Monday, 13 December 2010

UNAMKUMBUKA MATONYA??BADO ANATAMBA






 
matonya kazini

Ni umbali wa kilomita 48 kutoka mjini Dodoma ukifuata Barabara ya Singida.
Mita 50 pembeni mwa barabara hiyo upande wa mashariki, hapo ndipo ilipo nyumba anamoishi ombaomba maarufu nchini, Mzee Paulo Mawezi maarufu kwa jina la Matonya.

Yule Matonya aliyepata umaarufu jijini Dar es salaam na Morogoro kutokana na staili yake ya kuomba fedha kutoka kwa wapita njia. Ni Matonya aliyepata umaarufu zaidi baada ya mkuu wa zamani wa mkoa wa Dar es salaam, Yusuf Makamba kumtimua jijini na kuagiza mamlaka husika kuhakikisha haruhusiwi kuingia kwenye mipaka ya Dar es salaam.
Ni yule ambaye baada ya kutimuliwa Dar es salaam, aliibukia Morogoro ambako aliendeleza staili yake ya kuomba akiwa amelala chali huku mkono akiwa ameunyoosha juu kwa muda mredfu bila ya kutikisika hata kama jua ni kali kupita kiasi.

Kijijini, Matonya anaishi kwenye nyumba ya tembe ambayo ni mali  ya mtoto wake wa kike aitwaye Elizabeth Matonya. Nyumba hiyo ya asili ya watu wa Dodoma ipo kwenye Kijiji cha Bahi Sokoni katika Kitongoji cha Nghungugu, umbali wa kilomita 3 kutoka yalipo makao makuu ya wilaya ya Bahi.
Ilikuwa kazi ngumu kidogo kufika kwenye nyumba hiyo kwa kuwa nilikuwa nimeelekezwa kwamba makazi ya ombaomba huyo maarufu yapo katika Kijiji cha Kilimatinde wilaya ya Manyoni mkoani Singida, kumbe 'Komandoo' Matonya, kama anavyofahamika eneo hilo, alihama kijijini hapo zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Mkuu wa wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa ni sehemu ya mafanikio yangu katika kuifikia nyumba ya Matonya kwani ndiye alinielekeza kwa usahihi na hatimaye nikakifikia Kijiji cha Bahi Sokoni ambako nilimpata kwa urahisi kutokana na umaarufu wake.

Ilikuwa ni majira ya mchana, jua linawaka na hapo nikaingia kwenye nyumba iliyojengwa kienyeji (tembe) huku nikiwa nimelowa jasho na uchovu baada ya safari ndefu. Nikajikuta niko uso kwa uso na mwenyeji wangu Matonya na bila ya kuchelewa mazungumzo yetu yalianza mara moja.

Swali: Shikamoo Mzee Matonya; mbona umejificha mbali sana huku. Unataka watu wasikuone au unamuogopa Makamba asije akakukamata na kukupeleka kwenye makambi ya wazee? 
Jibu: Marahaba. Karibu sana, lakini mimi ni kiboko yao sio Makamba tu hata na wengine wananijua na wanatambua umuhimu wa mimi kuwepo katika Jiji la Dar es Salaam na Morogoro kwani ninachangamsha miji hiyo vizuri. Kwani wewe ni nani mbona unaniuliza hivyo?

(Baada ya kujitambulisha kwake, anaamuru watu wote wanaoishi katika nyumba hiyo kukusanyika na kusikiliza mazungumzo kati yangu na yeye huku akiwa ni mjanja wa kuuliza maswali ya kudadisi akitaka kujua zaidi lengo langu lilikuwa nini haswa).

Swali: Matonya hapa ni nyumbani kwako au unaishi kwa nani, na hawa unaoishi nao ni akina nani haswa; ningependa kufahamu?
Jibu: Mimi sina nyumba ila hapa ni kwa mtoto wangu wa kike anaitwa Eliza huyo hapo.....( bila ya kuona anamuonyeshea kwa mbele ingawa aliyekuwa amekaa mbele yake hakuwa Eliza. Watu wengine wananionyesha Eliza ambaye anatabasamu kidogo na kujibu kuwa ni yeye kweli.)

Swali: Ziko wapi mali zako ambazo umekuwa ukinunua kila unapotoka mjini ambako umesema kuwa huwa unakwenda kufanya kazi na huku unarudi kutumia?
Jibu:Watu wanasema kuwa nina mali, lakini ni ‘walambi’ (akimaanisha kwamba ni waongo). Mimi sina kabisa mali; hata mbuzi; hata kuku sina na wala sina mpango wa kununua tena hata kama nina pesa kwa kuwa walishazoea kuniibia, hivyo sitaki tena kuwa na mali.

