Thursday, 10 November 2011

MBOWE AJISALIMISHA POLISI

POLISI YAPIGA MARUFUKU MAANDAMANO NA MIKUTANO YOTE YA CHADEMA NCHINI



Waandishi Wetu
WAKATI Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akijisalimisha polisi jana na kutangaza kuendeleza mapambano ya kudai haki na demokrasia ya kweli, Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku maandamano na mikutano yote ya chama hicho nchi nzima kwa muda usiojulikana.
Kujisalimisha polisi kwa Mbowe kunatokana na amri iliyotolewa juzi na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Akili Mpwapwa baada ya kiongozi huyo kuwatoka polisi waliofanya operesheni ya kushtukiza alfajiri ya kuamkia juzi, kutawanya mamia ya wafuasi wa Chadema walioongozwa na viongozi hao wa kitaifa na kuamua kupiga kambi kwa siku tatu kwenye Uwanja wa NMC Unga Limited wakishinikiza kuachiwa kwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema.

Jana, Mbowe alifika Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Arusha, Barabara ya Makongoro, saa 5:45 asubuhi na kupokewa na Kamanda wa Operesheni Maalumu, Naibu Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Simon Sirro.

Muda mfupi kabla ya kukutana na Sirro, Mbowe alifanya mazungumzo na waandishi wa habari na kutangaza aina mpya ya mapambano dhidi ya kile alichokiita ukandamizaji, manyanyaso, kudharauliwa na uonevu wa dola kwa viongozi na vyama vya upinzani.
“Nimefikia uamuzi wa kwenda polisi baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa wananitafuta na wanatangaza uongo kuwa nilikimbia. Mimi Mbowe niwakimbie polisi! Mimi?… hawamfahamu Mbowe nini?”

Alisema wakati polisi wanavamia Uwanja wa NMC ulikofanyika mkesha kushinikiza kuachiwa kwa dhamana kwa Lema hakuwapo.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema msingi wa migogoro na matatizo ya Arusha ni uchaguzi wa Meya wa Manispaa na kusisitiza kwamba ufumbuzi wake hauwezi kupatikana kwa kutumia mabavu, dola wala mahakama, bali kinachohitajika ni busara na majadiliano ya pande zote husika akiilaumu Serikali kwa uamuzi wake wa kutumia vyombo vya dola kama rungu la kudhibiti wanaohoji mambo ya msingi kwa maslahi ya umma.

“Badala ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la Arusha, Serikali imeamua kutumia vyombo vya dola kukandamiza haki na fikra za wana Arusha huku Mkuu wa Mkoa mpya, Magessa Mulongo ambaye ni mgeni na hajui lolote kuhusu mgogoro huu akitumia nafasi yake kuwatisha wananchi,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema ushahidi kuwa utatuzi wa migogoro ya kisiasa unahitaji busara kuliko nguvu ya dola ni kitendo cha juzi polisi kulazimika kumwita kuwatuliza vijana na wafuasi wa Chadema waliogoma kutoka mahakamani hadi Lema apewe dhamana.

Mbowe alihoji iwapo virungu, risasi na mabomu ya machozi ni suluhu ya matatizo kwa nini hawakutumia mbinu hizo kuwatawanya vijana wa chama hicho waliohamaki baada ya kupata taarifa za mahakama kugoma kutoa hati ya kumtoa Lema mahabusu na badala yake polisi wakamtumia kuwaondoa kwenda Viwanja vya NMC, kazi aliyoitekeleza kwa maneno matatu tu: “Makamanda twendeni NMC”

“Kutokana na mikakati ya kukidhalilisha Chadema na viongozi wake na propaganda kwamba hiki ni chama cha vurugu ili kupunguza imani ya umma kwa chama na kwamba sisi viongozi tunawachuuza wananchi na wanachama wetu kuingia kwenye matatizo, leo nitachukua uamuzi mgumu, siogopi polisi, siogopi risasi wala mabomu au kwenda magereza. Namwogopa Mungu na ninaamini katika kweli.”

Mbowe alihojiwa na Ofisa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OC-CID), Faustine Mafwele kuhusiana na madai ya viongozi wa chama hicho kutoa kauli zenye mwelekeo wa uchochezi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Jumatatu ya Novemba 7, mwaka huu.Hadi jana saa 1:00 usiku, Mbowe alikuwa kishikiliwa ofisini kwa Kamanda wa polisi wa mkoa.

Marufuku ya polisi

Kwa upande wake, Kamishna wa Operesheni Maalumu na Mafunzo, Paul Chagonja alisema polisi wamepata taarifa za kiitelijensia kwamba Chadema kinakusudia kufanya maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia leo na kusema kwamba polisi haitaruhusu shughuli hizo akidai kwamba ni baada ya kubainika kuwa zitaandamana na vurugu na uvunjifu wa amani.

“Jeshi la polisi kama taasisi ya kusimamia sheria za nchi tumepiga marufuku maandamano na mikutano hiyo ya Chadema na atakayekiuka atachukuliwa hatua kali za kisheria na kila mtu wakiwamo viongozi watawajibika kwa kosa lake,” alionya Kamishna Chagonja.
Awali, Mkuu huyo wa Mafunzo na Operesheni alikwepa kukitaja Chadema kwa jina hadi alipobanwa na waandishi wa habari. Aliwasiliana kwanza na Kamanda Sirro ambaye pia alikuwapo katika mkutano na waandishi.

