Tuesday, 1 February 2011
WATOTO 11 WAKUTWA WAMEFUKIWA SHIMONI DAR
KATIKA hali isiyo ya kawaida, wakazi wa Mwananyamala Kwakopa, jijini Dar es Salaam wamepatwa na mshituko mkubwa baada ya kaburi moja kugundulika jana (Jumatatu) likiwa na watoto 11 waliozikwa ndani yake, tukio lililoelezwa kuwa ni ukatili wa kutisha, Uwazi lina habari kamili.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa mkazi mmoja wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina moja la Thabiti ndiye aliyeligundua kaburi hilo alipokuwa akitafuta sehemu ya kuchimba jalala, jirani na Hospitali ya Mwananyamala.
Ilielezwa kuwa mzee huyo alipofika eneo hilo alishtuka baada ya kuona nzi wengi wamezingira huku kukiwa na harufu kali, machale yakamcheza na kuhisi kuwa huenda kuna kitu kibaya kimefukiwa.
“Mzee Thabiti aliamua kuwataarifu polisi ambao walifika eneo la tukio, jirani na makaburi ya Mwananyamala. Baada ya kuona hali ilivyokuwa, polisi waliwapigia simu madaktari waliowasili muda mfupi baadaye,” kilieleza chanzo chetu.
POLISI KUFIKA ENEO LA TUKIO
Habari zinaeleza kuwa mara baada ya polisi kupewa taarifa hizo na kuwasili eneo la tukio wakiwa kwenye gari aina ya Landrover ‘defender’ walianza uchunguzi wao maraDakika chache baadaye shimo likiwa na urefu wa futi nne, lilionekana shuka jeupe likiwa limeviringishwa kitu. Lilipotolewa, kwa mshangao mkubwa maiti ya kitoto kichanga ikadondoka.
Polisi aliyekuwa akifanya kazi hiyo alipolichunguza vizuri shuka lile, aligundua kuwa kuna kitu kingine kimebaki. Alipoingiza mkono, alichomoa maiti nyingine ya kitoto kichanga.
KANGA KIBAO ZILITUMIKA
Askari huyo aliendelea na zoezi hilo na baadaye akalifunua kabisa shuka hilo, ndipo alipokuta maiti nyingine za watoto wachanga zikiwa zimevingirishwa kwenye kanga tofauti.
Zilipohesabiwa ilibainika kuwa jumla ya maiti 11 zilikuwa zimefukiwa kwenye kaburi hilo.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa moja ya kanga iliyokutwa kwenye kaburi hilo ilikuwa imebandikwa plasta yenye maneno yaliyosomeka: ‘Ruth Mtanga, Male Pre-mature (yakimaanisha kuwa mwanamke mwenye jina hilo alikuwa amejifungua ‘njiti’ wa kiume).
Haikufahamika maandishi yale kwenye plasta hiyo yameandikwa na nani katika hospitali gani, hivyo polisi wakaanzia uchunguzi wao hapo.
DAKTARI AKACHA WANAHABARI
Daktari mmoja wa Hospitali ya Mwananyamala aliyefahamika kwa jina moja la Karamahia, alipohojiwa kuhusiana na shuka hilo pamoja na maiti za watoto hao wachanga, alikataa kusema chochote kwa madai kuwa tayari sakata hilo lipo mikononi mwa polisi.
Polisi waliondoka na miili hiyo kuelekea Hospitali ya Mwananyamala, ilikoenda kuhifadhiwa wakati uchunguzi wa kina ukiendelea.
source:gpl
NI MATUMAINI YANGU WALIOHUSIKA NA KITENDO HICHO WATAKAMATWA NA KUCHUKULIWA HATUA IWAPO WATAGUNDULIKA NA MAKOSA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment