Tuesday, 8 February 2011

MB.JANUARY MAKAMBA AZUNGUMZIA DOWANS,IPTL


MBUNGE WA BUMBULI MH.JANUARY MAKAMBA

MBUNGE wa Bumbuli, January Makamba, amemwandikia waraka Waziri wa Nishati na Madini kumtaka afafanue bungeni mambo kadhaa yanayohusu wizara hiyo, likiwamo sakata la Kampuni ya Dowans.Sehemu ya waraka huo imeibua jambo kwa mwanasheria wa Tanesco aliyesimamia kesi ya Dowans ambapo mbunge huyu anaeleza jinsi alivyocheza karata pande zote mbili kwa kushauri mkataba dhidi ya kampuni hiyo uvunjwe huku upande mwingine akiisifia na kuiombea mkopo wa Sh 20 bilioni katika Benki ya Stanbic.

Katika waraka huo wenye kichwa cha  habari, "Yah: Taarifa ya Serikali Bungeni kuhusu Umeme Nchini,"  Mbunge Makamba ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba anataja mambo hayo kumi ambayo Waziri William Ngeleja, anapaswa kuyafafanua kwa umma kupitia Bunge.

Waziri Ngeleja alipoulizwa kwa njia ya simu alikiri kuupata waraka huo na kuongeza, "Lakini, hadi sasa sijaufanyia kazi. Upo ofisini nimeambiwa umefika."

Wakati Ngeleja akikuna kichwa, Makamba katika waraka huo ambao nakala imeenda kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema:, "Kuhusu shauri la Dowans, Watanzania wameshuhudia kioja cha mawaziri wa serikali kujibizana na kupingana kwenye magazeti kuhusu malipo ya tuzo ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) kwa kampuni ya Dowans."

...Taarifa ya Serikali bungeni kuhusu jambo hili ni muhimu ili kuweka bayana kwa Watanzania kwamba ni wakati gani, kwa njia gani na kwa jinsi gani Serikali inawasiliana na umma ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi na  sisi wabunge kuhusu msimamo wa Serikali kwenye masuala mbalimbali."

Mwanasiasa huyo kijana aliongeza, "Mheshimiwa waziri, mnamo tarehe 6 Januari 2011, ulizungumza na waandishi wa habari na kueleza Serikali inajipanga kuilipa Dowans tuzo iliyoamuliwa na ICC."

"Lakini, kwa kuwa mzigo huu ni mzito kwa umma..., kumekuwa na fikra ikiwemo pendekezo la kamati ya wabunge wote wa CCM kwamba ni muhimu kutumia mianya ya kisheria iliyopo kupinga rasmi kutekelezwa kwa hukumu hiyo."

Akionyesha msisitizo katika hilo alisema, kwa kuwa hiyo imekwishasajiliwa Mahakama Kuu nchini na huku kila siku inayopita faini kwa Tanesco huongezeka kwa Sh 17milioni ni wakati wa Serikali kueleza ni lini itapeleka pingamizi la hukumu hiyo.

"Na hatua hii inamuweka wapi Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na tamko lako la Januari 6, 2011 kwamba kupinga utekelezaji wa hukumu ya ICC ni kupoteza muda," alihoji Makamba. 

Akikazia katika Dowans, Makamba aliibua hoja akisema, katika viambatanisho vya hukumu ya ICC kama ilivyosajiliwa Mahakama Kuu zipo nyaraka zinazoonyesha mwanasheria aliyeishauri Tanesco kuvunja mkataba na kampuni hiyo akisema haukuwa halali na kusingekuwa na madhara kwa kuuvunja, ndiye huyo pia aliyeishauri Benki ya Stanbic kutoa mkopo wa dola za Kimarekani 20 milioni  kwa Dowans.

"Na ndiye huyo huyo aliyeiwakilisha Tanesco kwenye kesi iliyofunguliwa na Dowans, kesi ambayo imetokana na ushauri wake... Na baada ya hukumu, ndiye huyo huyo kwa mujibu wa maelezo yako aliyekuja kutoa ushauri kwamba hakuna njia nyingine zaidi ya kuilipa Dowans baada ya hukumu," aliibua hoja hiyo nzito na kuongeza,

"Mheshimiwa Waziri, jambo hili likibaki hivi hivi bila maelezo inaweza kujengeka sura kwamba Serikali ilikosa umakini kwenye jambo hili zima na maadili  hayakuzingatiwa... Itakuwa vyema kama taarifa ya serikali ikaeleza ni wanasheria gani waliotumiwa na Tanesco kwenye kila hatua shauri la Dowans."

Katika barua hiyo yenye kurasa tano, Makamba alitaka taarifa hiyo itaje wanasheria walioshiriki kuanzia kwenye ushauri kabla ya kuvunjwa kwa mkataba hadi ushauri baada ya kesi kuamuliwa na kiasi cha fedha walizolipwa kwa kila hatua, na utaratibu uliotumika.