“Ingawa ni haki ya kimsingi ya kikatiba na kisheria kwa vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa, lazima sheria na taratibu zifuatwe na pale tutakaporidhika na hali ya amani na usalama tutaruhusu tena mikutano na maandamano yao. Kwa sasa hapana,” alisema.

Maandamano Dar
Wakati Chagonja akipiga marufuku maandamano na mikutano ya Chadema, chama hicho kimetangaza kufanya maandamano makubwaDar es salaam kupinga hatua ya kukamatwa kwa viongozi wao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Sera na Utafiti wa chama hicho, Waitara Mwita alisema wamefikia hatua ya kuandamana baada ya viongozi wao kukamatwa na kupandishwa kizimbani mkoani Arusha.
Alisema maandamano hayo yatakayoanza saa 3:00 asubuhi yataanzia katika Ofisi za Chadema iliyopo Kimara Kona na kupitia Ubungo mataa na kumalizikia Manzese ambako kimeandaa mkutano wa hadhara.

“Tumeshatoa taarifa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, kama sheria inavyosema tutue taarifa ndani ya saa 48,” alisema Mwita
Mwita alisema wanafunzi wa vyuo vikuu wameombwa kufika kwa wingi kushirikiana na wanachama kupinga hatua ya jeshi la polisi kuwaonea kwa kuwakamata bila sababu za msingi viongozi wa chama hicho.
“Kesho(leo) hapatatosha kwani tuna imani mwitikio utakuwa mzuri. Tumeshachoka viongozi wetu kuonewa wakidai haki zao za msingi kwa niaba ya wananchi.”

Mwenyekiti wa Vijana wa chama hicho (Bavicha), John Heche alisema walishatoa tahadhari mapema kwa jeshi hilo kwamba vitisho vikiendelea maandamano yatakuwa nchi nzima akidokeza kuwa huo ni mwanzo tu.
Alisema leo maandamano hayo yatakuwa ya amani na ikiwa matatizo yao hayatatatuliwa, wataandamana mpaka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kueleza matatizo yao.

Alisema yeye na Waitara ndiyo watakaoongoza maandamano: “Hata inyeshe mvua ya mawe tutatoka na jeshi la polisi waje watulinde siyo kuturushia risasi kama kawaida yao, lakini sisi tutakuwa tayari kufa tukitetea haki za wananchi na viongozi wetu.”

Wabunge wang’aka
Wabunge jana waligeuka mbogo wakiitaka Ofisi ya Spika, kuchukua hatua kukomesha kile walichokiita unyanyasaji unaofanywa dhidi yao na polisi katika matukio ya kuwakamata wanapohusishwa na uvunjaji wa sheria.
Habari kutoka ndani ya kikao cha kutoa mwongozo kwa wabunge kuhusu Mkutano wa Tano wa Bunge kilichofanyika jana katika ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma zinasema kuwa wabunge waliochangia hoja hiyo walisema ukamataji unaofanywa na polisi kwa wabunge unaonekana kudhamiria kuwadhalilisha badala ya kusimamia sheria.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Pauline Gekul ndiye aliyeibua hoja hiyo huku akiitaka Ofisi ya Spika kuchukua hatua za kuwaondolea wabunge adha hiyo na kadri mjadala ulivyoendelea, suala hilo liliungwa mkono na wabunge wa kambi zote.
“Aliposimama Gekul kuzungumza baadhi ya wabunge walidhani kwamba pengine ni hoja ya wapinzani kuwatetea wabunge wa Chadema waliokamatwa Arusha, kwa hiyo baadhi yetu walikuwa kama wanaguna vile, lakini baadaye ilibainika kwamba kamatakatama hiyo imewakumba wabunge wote wa upinzani na wa CCM,” alisema mbunge mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Wabunge wengine waliotajwa kuzungumzia hoja hiyo ni Livingstone Lusinde wa Mtera (CCM), Murtaza Mangungu- Kilwa Kaskazini (CCM), Israel Natse- Karatu (Chadema) na Christopher Akunaay- Mbulu (Chadema).Kwa mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao walisema kwa nyakati tofauti kwamba mbunge anapotenda kosa anaweza kuarifiwa kwamba anahitajika kituo cha polisi na yeye kwenda bila kushurutishwa.

“Mbunge hawezi kutoroka au kuwakimbia polisi, dhamana aliyonayo ni kubwa kwanza wapigakura waliomchagua, Bunge kama taasisi na hata chama chake cha siasa, sasa huwezi kusema unamtafuta mbunge kama anavyoweza kumsaka mhalifu mwingine ambaye hatambuliki. Huu ni udhalilishaji,” alisema mbunge mwingine ambaye pia aliomba jina lake lihifadhiwe.Spika Anne Makinda aliahidi kuwasiliana na vyombo vya usalama ili vifuate utaratibu wakati wanapotaka kuwakamata wabunge kutokana na makosa mbalimbali wanayofanywa.

Miongoni mwa taratibu ambazo wabunge wamekuwa wakitaka zifuatwe ni Ofisi ya Spika kuarifiwa kabla ya kukamatwa na kuitwa kwenda polisi wenyewe badala yakufuatwa na idadi kubwa ya askari.

Hata hivyo, Spika aliwataka wabunge kwa upande wao kuwa makini kwa kuzingatia sheria na uhusiano mwema na vyombo vya dola ili kuepusha misuguano baina ya mihimili ya Bunge na Serikali.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment