Monday, 14 February 2011

POLITIKI NA UFISADI

Chenge ajitakasa kashfa ya rada


MWANASHERIA Mkuu wa Serikali wa zamani, Bw. Andrew Chenge ameitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kuwa yeye ni
mwadilifu, mtu safi, hakutenda kosa lolote katika kashfa ya rada, ambayo Serikali ya Tanzania imekuwa ikidaiwa kuinunua kwa bei ya juu kuliko thamani yake nchini Uingereza.

Bw. Chenge ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Miundombinu katika muhula wa kwanza wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kisha akajiuzulu kutokana na kashfa ya rada..., hakuwa tayari kutoa fursa kwa waandishi wa habari kuuliza maswali akidai kuwa maadili ya taaluma ya sheria hayamruhusu, kwani alichokuwa akisoma ilikuwa ni hukumu ya mahakama, si maneno yake.

Akisoma taarifa yake kwa vyombo vya habari inayotokana na hukumu ya kesi ya kashfa ya rada iliyoamuliwa hivi karibuni nchini Uingereza, Bw. Chenge alisema kuwa uchunguzi uliofanywa na vyombo husika, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Taasisi ya Makosa Makubwa (SFO) ya Uingereza, umebaini kuwa yeye ni mtu safi.

"Kama mnavyokumbuka kwa muda mrefu sasa, jina langu lilihusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada ya Serikali ya Tanzania kutoka Kampuni ya British Aerospace Systems maarufu kama BAE. Yalikuwapo madai kwamba nimehusika katika vitendo vya rushwa katika ununuzi wa rada hiyo mwaka 1999, madai ambayo mara zote nimekuwa nikiyakanusha.

"Kutokana na suala hilo kugusa hisia za watu na maslahi ya Serikali ya Uingereza, kulikuwapo na uchunguzi na kesi mahakamani kuhusiana na mwenendo wa BAE katika suala la rada, kesi ambayo iliendeshwa kwa uchunguzi wa Ofisi ya Kuchunguza Mashtaka Makubwa ya Jinai Uingereza (SFO).

Akisoma mwenendo wa uchunguzi na shauri hilo la rada, Bw. Chenge alisema;

"Kufuatia uchunguzi wa muda mrefu na wa kina kuhusu mikataba inayohusu nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Zzech, Hungary na Tanzania, tarehe 16 Februari mwaka jana, Ofisi ya Kuchunguza Rushwa nzito Uingereza, Serious Fraud Office (SFO), walifikia makubaliano na Kampuni ya British Aerospace Sytems P.L.C.

"Kufuatia makubaliano hayo, SFO iliishtaki Kampuni ya BAE Systems PLC kwa kuweka mahesabu yake kinyume cha utaratibu na sheria ya uendeshaji makampuni ya Uingereza. Malalamiko hayo yalikuwa kwamba kati ya mwaka 1999 na 2005, BAE Systems PLC kinyume cha utaratibu wa uendeshaji makampuni kama ulivyoainishwa katika Kifungu Namba 221 cha Sheria ya Makampuni ya Uingereza ya mwaka 1985.

Bw. Chenge ambaye jana ilikuwa ni mara ya pili kuwaambia waandishi wa habari kuwa yeye ni msafi kutokana na kutokutwa na hatia yoyote katika kashfa ya rada, akisoma taarifa ya mwenendo wa uchunguzi na shauri hilo lisema kutokana na uzito wa kesi hiyo Serikali ya Uingereza iliona umuhimu wa kuifikisha mahakama kuu, badala ya mahakama za chini kama ilivyo kawaida.

Aliongeza kuwa moja ya makubaliano ya kumaliza shauri kati ya SFO na Kampuni ya BAE ilikuwa ni kampuni hiyo ikubali kosa kwa shauri lililofikishwa mahakamani.

"Ifuatayo ndiyo misingi ya kulimaliza shauri hili; moja ya matukio yaliyofanyiwa uchunguzi na SFO ni mauzo ya rada kwa Serikali ya Tanzania. Tarehe 10 Septemba 1999, mkataba wa mauzo ya rada ulisainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na British Aerospace Defence Systems ukiwa na thamani ya dola za Marekani 39.97 milioni.

