WAKATI mgomo wa madaktari ukizidi kusambaa nchini, wanataaluma hao
wamesema hawako tayari kumfuata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ofisini
kwake, badala yake yeye awafuate wanakofanyia mikutano yao.
Juzi,
wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake
jijini Dar es Salaam, Pinda aliwaangukia madaktari hao kuwa yupo tayari
kukutana nao wakati wowote na kuwataka waende ofisini kwake kuonana naye
ili wazungumze kuhusu madai yao.
Mgomo huo wa madaktari ambao
ulianzia katika hospitali za Muhimbili na Ocean Road, hadi jana ulikuwa
umesambaa katika hospitali nyingine nchini ambazo ni pamoja na Bugando
ya Mwanza, KCMC Moshi, Bunda mkoani Mara na Meta mkoani Mbeya na
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
'Pinda njoo wewe'
Akijibu
ombi hilo la Pinda, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo
huo, Dk Stephen Ulimboka alisema hatua ilipofikia madaktari hawatakuwa
tayari kumtafuta Waziri Mkuu.
“Kwa sasa mtu yeyote anayetutaka
atufuata hapa, hatuwezi kumtafuta tena Waziri Mkuu sababu tulishafanya
juhudi hizo bila ya mafanikio,” alisema Ulimboka ambaye pamoja na
wenzake wanafanya mikutano yao ukumbi wa Starlight.
Wizara yahaha
Madaktari
wakimtaka Pinda awafuate, wizara yenye dhamana na afya jana ilitoa
tamko kuhusu mgomo huo ikisema madaktari watapewa nyumba za kuishi
karibu na vituo vya kutolea huduma.
Tamko hilo lilitolewa Jijini Dar
es Salaam na Waziri wa Afya na Usatawi wa Jamii Dk Hadji Mponda
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mponda akijibu dai moja
baada ya jingine la madaktari hao, alisema serikali kupitia wizara
hiyo Menejimenti ya Utumishi wa Umma na wizara ya Fedha, inaendelea na
kazi ya kurekebisha waraka utakaoruhusu madaktari kupewa nyumba bila
kujali madaraja yao na mishahara.
Akifafanua kuhusu rufaa za
wagonjwa hususani vigogo kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu, alisema
wizara hugharamia watanzania wote bila kuangalia ni wa aina gani ili
mradi watimize vigezo vya kwenda kutibiwa nje.
Muhimbili hali mbaya
Katika
hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana wagonjwa waliambiwa warudi
nyumbani hadi watakapopata taarifa za kumalizika kwa mgomo kupitia
vyombo vya habari.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wagonjwa hao
walisema walipewa taarifa na baadhi ya wafanya kazi katika vitengo
tofauti, vinavyotoa huduma za kliniki hospitalini hapo.
Vitengo
vilivyodaiwa kuwatangazia habari hiyo wagonjwa hao ni Taasisi ya Mifupa
(MOI), kitengo cha kuhudumia watoto wenye matatizo ya upungufu wa damu
na kitengo cha Kliniki ya matatizo ya moyo.
Mmoja wa wagonjwa hao,
Rukia Hamisi alisema alipofika MOI alitokea mmoja wa wafanya kazi katika
taasisi hiyo na kuwatangazia kuwa wagonjwa wote waondoke eneo hilo hadi
watakapotangaziwa kuwa mgomo umekwisha.
“Mimi nimekuja tangu
asubuhi, lakini ilipofika saa tatu asubuhi alikuja mfanyakazi mmoja na
kututangazia kuwa tuondoke katika eneo hilo hadi tutakapo tangaziwa kuwa
mgomo umekwisha kupitia vyombo vya habari,” alisema Hamisi.
Mmoja wa
wafanya kazi wa MOI ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alikiri
kutoa taarifa hizo na kusisitiza kuwa hali hiyo imetokana na
madaktari wanaotakiwa kuwahudumia wagonjwa hawakuwapo kazini.
Muhonewa
Mfaume ambaye alikwenda hosptalini kwa ajili ya kutaka barua yake
aliyopewa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iweze kusainiwa na daktari
ili aweze kwenda kutibiwa nje ya nchi, alisema alipofika katika kitengo
hicho aliambiwa na mmoja wa wafanyakazi wa idara ya mapokezi kwamba,
arudi nyumbani
Afisa Habari Mwandamizi wa Hosptali ya Taifa
Muhimbili Aminiel Aligaesha alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alijibu kwa
kifupi kuwa hana taarifa na pia akasisitiza kuwa, huduma zinazoendelea
vizuri.
KCMC nako mambo yaharibika
Mgomo huo umezidi kutikisa
nchi na kuvuruga huduma za utabibu baada ya madaktari katika hospitali
ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi nao kujiunga rasmi kwenye mgomo.
Hata
hivyo, madaktari hao wamekubaliana kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura
tu wakiwamo wa ajali, wanaohitaji kujifungua na walioko wodi ya
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu(ICU).
