataalamu wa Tanzania na China na kwamba yakikamilika mkataba huo wa
kifedha utasainiwa.
“Ahadi ya Rais itatekelezwa kama alivyosema,
kuna sehemu chache tu bado wataalamu wetu wanajadiliana na wenzetu wa
China, wakikamilisha basi nadhani tutaweza kusaini ili kuwezesha mradi
huo kuanza,” alisema Dk Likwelile.Kwa upande wake, Ngeleja alisema
wizara yake imejipanga kusimamia kikamilifu ujenzi wa bomba hilo, baada
ya mkataba wa fedha kusainiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini, January Makamba katika maoni yake alisema kuchelewa
kusainiwa kwa mkataba wa kifedha kunaweza kuathiri kasi ya utekelezaji
wa mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara.“Ni vigumu sana kuwa na uhakika
wa kutekelezwa kwa mradi kabla ya kuwa na uhakika wa fedha, sina uhakika
kama hilo limefanyika lakini kwa kuwa tunaanza vikao vya kazi zetu
karibuni, nadhani tutapata taarifa,” alisema January.Vikwazo
vingineWakati Serikali ikihaha kukamilisha mchakato wa kusainiwa kwa
mkataba wa fedha, habari kutoka ndani ya Serikali na Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) zinasema kinahitajika kiasi kikubwa cha fedha kwa
ajili ya kujenga vituo vya kusambaza umeme na njia mpya za kusambaza
umeme huyo.
Mmoja wa wahandisi ndani ya Tanesco ambaye aliomba
jina lake lihifadhiwe alisema ikiwa kiasi hicho cha megawati 3,000 za
umeme kitafikishwa Dar es Salaam basi vinahitajika vituo 30 kwa ajili ya
kusambaza umeme.“Ujenzi wa kituo kimoja (sub-station) gharama zake si
chini ya Dola za Marekani milioni 15 (zaidi ya Sh23 bilioni) kwa hiyo
piga hesabu kama tunahitaji vituo 30 basi zidisha utapata majibu ni
kiasi gani cha fedha kinachohitajika,” alisema mhandisi huyo wa umeme.
Kwa
kuzingatia hesabu hizo, Serikali inalazimika kutafuta zaidi ya Sh700
bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo ambavyo hata hivyo, hadi sasa
bado mpango wake haujawekwa wazi. Pia italazimika kutafuta kiasi kama
hicho kwa ajili ya ujenzi wa njia mpya ya kusafirishia umeme huo.
Habari
zaidi zilisema ili kupatikana kwa megawati 3,000 za umeme, kunahitaji
pia njia mpya za kusafirishia nishati hiyo ya msongo wa kilovolt 400,
tofauti na njia za sasa ambazo uwezo wake ni msongo wa kilovolt
220.“Kama tunataka kuongeza kiasi cha umeme katika njia zetu za sasa,
lazima tuongeze uwezo maana njia zetu zinazidiwa ndiyo maana wakati
mwingine umeme unakatika ovyo,” alisema mhandisi huyo.Hivi sasa Serikali
inajenga njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovolt 400 kutoka
Iringa kupitia Dodoma, Singida hadi Shinyanga, ujenzi ambao utaigharimu
kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 (karibu Sh800 bilioni) hadi
utakapokamilika.
Hata hivyo, njia hiyo ni maandalizi ya umeme
unaotarajiwa kuzalishwa kutoka miradi ya makaa ya mawe ya Ngaka mkoani
Ruvuma na Mchuchuma Wilaya ya Ludewa mkoani Iringa na siyo kwa ajili ya
usafirishaji wa umeme utakaozalishwa kutokana na gesi ya Mnazi Bay
kutoka Mtwara.Gharama za UmemeIkiwa ahadi ya Rais Kikwete itashindwa
kutekelezwa katika muda wa miezi 18 kama alivyoahidi, inaamanisha kwamba
taifa litaendelea kutumia umeme wa gharama kubwa unaozalishwa kwa
mafuta.
Tayari gharama hizo zimeanza kuwaelemea watumiaji baada ya
Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura), kuiruhusu Tanesco
kupandisha gharama za umeme kuanzia leo kwa asilimia 40.29.Upandishaji
huo umezua kilio nchi nzima ambako watu wa kada tofauti wamesema
utaongeza gharama za maisha na kuwaathiri wananchi wa kipato cha chini.
Kutumika
kwa umeme wa mafuta kunatokana na kutokuwepo kwa maji ya kutosha katika
mabwawa ya kuzalisha umeme. Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita,
uzalishaji ulikuwa ni asilimia 62.9 ya uwezo wa mabwawa hayo.Meneja
Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alisema hadi sasa umeme unaotokana na
maji ni megawati 353 kati ya 561 zinazotakiwa na kwamba hali hiyo
inatokana na uhaba wa maji.Mwisho……
|
|
No comments:
Post a Comment