"Mwanzoni kabisa mwa majadiliano ya ununuzi wa rada hiyo, Kampuni ya Siemens Plessey Electronics Systems Limited ilimteua Bw. Shailes Vithlani kuwa mshauri wake nchini. Na akiwa Tanzania, Bw. Vithlani alipewa jukumu la kusaidia majadiliano na kufuatilia taratibu zote za mauzo... Mwaka 1998, BAE Systems Group, iliinunua Kampuni ya Siemens Electronic Systems Limited," alisema Bw. Chenge.

Alisema kuwa baada ya BAE Group kuinunua Siemens Limited, iliendeleza mkataba na Bw. Vithlani kuwa mshauri wa mambo ya masoko nchini Tanzania, mkataba uliohusisha kampuni tanzu mbili zilizo chini ya BAE P.L.C kwa upande mmoja na kampuni nyingine mbili za Bw. Vithlani ambazo ni Merlin International Ltd (Merlin; iliyosajiliwa Tanzania) na Envers Trading Corporation Ltd (Envers; iliyosajiliwa nje ya nchi).

Mbali ya uteuzi wa kampuni hizo mbili kuthibitishwa na uongozi wa juu wa BAE, chini ya makubaliano hayo, alisema Bw. Chenge, Merlin ingepata asilimia 1 kama malipo ya kibiashara ya mkataba na Envers ingelipwa asilimia 30.

Hivyo mara baada ya mkataba wa rada kusainiwa, kwa mujibu wa Bw. Chenge, malipo ya karibu dola za Marekani milioni 12.4  yalifanywa kwa makampuni ya Merlin na Envers, ambayo yaliwekwa katika rekodi za mahesabu ya BAE Defense Sytems Limited, yakionesha kuwa ni malipo ya kutoa huduma za kitaalamu.

"Makubaliano yaliyofikiwa mahakamani kulimaliza shauri hilo ni kama ifuatavyo; SFO haitamshtaki mtu yeyote kufuatia uchunguzi huo labda kwa walioshukiwa na kashfa za Jamhuri ya Czech na Hungary. SFO isitishe uchunguzi wowote unayoihusu Kampuni ya BAE Systems Group. Hakutakuwa na mashtaka ya aina yoyote yatakayohusu uongozi wa BAE Systems kufuatia uchunguzi uliofanywa na SFO.

"Kutokana na yaliyozungumzwa mahakamani, imejitokeza wazi kwamba SFO wamemaliza uchunguzi wao kuhusu Kampuni ya BAE na shughuli zake Tanzania. Na imekubalika kwamba SFO hawatafanya uchunguzi mwingine kwa kuwa hakuna ushahidi wowote wa rushwa. Jaji wa mahakama kuu amekubaliana na upande wa mashataka kuwa kwa sasa itakuwa vigumu kujua Vithlani amezitumiaje pesa alizolipwa.

"Bwana Andrew Chenge alikua Waziri wa Miundombinu katika Serikali ya Tanzania mpaka alipojiuzulu wadhifa huo tarehe 20 April, 2008, ili kutoa fursa kwa SFO na TAKUKURU kufanya uchunguzi wao na ambao sasa umekamilika.

"Tarehe 8, Novemba 2010, TAKUKURU walitangaza kuwa wamekamilisha uchunguzi wao na kwamba kutokana na uchunguzi uliofanyika, hakuna ushahidi wowote unaomhusu Bwana Andrew Chenge. Na sasa ni wazi kuwa uchunguzi uliofanywa Uingereza na Tanzania na mamlaka husika umegundua kuwa Bwana Chenge hahusiki.

"Mimi ni muadilifu, nimefanya kazi katika awamu zote nne za uongozi wa nchi yetu. Hata nilipojiuzulu sikuwa na hofu wala mashaka ya kupoteza kazi, kwa kuwa nilijiamini kuwa sikutenda kosa lolote katika kashfa hiyo ya rada, na nilisema iko siku ukweli utajulikana.

"Uchunguzi umefanyika na sasa ukweli umejulikana. Wahenga wamenena 'kwenye ukweli uongo hujitenga'. SFO na TAKUKURU wamefanya uchunguzi wa kina na matokeo ya uchunguzi wa vyombo hivyo viwili yamedhihirisha kuwa mimi ni mtu safi," alisema Bw. Chenge.

Alisema kuwa ukweli umejulikana kuwa ununuzi wa rada ulifanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zote za serikali.

MAJIRA

No comments:

Post a Comment