Tuesday, 24 January 2012 20:52 |
HUDUMA MOI ZASITISHWA, WAGONJWA WARUDISHWA NYUMBANI, UONGOZI WADAI HALI NI SHWARI HUDUMA
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jana zilizorota kutwa nzima
kutokana na mgomo wa madaktari nchi nzima uliotangazwa juzi jioni na
kuanza jana huku uongozi wa hospitali hiyo ukisisitiza kuwa huduma
zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Mbali na hospitali hiyo, mgomo
huo pia uliripotiwa kuathiri utoaji wa huduma katika Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road huku huduma zikiendelea kama kawaida katika
hospitali nyingine karibu zote nchini. Idara zilizoathirika zaidi na mgomo huo Muhimbili ni katika kitengo cha Tiba ya Mifupa (Moi) na Idara ya Wagonjwa wa Nje (OPD).
Tangu
saa 12:30 asubuhi, idara hizo na wodi mbalimbali zilikuwa na msongamano
wa wagonjwa hasa Moi, huku wagonjwa wa nje waliokuwa wamepokewa,
wakiendelea kusubiri huduma ambayo hata hivyo, haikutolewa. Huduma katika Idara ya Wagonjwa wa Dharura ziliendelea kama kawaida.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, baadhi ya wagonjwa waliilani hatua ya madaktari
hao kugoma huku wengine wakiitupia lawama Serikali kwa kile walichoeleza
kuwa ndiyo chanzo cha adha hiyo.
Mmoja wa wagonjwa
walioathirika, Damian Mselea ambaye kwa sasa anaishi Kimara, Dar es
Salaam alisema alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya
KCMC Moshi kabla ya kuhamishiwa Moi.
“Nimesafiri kutoka Moshi
nikiwa na ndugu zangu na nilipofika leo (jana), wakalazimika
kuniwahisha ili niweze kupata huduma ya matibabu, lakini hadi sasa
sielewi nini kinaendelea,” alisema Mselea akiwa ndani ya gari la ndugu
yake akiwa ameshakaa humo kwa zaidi ya saa saba bila ya kupata huduma.
Mgonjwa
mwingine, Salome Raphael (64), mkazi wa Kinyerezi, Dar es Salaam ambaye
alifika Moi kupata tiba ya mguu wake uliovunjika alisema: “Nimefika
asubuhi na kuambiwa na watu wa mapokezi niende ofisi ya madaktari
nikaangalie kama wapo kisha nirudi mapokezi ili waniandikie niende
kumuona daktari.” Alisema kwa kawaida, mgonjwa kabla ya kumuona
daktari huanzia mapokezi na baada ya kuandikisha maelezo ndipo
huelekezwa chumba cha daktari.
Kwa upande wake, Rehema Mohamed wa
Madale, Dar es Salaam ambaye alifika Moi kutolewa nyuzi katika jeraha
lake la mguu alisema licha ya kukaa wodini kwa muda mrefu hakuweza
kumwona daktari na wala hakukuwa na dalili yoyote ya kuonana naye.
Vurugu OPD Wakati
wagonjwa hao wakiendelea kusubiri huduma, eneo la OPD nusura ligeuke
uwanja wa mapambano baada ya wagonjwa waliofika kupata huduma za
kliniki, kukosa tiba na kuanza kudai fedha zao. Wagonjwa hao na ndugu zao walisema kuwa wanapaswa kurudishiwa fedha zao walizolipa kujiandikisha kwa kuwa hawakuwaona madaktari.
Hata
hivyo, wagonjwa na watendaji katika eneo hilo walifikia mwafaka baada
ya kukubaliana kupangiana tarehe nyingine za kwenda kuonana na daktari
kwa fedha walizokuwa wameshatoa. Mmoja wa wagonjwa hao, Willy
Rwehumbiza alisema mgomo huo umemuathiri kwa ametokea mbali kufuata
huduma za kliniki ambazo ni kila baada ya miezi sita.
“Sina
ndugu, nimetoka Bukoba Mkoa wa Kagera, ni mfanyakazi katika Idara ya
Elimu na nina matatizo ya moyo, kitendo hiki kimeniathiri sana, sijui
itakuwaje” alisema akiwa kwenye foleni ya kwenda kupangiwa tarehe
nyingine. Mgonjwa mwingine, Flora Roman alilalamikia kupangiwa
kurejea Machi 27, mwaka huu... “Hii ni hatari, sisi tutakufa sasa, leo
nimekuja nimekosa huduma napangiwa Machi 27, hii si hatari! Tutafika
kweli?.”
