Monday, 5 December 2011

UINGEREZA YARUDISHA MABILIONI YA RADA


ZAINGIZWA KATIKA AKAUNTI YA BoT LONDON, YAAGIZA WATUHUMIWA WABURUZWE MAHAKAMANI Patricia Kimelemeta
BAADA ya vuta nikuvute ya muda mrefu kuhusu kurejeshwa fedha za ziada zilizotumika katika ununuzi wa rada, hatimaye Serikali ya Uingereza imeingiza Sh29.5 bilioni kwenye akaunti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), tawi la Uingereza kama marejesho ya fedha hizo.Uamuzi huo wa Uingereza kurejesha fedha hizo, unakwenda sambamba na ombi lake la kutaka watuhumiwa wote wa hapa nchini waliohusika na ununuzi wa rada hiyo mtumba kutoka Kampuni ya BAE Systems, washitakiwe Tanzania au Uingereza baada ya kubainika dosari kwenye ununuzi huo ambao kama ungefanyika kihalali ungehitaji Pauni 10.5 milioni, kununua rada mpya.

Akizungumza na gazeti katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, alisema fedha hizo tayari zimekabidhiwa kwa tawi hilo la BoT nchini Uingereza ili ziweze kurejeshwa nchini.

Waziri Mkulo alisema kutokana na masharti waliyopewa, Serikali imekusudia kupeleka fedha hizo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ili ziweze kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya elimu nchini.

‘’Tulikaa na kujadili namna ya matumizi ya fedha hizo kutokana na masharti tuliyopewa, jambo ambalo limesababisha tuamue kuziwasilisha Wizara ya Elimu ili kutatua changamoto zilizopo,’’ alisema Waziri Mkulo.

Aliongeza kwamba kutokana na hali hiyo, Wizara ya Elimu tayari imewasilisha mchanganuo wa matatizo yaliyopo na kiasi cha fedha zinazohitajika ili ziweze kupitishwa kwa matumizi.

Kwa mujibu wa Mkulo, kinachosubiriwa sasa ni kikao cha majadiliano kati ya wizara yake, Wizara ya Elimu, Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa Uingereza ili kuweza kupanga namna bora ya matumizi ya fedha hizo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanaamini matatizo mengi yanayoikabili Wizara ya Elimu yatapunguzwa kwa fedha hizo. Mengine yanayoweza kupatiwa ufumbuzi ni pamoja malalamiko ya madai ya walimu, uhaba wa vitendea kazi na mahitaji mengine ya wizara hiyo.

"Tulikaa na kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya elimu, jambo ambalo limetufanya tuipitishe katika matumizi ya fedha hizi, kutokana na hali hiyo tunasubiri kibali cha Ubalozi wa Uingereza ili tuweze kuzichukua na kuzitumia kama ilivyokusudiwa,’’ alisisitiza Waziri Mkulo.


Siri zaidi

Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani, kashfa nyingine imeikumba Serikali ya Tanzania ikituhumiwa kwamba ina mkakati maalumu kuzuia watuhumiwa wa ufisadi wa rada kufikishwa mahakamani.

Taarifa za mtandao wa Wikileaks ambao umekuwa ukifichua siri za kidiplomasia na ufisadi duniani, umeibua tuhuma hizo mpya kwa Serikali na kwamba hicho ndicho kikwazo cha watuhumiwa husika kutofikishwa mahakamani.

Taarifa ya mtandao huo iliyosambazwa hivi karibuni, imeeleza kuwa mpango huo ndiyo ulioathiri jitihada za aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa (DFID) Clare Shot aliyepinga BAE Systems kuizia Tanzania rada hiyo kuukuu kwa bei ghali wakati ni nchi masikini inayotegemea misaada ya wahisani.

Kwa mujibu wa mtandao huo, juhudi za Shot zilijumuisha kuinyima Tanzania misaada inayofikia Pauni 35 milioni kutokana na kununua rada hiyo kwa bei ya kuruka.

"Pamoja na shinikizo hilo, juhudi za Shot zilishindwa kabisa kuzuia ununuzi wa rada hiyo ambayo thamani yake ilikuwa Pauni 28 milioni kutoka kwa kampuni ya BAE Systems ya Uingereza," ulisema mtandao huo na kuendelea:

"Suala hilo si jipya. Gazeti la The Guardian la Uingereza liliwahi kutoa ripoti ya uchunguzi wake kuhusu uuzwaji wa rada hiyo ambao ulimsababishia pia Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, kisha Tony Blair akiwa Waziri Mkuu wa nchi aliamuru kikosi chake cha Kuchunguza Makosa Makubwa (SFO), kuingilia kati na kuchunguza namna BAE ilivyohusika."

Ilichobaini Wikileaks ni kwamba, viongozi wa Serikali ya Tanzania walikuwa wakifanya juhudi za kuficha kasoro zote zilizokuwa katika mpango wa ununuzi wa rada hiyo.

Hata kwa upande wake, mtu mahususi aliyetakiwa kushughulikia kashfa hiyo kwa kufanya uchunguzi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Takukuru), Dk Edward Hoseah alinukuliwa akimweleza Ofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini kwamba, aliwahi kutishiwa kuuawa mara kadhaa na kukumbushwa kwa ujumbe wa maneno kila siku.

BAE Systems ni kampuni kubwa ya uuzaji wa vifaa vya ulinzi ambayo iwapo ingefungiwa kufanya biashara yake, kungekuwa na athari kubwa kwa Uingereza.

Suala la uchunguzi wa aina yoyote ambao ungemweka matatani Rais wa zamani, Benjamin Mkapa na washirika wake wa karibu (kwa mujibu wa Wikileaks), lilikuwa ni gumu kuweza kufanyika.