Alienda mbali akisema, katika kuondoa Watanzania wasiwasi ambao wanaamini Tanesco ilishindwa kwenye kesi hiyo ya Dowans kutokana na upungufu wa weledi kwa wanasheria walioiwakilisha kwenye kesi hiyo, "Nashauri taarifa ya Serikali ieleze utaratibu uliotumika kuwapata wanasheria walioiwakilisha Serikali na Tanesco kwenye mashauri yaliyofunguliwa."

Amtaka atoe maelezo kesi mbili za IPTL
Mbunge huyo alisema anamsihi waziri atoe pia maelezo kuhusu kesi mbili zinazohusiana na mkataba wa uzalishaji wa umeme wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Makamba anataka waziri aeleze mchakato wa kesi hizo zilizofunguliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong dhidi ya Serikali na Tanesco kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kesi za Uwekezaji (ICSID).

Makamba alifafanua, "Kesi hizo ni ICSID No ARB/10/20 dhidi ya Tanesco iliyofunguliwa Oktoba Mosi, 2010 na ICSID No ARB/10/12 dhidi ya Jamhuri ya Muungano iliyofunguliwa Juni 11, 2010, zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa umma na zinaweza hata kuigharimu Serikali pesa nyingi kuliko zinazodaiwa katika kesi ya Dowans."

Alisema taarifa ya Serikali bungeni kuhusu kesi hizo mbili itasaidia Watanzania kufahamu:, "Nini kinadaiwa dhidi ya Tanesco na Serikali pamoja na maandalizi ya Serikali kushinda kesi hizi ili kuepukana na marudio ya zahama ya Dowans."

Katika kuonyesha msisitizo, mbunge huyo, alimtaka waziri kama ataona inafaa awajulishe Watanzania sababu za Serikali kutotoa taarifa za kesi hizo mbili muhimu kwa maslahi ya umma hadi sasa.

..Ahoji matamko sita ya Serikali kumaliza tatizo la umeme

Akizungumzia zaidi ahadi na matamko ya kumaliza tatizo la umeme, Makamba alisema tangu mwaka 2006 hadi sasa zimetoka ahadi na matamko sita ya Serikali ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme nchini, lakini hadi sasa bado mgawo unaendelea.

Makamba aliweka bayana kwamba, ingawa kila kunapotokea mgawo kumekuwa na maelezo na sababu mbalimbali, lakini ahadi hizo mara nyingi zimekuwa zikijirudia na kuongeza:, "Wewe (Ngeleja) mwenyewe umetoa ahadi kadhaa za kumaliza tatizo hili, lakini ahadi hizo hazikutumia."

Alisema matokeo ya hali hiyo ni wananchi kupoteza imani na uwezo wa Serikali yao kutatua tatizo la umeme nchini na hata matatizo yao mengine na kuonya:, "Kuna gharama kubwa kwa wananchi kupoteza imani na Serikali yao."

"Mimi naamini kwa dhati kabisa, kama Serikali ikitoa tamko la dhati kabisa bungeni linalobainisha kwa kina na uwazi sababu za ahadi hizi za mara kwa mara basi tutakuwa tumepiga hatua kwenye kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao," aliongeza.

IPTL inavyoigharimu Serikali
Akikazia katika IPTL, alisema mtambo unaozalisha umeme wa kutumia mafuta mazito aina ya HFO unaigharimu Serikali mabilioni ya shilingi kwa mwezi licha ya kuzalisha umeme chini ya nusu ya uwezo wake, kutokana na uhaba wa na bei kubwa ya mafuta.

Mbunge huyo alisema kutokana na gharama hizo kubwa, Serikali imeamua kulipia gharama zote za kubadilisha au kukarabati mitambo hiyo ambayo si mali yake bali IPTL ili itumie gesi asilia badala ya mafuta mazito ya HFO.

"Mwaka 2006, Serikali iliingia mkataba na Kampuni ya Alstom Power Rentals kuzalisha umeme mkoani Mwanza kwa kutumia mitambo ya mafuta, kutokana na shida na gharama ya upatikanaji mafuta na kuyasafirisha mpaka Mwanza, mtambo huo haukutumika kuzalisha umeme hata siku moja ndani ya miezi 12 ya mkataba, zaidi ya saa 20 tu kwa ajili ya majaribio kabla ya mtambo kukabidhiwa kwa Serikali," alisema na kuongeza,

"Kwa kifupi ni kwamba kampuni hiyo ililipwa kiasi cha dola za Marekani 1.7 milioni (takriban Sh 2.5bilioni), kwa mwezi za bure, bila kuzalisha umeme wowote. Ili wananchi waone kwamba Serikali yao ina uchungu na rasilimali za umma, nashauri taarifa ya Serikali ieleze hatua za uwajibikaji kwa hasara hii ya takriban dola 20 milioni." 

Mzimu wa mikataba ya umeme Tanesco imekuwa ikiitikisa nchi ambayo mwaka 2008, ilisababisha Baraza la Mawaziri la kwanza la Serikali ya awamu ya nne kuvunjwa, baada ya Kamati Teule ya Bunge kubaini mkataba kati ya Kampuni ya Richmond na shirika hilo ulikuwa na walakini

source:mwananchi

No comments:

Post a Comment