Send to a friend |
Tuesday, 22 November 2011 21:02 |
ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kushindwa kuweka kumbukumbu za ununuzi wa magari chakavu yenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni. Mbali ya Mattaka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa shirika hilo, Elisaph Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, William Haji. Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincon alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo kati ya Juni na Julai, 2007. Katika shtaka la kwanza ambalo linawahusu wote watatu, ilidaiwa kuwa kati ya Juni na Julai, 2007 Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam washtakiwa kwa nafasi zao walishindwa kutunza kumbukumbu za taarifa za kukubali zabuni ya ununuzi wa magari chakavu 26. Mwendesha mashtaka alidai kuwa katika shtaka la pili ambalo pia linawahusu washtakiwa wote, kati ya Julai 2 na Agosti 23, 2007 kwa pamoja, walishindwa kufuata taratibu za ununuzi wa umma katika magari chakavu 26 yenye thamani ya Dola za Marekani 809,300,000 kutoka katika Kampuni ya Bin Dalmouk Morots Co. Ltd ya Dubai. Katika shtaka la tatu linalomuhusu Mattaka, ilidaiwa kuwa kati ya Julai 2 na Agosti 23, 2007 akiwa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, alitumia madaraka yake vibaya katika ununuzi wa magari hayo bila kuwepo kwa mkataba wa zabuni uliosainiwa na pande zote mbili na kuhakikiwa na bodi ya zabuni ya shirika hilo suala ambalo ni kinyume cha sheria. Baada ya kusomwa mashtaka hayo, upande wa mashtaka kupitia kwa wakili wa Serikali Oswald Tibabyekomya ulisema kuwa haupingi dhamana kwa washtakiwa lakini ukaitaka mahakama kuzingatia kifungu namba 148 (5) (e) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Kwa mujibu wa kifungu hicho, mshtakiwa wa kosa linalozidi Sh10 milioni anatakiwa kuweka mahakamani nusu ya fedha alizoshtakiwa nazo kama dhamana. Hata hivyo, upande wa utetezi uliokuwa unaongozwa na Mawakili, Peter Swai na Alex Mgongolwa ulipinga kifungu hicho kwa madai kuwa hakiendani na mashtaka yanayowakabili wateja wao. “Tunapinga hoja za upande wa mashtaka kwa sababu katika mashtaka yanayowakabili wateja wetu hakuna mahala palipotajwa kwamba wamesababisha hasara ama wizi,” alisema Swai. Mshtakiwa wa pili ambaye hakuwa na wakili, aliiomba mahakama impe dhamana kwa madai kuwa yeye ni mfanyakazi mwaminifu wa Serikali kwani ni mwanataaluma ambaye amesajiliwa na Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), anayekagua hesabu za Serikali na taasisi mbalimbali. Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Mkazi, Rita Tarimo alikubaliana na hoja za upande wa utetezi kwamba mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao hayahusiani na kusababisha hasara au wizi hivyo akatoa masharti ya dhamana. Katika masharti hayo, kila mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini dhamana ya maneno ya Sh10 milioni. Washtakiwa wote walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi Desemba 5, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena. Mattaka alistaafu utumishi wa umma Mei mwaka huu baada ya kuitumikia ATCL kwa miaka mitano. chanzo,mwananchi |
No comments:
Post a Comment