Kwa upande wake, mgonjwa Theresia Mapunda wa Kimara,
Temboni Dar es Salaam, alisema alifanyiwa operesheni Septemba mwaka jana
na alipangiwa na daktari kurejea kwa uchunguzi kila mwezi lakini. “Nimeshangazwa
na hutua hii. Kila mwezi nakuja kufanyiwa uchunguzi, leo nimekuja
Sh5,000 wamechukua na nimepangiwa kurudi Machi 27,” alisema Mapunda.
Waokoa jahazi Wakati
madaktari wakiwa katika mgomo, habari zilizopatikana zimesema waliokuwa
wanaendelea kufanya kazi katika vitengo mbalimbali hospitalini hapo ni
madaktari walio kwenye mkataba na wanafunzi waliotoka chuoni. Hata
hivyo, eneo lililokuwa likiendelea kutoa huduma katika Taasisi ya Moi ni
la wagonjwa wa dharura pekee ambalo mmoja wa madaktari alisema wameona
ni vyema kutoa huduma hapo kwa sababu wanaofikishwa ni wagonjwa wenye
mahitaji ya haraka.
Licha ya kuwapo kwa hali hiyo, Ofisa Habari
Mwandamizi wa Hospitali hiyo, Aminiel Aligaeshi aliwaambia waandishi
kuwa madaktari wanaendelea na kazi na hakuna hata mmoja anayegoma. “Hapa kazi zinaendelea kama kawaida, wagonjwa wanatibiwa oneni wenyewe” alisema Aligaeshi. Alisema hospitali hiyo ya taifa ina madaktari 248 na madaktari walio katika mafunzo ya vitendo 174 na kwamba wote wako kazini.
Ofisa huyo aliwatembeza waandishi wa habari katika moja ya wodi hospitalini hapo kujionea hali halisi. Hata
hivyo, ofisa huyo alikataa kuwapeleka waandishi katika kitengo cha OPD
ambako ndiko kulikokuwa na idadi kubwa ya wagonjwa waliokuwa wakisubiri
huduma akisema: “Muda umekwisha si mmeshaona watu wanafanya kazi!”
Mgomo wayeyuka Hata
hivyo, wakati mgomo huo ukifanikiwa Muhimbili, huduma katika hospitali
nyingine kubwa nchini zikiwamo Temeke, Ilala, Mwananyamala na Hospitali
za mikoa ya Tanga, Dodoma, Iringa, Shinyanga, Arusha, Mara na
Kilimanjaro ziliendelea kama kawaida.
Madaktari katika Hospitali
za Mount Meru, Bugando, Bombo, Hospitali Teule ya Muheza, Korogwe na
Bunda waliendelea na kazi. Madaktari katika Hospitali za Magunga na
Bombo mkoani Tanga walisema wanasubiri kwa hamu maagizo kutoka kwa
viongozi wao ili nao wagome kuishinikiza Serikali ili isikilize kero
zao.
Katibu Mkuu wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda, Billy
Kinyaha alisema hakuna mgomo wowote kauli iliyothibitishwa pia na baadhi
ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo.
Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Mara, Dk Samson Winani alisema hakuna mgomo wowote uliofanyika:
“Sisi huku hatujagoma. Wanaogoma ni wa huko Dar es Salaam.”
Katika
Hospitali ya Mount Meru, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ya Mkoa wa
Arusha, Dk Omar Chande amesema madaktari wote jana walikuwa wakichapa
kazi. Hata hivyo, hakuna daktari aliyekuwa tayari kueleza ni kwa nini
hawakutekeleza maagizo ya kugoma kuanzia jana.
CUF walia na mawaziri Katika
hatua nyingine, Chama Cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete
kuwawajibisha Waziri wa Afya, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy
Nkya kwa kile kilichodai kuwa wameshindwa kutatua tatizo hilo.
Katika
taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, chama hicho
kilisema mbali na viongozi hao wa kisiasa, Rais pia anapaswa
kuwawajibisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Blandina Nyoni na Mganga Mkuu
wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
“CUF tunamtaka Rais Kikwete
kuwawajibisha wote kuanzia waziri, naibu waziri, katibu mkuu, mganga
mkuu wa Serikali, ambao wote ni wahusika wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, kwa kufanya kazi kwa dharau,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo
iliyosainiwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Haki za Binadamu,
Amina Mwidau. Habari hii imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Aidan
Mhando, Gedius Rwiza, Burhani Yakub na Raisa Said, Tanga; Ahmed Makongo,
Bunda; Mussa Juma, Arusha na Sheilla Sezzy, Mwanza. | | |
|
No comments:
Post a Comment