Ulisema baada ya kumalizika kwa kipindi cha ukimya bila kushughulikiwa kwa kashfa hiyo, suala la kutafuta ufumbuzi lilionekana kuwa muhimu kwa nchi zote mbili, lakini kasoro kubwa ni pale kila aliyehusika katika kashfa hiyo ya BAE nchini Uingereza na Tanzania, kukwepa kuchunguzwa.

Hata hivyo, Blair alifanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba SFO wanafanya uchunguzi na kwamba, ikiwezekana BAE ifungiwe kufanya kazi katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Kwa upande wake, Tanzania ilikuwa ikilaumiwa kwa kufanya juhudi za kutetea ununuzi huo na hata kumtisha Mkurugenzi wa Takukuru kumtaka aachane na suala hilo.

Dk Hosseah
Mtandao wa Wikileaks ulidai kuwa Dk Hoseah, ameshindwa kuwafikisha mahakamani vigogo waliohusika na kashfa ya rada kwa sababu anahofia usalama wake.
Mbali na hofu hiyo, mtandao huo ulieleza kuwa Dk Hoseah alipewa maelekezo maalumu na Rais Kikwete, kutoshughulikia kesi za rushwa zinazowahusu vigogo katika Serikali yake na hasa marais waliomtangulia.

The Guardian lilitoa taarifa hiyo likiunukuu mtandao wa habari wa WikiLeaks uliojizolea umaarufu duniani kwa kutoa habari za kiuchunguzi hasa baada ya mwasisi wake, Julian Paul Assange, kutiwa matatani.

Akijibu hoja hizo mwaka jana, Dk Hoseah alisema ni kawaida kwake kukutana na mabalozi wa nchi mbalimbali kila mwaka na kujadiliana nao mambo mengi kuhusu Tanzania, lakini hakumbuki kuzungumza naye mambo hayo.

Alisema mabalozi ni wadau wakubwa katika bajeti ya Tanzania na hivyo huwa wanakutana kila mwaka kujadili mambo mbalimbali kuhusu kusaidia bajeti ya Serikali.

“Mimi huwa nakutana na mabalozi wa nchi mbalimbali kwa sababu wao ni wadau katika mradi wa ‘Government Budget Support’ (Mpango wa Kusaidia Bajeti ya Serikali), hivyo hilo sio tatizo,” alisema Dk Hoseah

“Msimamo wangu ni kwamba mapambao dhidi ya ufisadi ni endelevu hadi hapo tutakapofanikiwa kumaliza tatizo hili,” alisema Dk Hosea na kukiri:

“Vitisho vipo vingi tu, kutoka kwa watu wanaotuhumiwa, lakini si hata ninyi waandishi mnamwagiwa ‘tindikali’ katika mapambano yenu, hivyo hivyo hata mimi napata vitisho.”

Lakini alisisitiza kuwa pamoja na vitisho hivyo, hawezi kurudi nyuma katika mapambano ya rushwa na ufisadi.

“I’m a Tanzanian, I will die in Tanzania, it is my country’ (mimi ni Mtanzania, nitafia Tanzania, ni nchi yangu), siwezi kuhama nchi kwa vitisho vya watu wachache wanaotuhumiwa kwa ufisadi na rushwa,” alisisitiza Dk Hoseah.

Kuhusu Rais Kikwete kukwamisha mapambano ya ufisadi kama alivyonukuliwa na gazeti hilo la The Guardian, Dk Hoseah alipiga chenga kulijibu akisema:

“Ili umpeleke mtu mahakamani si lazima umtuhumu na kumfanyia uchunguzi? Lakini pia lazima tujenge utamaduni wa kuwaheshimu viongozi wetu.”

Siku hiyo, Takukuru ilituma taarifa iliyoeleza kuwa Dk Hoseah alishangazwa na Ofisa wa Ubalozi wa Marekani kumnukuu vibaya huku akisema hajui ana lengo gani.

Katika taarifa hiyo, Dk Hoseah alikiri kukutana na ofisa huyo wa Ubalozi wa Marekani ofisini kwake Julai mwaka 2007, lakini akasema ripoti ya mazungumzo yao aliyoipeleka nchini kwake imechakachuliwa.

“Kwa mfano haikutokea katika mazungumzo yetu kusema kwamba Rais Jakaya Kikwete hakutaka kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake, kuwashitaki vigogo wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi kama ilivyodaiwa na Ubalozi wa Marekani,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Uhusiano ya Takukuru.

Bunge la Uingereza
Taarifa ya mtandao huo ilikuja siku moja tangu Bunge la Uingereza liitake Serikali ya Tanzania kuwafikisha mahakamani watu wote walioshiriki mchakato wa ununuzi wa rada na kuingiza nchi katika hasara ya mabilioni ya fedha.

Kupitia Kamati yake ya Maendeleo ya Kimataifa, Bunge hilo lilisema lingependa kuona watu wote walioshiriki kwenye mchakato wa ununuzi wa rada hiyo, wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ufisadi.

Taarifa ya kamati hiyo iliyonukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), ilieleza kuwa wajumbe wake ambao ni wabunge kutoka vyama mbalimbali, watatoa ushirikiano wa dhati kwa Tanzania iwapo itaamua kuwashtaki watuhumiwa hao nchini Tanzania au Uingereza.

Wito huo wa wabunge wa Uingereza umekuja wakati tayari Kampuni ya BAE System, iliyoiuzia Tanzania rada hiyo, ikikubali kuwa kulikuwa na kasoro katika mchakato wa ununuzi wa rada hiyo, hivyo kuirudishia Tanzania Dola za Marekani 46 milioni kama fidia. 
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment