Hivi karibuni kumeibuka mjadala juu ya ongezeko la posho za wabunge kwa karibu ya asilimia mia mbili (200%) kutoka shilingi Elfu sabini mpaka shilingi Laki Mbili.
Malipo hayo yaliyoibua mjadala baina ya wadau mbalimbali, ni yale yanayohusisha posho ya kikao cha bunge kwa siku.
Chama Cha Mapinduzi kimefuatilia kwa ukaribu suala hilo la nyongeza ya posho hiyo ya wabunge kama lilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na baadae kutolewa maelezo na Katibu wa Bunge Dokta Thomas Kashilila na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa ANNE MAKINDA.
Kwa namna suala lenyewe linavyopewa msukumo, CCM imeona si vema kuliacha bila kutoa msimamo wake kama ifuatavyo:-
i. Linapotekelezwa jambo lolote kwa kigezo cha ugumu wa maisha au kupanda kwa gharama za maisha, ni lazima jambo husika lilenge kutatua ugumu huo wa maisha kwa makundi yote katika jamii na si kwa makundi machache ndani ya jamii.
ii. Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza pengo/tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi.
iii. Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kama hayo yaliyoainishwa na Spika wa Bunge kuwa sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma, ndiko kulikosababisha hofu na mashaka miongoni mwa watanzania. Na kwakweli swali kubwa hapa inakua je, maisha yanapanda Dodoma pekeake na kwa wabunge tu?
Hivyo basi CCM inashauri kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi na jamii yetu kwa ujumla, waheshimiwa wabunge wetu na mamlaka zingine zinazohusika na swala hili, kulitafakari upya jambo hili. Tunaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafisiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo Walimu, askari, Madaktari na wengineo.
Ni muhimu ifahamike kuwa kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa wabunge kuonsha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndiyo wanaowawakilisha bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo ambalo ni hatari.
Katika hatua nyingine Chama Cha Mapinduzi Kinawapongeza sana watanzania kwa ujumnla wao, bila kujali tofauti yao, kwa kushiriki kwa amani na utulivu, maadhimisho ya miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Ushiriki wao kwa pamoja, umeyafanya maadhimisho hayo yafane sana. CCM inaamini kuwa maadhimisho haya ya miaka hamsini yatatumika kuendelea kujenga uzalendo, umoja na mshikamano wan chi yetu katika kufikia maendeleo.
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
11/12/2011
No comments:
Post a Comment