Swali:Kwani walikuibia nini hadi unasema kuwa hutanunua na hicho walichokuibia kilitoka wapi?
Jibu:Nilikuwa na ng’ombe wengi sana. Kila wakati walikuwa wakiwaiba wakati ninaishi Kilimatinde na ng’ombe hao nilinunua kwa pesa yangu ya kuomba huko Dar es Salaam. Walikuwa wengi lakini waliibwa wote na ndugu zangu.

Swali: Hebu niambie hao ng’ombe walikuwa wangapi na waliibwa lini. Hao ng’ombe uliwanunua kwa muda gani?
Jibu: Mimi nilianza kuomba Dar es Salaam siku chache kabla ya Nyerere kutundika bendera yake na kushuka ile ya mkoloni (Desemba 09,1961) na kwa hiyo mimi niliingia pale kabla ya Nyerere kutawala ndiyo maana huyo Makamba wenu sitaki anihangaishe kwa kuwa hata mimi ni mtoto wa mjini. Kwa hiyo tangu wakati huo nilikuwa namaliza wakati mwingine miezi sita au mitano narudi na kila niliporudi niliweza kununua kati ya ng’ombe watatu mpaka watano na kwa mwaka mmoja niliweza kununua kati ya ng’ombe nane au 10?.

Swali: Hao ng’ombe ulikuwa ukiweka kwa nani na ulikuwa ukimlipa ujira kiasi gani ili aweze kukulindia mifugo yako?
Jibu: Ng’ombe walikuwa wakitunzwa na ndugu zangu akiwepo mdogo wangu ambaye alikuwa akiishi nyumbani kwangu Kilimatinde. Mimi nilikuwa namsaidia kila alichokuwa akikihitaji lakini baadaye walianza kunifanyia fujo na kuiba na walipoondoka nyumbani, watu wengine waliiba ng’ombe 37 ambao walikuwa ndio wa mwisho; nikachukia na kuhama huko nikaja katika kijiji cha Mpamantwa (kilomita 3 kutoka Bahi sokoni).

Swali: Kama hutaki kununua tena mifugo, pesa unazorudi nazo unafanyia kazi gani sasa?
Jibu:Nakula mimi na wakati mwingine nawapa watoto wangu nao wanakwenda kuhemea chakula ambacho tunakula wote nikiona zinakaribia kuisha, naondoka tena. Lakini nyingine zinanisaidia kununua mboga za kubadilisha nikiona nimechoka mboga zao. Kitendo cha kuibiwa na kunyanyaswa na ndugu zangu ambao wanaona kilinikera sana na nikakata tamaa ya kununua mifugo na hata kujenga nyumba ingawa uwezo huo ninao, lakini nahofia kuwa watanidhuru.

Swali: Hivi Matonya una mke au watoto na kama unao ni wangapi na wako wapi kwa sasa?
Jibu: Mke sina kwani niliachana na mke wangu wakati wa Vita ya Idd Amini na Nyerere (1978-1979) na tangu wakati huo sijaoa na sina mpango huo kwa kuwa huyo alikuwa ni mke wangu wa tatu katika maisha yangu hivyo sitaki kuoa tena.

Swali: Vipi kuhusu watoto. Una wangapi na wako wapi? Na hao watoto ni wa mke wako yupi kati ya hao watatu uliowahi kuishi nao?
Jibu:Nina watoto wawili Eliza na Ernest, huyo hapo ni Eliza na Ernest yuko Dar es Salaam ni dereva wa magari ya huko. Watoto hawa ni wa mke wangu wa mwisho ambaye yuko hapo Mpamantwa anaitwa Paulina Ngalya.
Swali: Ni lini unafikiria kustaafu kazi yako ambayo umeifanya kwa muda mrefu?
Jibu:Labla serikali inijengee nyumba nzuri hapa na inipe mtu wa kunitunza au hata wakijenga nyumba nzuri kwa mtoto wangu halafu wanisaidie na chakula pamoja na chai ya kila siku, mimi naweza kustaafu kazi yangu lakini bila ya kufanya hivyo kazi yangu nitakufa nayo.