Katika tamko lao
hilo, madaktari hao waliokutana katika ukumbi wa maktaba walisema katika
kipindi chote cha mgomo hawatapokea wagonjwa wa nje na kwamba kliniki
zote hazitafanya kazi.
Ingawa hospitali hiyo inamilikiwa na
Shirika la Msamaria mwema (GSF) lakini wapo madaktari ambao mikataba yao
ya ajira ipo chini ya shirika hilo na wapo ambao ajira zao ziko moja
kwa moja serikalini.
Bugando
Jana madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando waliungana na wenzao katika mgomo unaoendelea kusambaa nchi nzima hivi sasa.
Madaktari hao walianza mgomo kwa kukataa kuwapokea wagonjwa wapya isipokuwa wagonjwa wa dharura tu.
Wakizungumza
wakati wa mkutano wao uliofanyika katika hosteli ya madaktari
wanafunzi, walisema kurudi kwao kazini kutategemea maelekezo kutoka kwa
uongozi wa kamati maalum waliyoiunda kuratibu mgomo huo.
Juhudi
za uongozi wa hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi wake, Dk Charles
Majinge kuzuia mgomo huo ziligonga mwamba baada ya madaktari hao
kumweleza kuwa mgomo huo haujaitishwa dhidi ya hospitali hiyo wala
uongozi wake na kwamba, madai yao yako nje ya uwezo wa utawala wa
Bugando.
Dk Majinge alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mgomo wa madaktari katika hospitali yake.
Bunda
Huduma
ya tiba kwenye baadhi ya vituo vya afya wilayani Bunda, jana zilidorora
kufuatia baadhi ya madaktari na wahudumu kuitisha mgomo.
Mwananchi imebaini kuwa ingawa wahudumu na madaktari hao wamefika kazini kwa wakati lakini walikataa kuwahudumia wagonjwa.
“Mimi
nimefika hapa saa 3:00 asubuhi lakini sijahudumiwa. Wanaingia
(wahudumu) wanakaa ndani kisha wanatoka bila kuwaita wagonjwa," alisema
mmoja hospitalini hapo saa 8:00 mchana jana.
Kaimu mganga mkuu wa
wilaya hiyo Dk Fransic Mayengera alikana uwepo wa mgomo hospitalini
hapo na huku aiita hatua hiyo kuwa ni kutokana na uzembe wa watumishi wa
hospitali na kwamba uongozi wake umeanza kuwashughulikia."
Wajawazito wateseka Mbeya
Mgomo
wa madaktari katika Hospitali ya Meta mkoani jana uliwaathiri zaidi
kina mama wajawazito huku wengine wao wakiambiwa kuwa waende katika
hospitali nyingine kwa vile hospitalini hapo hakuna huduma.
Kila
mgonjwa aliyefika hospitalini hapo jana alielezwa kuwa hakukuwa na
huduma hivyo, akatafute hospitali nyingine huku baadhi ya wauguzi
wakijibizana na wagonjwa.
Baadhi ya Waandishi wa habari
waliofika katika kituo hicho cha Meta walishuhudia mama mjamzito, Sarah
Christopher akiambiwa aende kwenye hospitali nyingine huku hali yake
ikionyesha ni mbaya.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo ya Meta Dk
Leter Msafiri alisema kutokana na mgomo unaoendelea, kuna baadhi ya
huduma zimesitishwa ila wanatoa huduma za dharura ambazo ni pamoja na
upasuaji unaofanywa na madaktari bingwa.
Dk Msafiri alisema huduma zilizositishwa ni kliniki na huduma ambazo wagonjwa wanaonekana kuwa hali zao siyo mbaya.
Kilaini
Askofu
Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilani alisema inasikitisha
kuona wagonjwa wakiteseka hospitalini kutokana na mgomo huo.
"Kwa namna yoyote ile, wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kwa sababu suala la matibabu linahusisha ni uhai," alisisitiza na kuongeza:
"Inaleta
shida kidogo kujua kwa nini Serikali haitatui madai ya madaktari ambayo
ni ya msingi, au haina fedha? Kama Serikali haina fedha iseme ili
wahusika na Watanzania wote wajue.’’
Baregu LHRC
Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu (LHRC), kimemtaka Pinda, kwenda kuonana na
madaktari hao badala ya kusubiri wamfuate ofisini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba alisema haiwezekani Waziri Mkuu
aendelee kukaa ofisini wakati anajua kuwa madaktari wanagoma na wagonjwa
wanataabika.
“Hakuna haja ya Pinda kusema madaktari wakiwa tayari
waende kuonana naye kwa sababu huu ni ubabaishaji. Wao (madaktari) wako
tayari na ndio maana wakagoma hadi pale madai yao yatakaposikilizwa sasa
yeye (Pinda) akiendelea kuwasubiri ofisini maana yake nini kama sio
kuleta vifo?"
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment