Monday, 10 January 2011

Sitta: Dowans wanacheza na makaratasi wasilipwe

WAZIRI wa Afrika ya Mashariki, Samuel Sitta amesema Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Dowans wanacheza mchezo katika makaratasi ili wajipatia mabilioni ya shilingi ya Watanzania.
Sitta ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipinga Serikali kuilipa kampuni hiyo alisema kitendo cha kuwailipa itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

" Dowans ni wajanja wamecheza mchezo katika makaratasi kitu ambacho ukikaa chini na kukichunguza kwa makini utagundua kuwa, tumelipa mamilioni ya fedha bila ya sababu za msingi," alisema.

Mahakama ya Kimataifa ya Biashara imeamru Tanesco kuilipa Dowans Sh 94 bilioni kwa madia kuvunja mkataba kiyume cha taratibu.

Waziri Sitta alisikitishwa na uamuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema na Waziri wa Nishati na Madini William, Ngeleja wa kukubali kirahisi  kuilipa kampuni feki Dowars  mabilion ya fedha za wananchi.
“Kitu hicho ni hatari sana na jamii itakuja kutuhukumu kwa hilo,” alisema Sitta wakati wa mahafali ya shule ya Sekondari ya Marathani iliyoko eneo la Mianzini jijini Arusha.

Waziri Sitta alisema serikali haikupaswa kuilipa haraka Kampuni ya Dowans kwani bado ni tata na kulikuwa na nafasi ya kuendelea na shauri hilo.
Alisema Dowans kulipaswa kufikishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri, ili kujadiliwa kwa kina hasa kutokana na utata wake kuliko kufanya maamuzi ya haraka.

Waziri Sitta alisema, Dowans ni ndugu wa Kampuni ya Richmond ambayo iligundulika na kamati ya Dk Harrison Mwakyembe kuwa ni kampuni ambayo hakuwa halali.

‘’Mzabuni feki anacheza karata zake na mbia wake Dowans na sisi tunadiriki kulipa kitu ambacho  haramu kamwe haiwezi kuwa halali katika maisha yote... binafsi nimesikitika sana.’’

Waziri Sitta alitoa mfano wa mtu mmoja wa hapa nchini (hakumtaja jina) kuwa ana makampuni 17, lakini jina lake halimo katika kampuni yoyote kati ya hizo na anachezea michezo michafu Serikali na kulipwa mamilioni ya fedha.
"Kuna watu wanacheza na makaratasi kufanya  ujanja na kuhalalisha wakati ni haramu kujipatia mamilioni ya fedha za walipa kodi wa nchi hii, lazima tuwe makini nao," alionya Sitta.

Waziri Sitta ambaye alikuwa Spika katika bunge la tisa lililoibua tuhuma nzito kwa kampuni ya Richmond, alisema amesikitishwa na kauli ya Mwanasheria wa Serikali ya kunawa mikono mapema na kukubali kuilipa Dowans hatua iliyomshitua.

Alisema jambo zito kama hilo ni lazima serikali ingelikaa chini na kuliangalia suala kwa mapana na hata ingewezekana kuitisha kikao cha baraza la mawaziri kulijadili kwa kina na kulipatia ufumbuzi wa pamoja.
Sitta alisema fedha hizo zingeweza kujenga shule za sekondari 300 na kujenga barabara ya lami ya kilo mita 100 yenye ubora wa hali ya juu.

‘’Naweza kusema wajanja wametuzidi akili na wamefaidi kodi za wananchi kujilipa, lakini elimu bila maadili inaweza kwenda mrama,’’ alisema Sitta.

Waziri Sitta alisema kwa sasa huwezi kufanya chochote juu ya kulipa au kuacha kuilipa Dowans.
Sita alikejeli akisema: Unawezaje kufunga zizi la ng’ombe wakati ng’ombe wote wameshaondoka”.
Alisema yeye ataendelea kusema ukweli mwanzo hadi mwisho bila ya kumwogopa mtu yoyote na kamwe hawezi kuwa mwongo na mnafiki kwa jambo lolote.

Waziri Sitta pamoja na wabunge wengine kadhaa, walikuwa katika kundi lililokuwa linapiga vita ufisadi ndani ya CCM, amekuwa akipinga kulipwa kampuni ya Dowans mara kadhaa lakini sasa serikali imeamua kuilipa.
 source:mwananchi

NB:TUTASIKIA MENGI MWAKA HUU LAKINI NDO HIVYO TUSHALIWA TENA HIZO DOLALE JAMAA WATALIPWA TUPENDE TUSIPENDE NA WANANCHI WASHAANZA KUKAMULIWA KUZILIPIA KUTOKA KWENYE BEI ZA UMEME ZILIZOPANDA,YAANI HADI KIZUNGUZUNGU UMEME UMEPANDA BEI LAKINI HAUWAKI VILE VILE BADO WA MGAO NA WATU WANAISHI KIZANI MUDA MWINGIUONEVU GANI HUO 

No comments:

Post a Comment