Monday 26 December 2011

WASOMALI 103 WAKAMATWA NA POLISI HANDENI

Mohammed Mhina, Handeni

Jeshi la Polisi Mkoani Tanga limewakamata watu 103 Raia wa Somalia wakiwa njiani kwenda nchini Malawi kutafuta maisha.
Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga ACP Costantin Masawe, amesema kuwa wahamiaji hao haramu wamekamatwa jana na Polisi wilayani Handeni katika maeneo mawili tofauti.
Amesema wasomali 32 walikamatwa majira ya saa 4.30 usiku huko kwenye kijiji cha Kwenjugo nje kidogo ya mji wa Handeni Chanika na wengine 71 walikamatwa saa 4.00 eneo la Vibaoni wilayani humo.
Amesema kuwa wasomali hao walikamatwa katika operesheni maalum ya kupambana na uhalifu katika kipindi hiki cha siku kuu za krismas kuelekea mwishoni mwa mwaka.
Kamanda Masawe amesema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao wa kigeni kunatokana na taarifa za kiintelijensia zilizopatikana za kuwepo kwa watu hao katika maeneo hayo.
Amesema kuwa kutokana na operesheni na ukaguzi unaofanywa na Polisi kwenye barabara kuu wasomali hao wamekuwa wakishushwa kutoka kwenye magari ya mizigo na kutembea kwa miguu maporini ili kukwepa vizuizi vya Polisi hatua ambayo Polisi waliibaini.
Hiyo ni mara ya tatu kukamatwa kwa wasomali wilayani humo katika kipindi cha kuanzia mwezi septemba mwaka huu.
Wakimbizi wengine wawili walikamatwa eneo la Kabuku na wengine 12 walikamatwa eneo la wilayani Handeni wakiwa njia kuelekea Malawi kupitia mkoa wa Morogoro.
Kamanda Masawe ametoa wito kwa wanchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwafichua wahalifu wakiwemo wahamiaji haramu.

No comments:

Post a Comment