Matonya anasema kuwa amekuwa akipata kati ya Sh50,000 hadi 100,000 kwa mwezi na mara nyingi anarudi kijijini kila baada ya miezi miwili au mitatu tangu alipoanz`a kazi hiyo mwaka 1961.
Kurudi kwake nyumbani kunasukumwa na woga kuwa akikaa muda mrefu watu wanaweza kumvamia na kumnyang’anya fedha ambazo anakuwa ameshadunduliza, lakini pia anasema amekuwa akikumbuka sana mazingira ya nyumbani, hasa chakula cha asili ukiwemo ugali na mlenda.
Kuhusu sababu za kufanya kazi yake ya kuomba jijini Dar es salaam na Morogoro badala ya mkoa wake wa Dodoma, Matonya anasema: “Siwezi kuomba Dodoma kwa kuwa bado ni mji mdogo sana tena hauna wazungu ambao wanaweza kunipa hata Sh 1,000 kwa mara moja. Matajiri wa Dodoma ni wachoyo sana; wanatoa Sh50 au Sh100, sasa mtu si unaweza kufa kwa njaa.”
Kuhusu miji ya Dar es Salaam na Morogoro, Matonya anasema kuwa Dar ni kuzuri kuliko Morogoro kwa kuwa kipato cha Morogoro ni Kati ya Sh4,000 na Sh5,000 kwa siku wakati Dar ni kati ya Sh5,000 hadi Sh7,000 kwa siku na chakula cha Dar es Salaam bei ndogo kuliko mahali pengine lakini pia anasifia kwa usafi kuwa hawezi kupata Kipindupindu.
“Lakini hata hapa nina maandalizi ya kwenda Dar es Salaam ili nikale Sikukuu ya Krismasi huko kwa kuwa kule kunakuwa kumechangamka zaidi ya maeneo mengine na wakati huo pesa zinakuwa ni nyingi," anasema Matonya.

Kuhusu nani amekuwa akimpeleka huko, Matonya anasema: “Sina shida kwa kuwa ninaporudi na pesa zangu baadhi huwa za kula na nyingine za nauli. Huwa naweka ambazo nikishuka naweza kukodisha gari inanipeleka mahali ambapo napataka mimi na ninafika huko nikiwa na pesa za kula angalau siku moja au mbili lakini nakumbuka nauli yangu ya kwanza miaka hiyo (1961) nilikopa kwa ndugu yangu mmoja wa Kintinku sasa hivi sitaki kukopa tena.”
Elizabeth, 36, mtoto wa kwanza wa Mzee Matonya, anasema kuwa walipokuwa wadogo walishuhudia baba yao akiwa na ng’ombe wengi, lakini wote walikwisha wakati wao wakiwa wadogo.

Kuhusu maisha ya baba yake ya kuomba, Eliza anasema hata kama angefungwa kwa minyororo ya chuma bado angeondoka na kwenda kuomba kwa kuwa ndiyo maisha yake waliyomkuta nayo wakati wanazaliwa.
“Sisi hatumuwezi kwa kuwa nimekuwa nikimlazimisha kukaa nyumbani kutokana na umri wake kuwa mkubwa, lakini anakataa na wakati mwingine ananitukana kwa hiyo nilishamuacha."

Kuhusu maisha ya kaka yake anayeishi Jijini Dar es Salaam, anasema 'mambo yake sio mabaya' ingawa anapingana na kauli ya baba yake kwa kusema kuwa sio dereva bali siku za nyuma aliwahi kufanya kazi katika magari ya abiria, lakini kwa saa hajui anafanya kazi gani.
Alisema ana mke na watoto watatu.
Anasema sababu kubwa inayomkimbiza baba yake kijijini ni kutaka kunywa chai kila wakati na anapokosa kutokana na ugumu wa maisha ya kijiji, inakuwa ni tabu kwake.

Mwenyekiti wa mtaa, Adam Mwalami anasema kuwa amekuwa akimuona Matonya akirudi nyumbani zaidi ya mara tatu kwa mwaka na kila anaporudi amekuwa ni mmoja wa wazee wasio na tabu katika maisha ya kawaida ingawa anasema ni mkorofi anapobaini kuwa haki haikutendeka kwa jambo linalomhusu.
Naye mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mkwasa anakiri kuwa dereva wake amekuwa akimrudisha mara kadhaa kila anapokuwa ametimuliwa huko jijini na kwamba kila anaporudishwa hukabidhiwa kwa mtoto wake wa kike, lakini baada ya siku kadhaa huondoka tena.
===========================================
DONDOO KUHUSU MATONYA

Jina lake halisi ni Paulo Mawezi
Jina Matonya ni la utotoni
Ni mume wa wake watatu
Ni baba wa watoto wawili, Elizabeth na Ernest
Aliishi Kilimatinde, Singida miaka 30 iliyopita
Sasa ni mkazi wa Bahi Sokoni, Dodoma
Alianza 'kazi' ya ombaomba kabla ya uhuru
Hukusanya kati ya sh 4000 na 7000 kwa siku
Alitoroka kambini Moro, akapandishwa kizimbani
Kuila Krisimas 2010 jijini Dar es Salaam

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment