Thursday, 7 July 2011

Dk Slaa amwanika Chenge sakata la rada


 Send to a friend
Thursday, 07 July 2011 00:07
0diggsdigg
Geofrey Nyang’oro, Dar na Leo Bahati, Dodoma
SIKU moja baada ya Serikali kumkingia kifua Mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), Andrew Chenge ili asishtakiwe kwa rushwa katika mchakato wa ununuzi ya rada, Chadema imeweka hadharani kurasa 11 za ushahidi inaodai kuwa unaweza kumtia hatiani Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani wa Serikali kama atashtakiwa.Ushahidi huo uliotolewa jana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, ni ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Shirika la Upelelezi la Makosa Makubwa ya  Jinai la Nchini Uingereza (SFO).

Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa amefikia hatua hiyo baada ya kusikitishwa na majibu ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe kuhusu suala hilo alipokuwa akijibu hoja za wabunge.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, ukurasa wa tano wa ripoti hiyo, unaeleza jinsi Chenge alivyoshinikiza utekelezwaji wa mkataba huo na namna alivyofaidika kwa malipo ya kitita cha Dola 1.5 milioni kupitia akaunti ya Benki ya Barclays iliyoko katika kisiwa cha Jersey nchini Uingereza.

"Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kati ya mwaka 1995 na 2006. Katika kipindi hicho, BAE na SPS walikuwa wakifanya majadiliano ya ununuzi wa rada kwa ajili ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na Chenge alihusika moja kwa moja katika mchakato huo hasa kushinikiza ununuzi huo," alisema Dk Slaa akinukuu waraka huo alioutoa pia kwa waandishi wa habari.

Aliendelea,"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ilitakiwa kutoa maoni na kuthibitisha malipo hayo na bila Chenge kukubali, kusingeweza kufanyika chochote."

Kwa mujibu wa Dk Slaa, kauli ya Waziri Chikawe kuwa serikali haina ushahidi unaowataja watuhumiwa wa kashfa ya rada moja kwa moja na kutaka mwenye ushahidi wauwasilishe kwake, ni hatari kwa kuwa inaonyesha kuwa haina dhamira ya kweli ya kushughulikia rushwa na ufisadi huo.

Alisema ripoti hiyo ya SFO, ambayo anaamini Serikali inayo, ni ushahidi tosha unaoweza kumtia hatiani Chenge ambaye pia angeweza kusaidia kutaja wahusika wengine katika sakata hilo.

Alisema ushahidi huo huo ambao hata Mbunge wa sasa kupitia Chadema Tundu Lisu aliyeibua hoja hiyo upo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kusisitiza kuwa kama Serikali haina taarifa hiyo, ilipaswa kumwajibisha Mwanasheria wake na si kusafisha watuhumiwa wa ufisadi.

“Kinachofanywa sasa ni mpango wa makusudi wa Serikali ya CCM ambayo imeanza taratibu ya kuwasafisha watuhumiwa wa ufisadi  kabla ya kufanyika kwa vikao vya chama hicho,”alisema Dk Slaa.

Dk Slaa alikemea hilo na kusisitiza kuwa  chama chake hakitalala bali kitatoka nje ya Bunge na kuendelea na maandamano ya kuelimisha Watanzania kuhusu suala hilo hadi hapo mafisadi wote watakapofikishwa mahakamani.

Kuhusu uhusika wa Chenge, alisema uchunguzi wa SFO  umemwingiza moja kwa moja katika sakata hilo kwa sababu katika kipindi hicho, yeye (Chenge), alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Katika sakata hilo, Chenge anaingia moja kwa moja kwa sababu makubaliano yoyote katika mkataba huo, alikuwa ndiye mwenye uamuzi wa mwisho,”alisema Dk Slaa huku akinukuu ripoti ya SFO.

“Wakati suala la uuzwaji wa rada kutoka BAE kwa  Serikali ya Tanzania likifikia ukingoni kati ya mwaka  1996/7, Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ni katika kipindi hiki ndipo Kampuni ya  Franton Investment Ltd inayomilikiwa na Chenge ilipoingiziwa Sh1.5 milioni katika Benki ya Barclays katika visiwa vya Jersey,”alisema Dk Slaa.


Lissu: Chenge akishtakiwa hatoki

Kutoka Dodoma, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tindu Lissu amesema iwapo Watanzania wataamua kumshitaki Chenge, atatiwa hatiani mara moja kwa sababu ushahidi uliopo hawezi kuukabili.

Lakini akasema tatizo ni Serikali kumkingia kifua ili asishtakiwe ingawa wao kama wabunge wa upinzani, wataendelea kupambana naye nje ya Bunge kwa kutumia majukwaa ya kisiasa ili umma wa Watanzania utoe hukumu.

Mbunge wa CCM achukizwa kauli ya Chikawe

Wakati Lissu akisema hayo, Ally Mohamed (Nkasi Kaskazini-CCM), alisema juzi hakupata usingizi kutokana na hasira alizopata baada ya kuchukizwa na kauli ya Chikawe kuwa Serikali haina ushahidi wa kumshtaki Chenge.

Wakati akifanya majumuisho wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mahusiano na Uratibu, Chikawe alisema uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) unaonyesha hakuna Mtanzania aliyehusika na ufisadi wa ununuzi wa rada isipokuwa Waingereza watatu.

Licha ya Lissu kusema kuwa SFO iliwasilisha serikalini ushahidi kuwa Chenge alihusika na ufisadi huo, Chikawe alisema wao hawana na kumtaka apeleke ushahidi huo ili wautumie kumshitaki.

Lakini jana Lissu alisema hana haja ya kuwapelekea ushahidi alio nao kwa sababu anatambua wazi hicho ni kiini macho.

Alisema kwamba anatambua wazi kuwa barua hiyo ya SFO, Serikali inayo.

"Barua hiyo mimi nimeipata kutoka huko serikalini, wao wanasema niwapelekee, siwezi kufanya upumbavu wa namna hiyo," alisema Lissu akisisitiza:

"Limeshindikana hapa bungeni kwa sababu Serikali inamkingia kifua. Sisi hatuna haja ya kuendelea kujisumbua. Sasa tumeamua tutaingia mitaani maana huko ndiko waliko walioumia kutokana na ufisadi huo," alisema Lissu.

"Lakini kwa hakika leo hii Chenge akifikishwa mahakamani ni kitanzi tu," alidai Lissu ambaye ana taaluma ya sheria akimanisha kuwa ushahidi wa SFO unaweza kumtia hatiani.

Kuhusu kuwepo kwa ushahidi unaotosheleza, Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuwa barua hiyo iliyoandikwa na SFO kwenda kwa Mwanasheria wa Serikali Machi 21, 2008, inaonyesha wazi jinsi fedha zilivyolipwa kwenye akaunti ya Chenge iliyopo katika kisiwa cha Jessy.

Alidai pia kuwa barua hiyo iliyosainiwa na Msimamizi wa Kesi za SFO, Mathew Cowie ilieleza jinsi sehemu ya fedha hizo zilivyotolewa na kupewa mtu mwingine anayefahamika kwa jina la Idriss Rashid.

Alifafanua kuwa kwa sheria za sasa za Takukuru, zinaweza kumtia hatiani Chenge kwa sababu zinasema kuwa uamuzi wowote uliofanywa na kiongozi wa Serikali wenye dalili inayoashiria kutokuwepo kwa maslahi ya umma, ni kosa litakalohesabika kuwa ni rushwa.

Akasema barua ya SFO inaonyesha kuwa kulikuwapo na mkakati ambao ulifanywa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo wa kuingia mkataba na benki iliyotoa fedha hizo kuwa tatizo lolote litalakalotokea, halipaswi kushughulikiwa kwa namna yoyote na Serikali ya Tanzania bali ya Uingereza.


Chikawe alimkingia kifua Chenge muda mfupi tu baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kukabidhiwa ripoti  inayolitaka Bunge kuishauri Serikali iwashitaki wote waliohusika na kashfa hiyo ya rada.

Ripoti hiyo ilitolewa na timu maalumu ya wabunge wanne, iliyoongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai ikitoa pendekezo hilo baada ya kubaini kuwa kwenye sakata hilo kuna ufisadi wa kutisha.

Chenge asema apelekwe
kwa Takukuru, DPP

Alipotafutwa na gazeti hili ili azungumzie tuhuma hizo jana, Chenge alihoji "kwanini watu wazunguuke? Kama wana ushahidi ni vema wakaupeleka Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) halafu wao wataniita."

Chenge maarufu kama mzee wa vijisenti, alisema anashangazwa na watu ambao wamekuwa wakizunguka huku na kule kushikia bango jambo ambalo tayari limekwishafanyiwa uchunguzi na kutolewa maamuzi.

"DPP pia yupo na Takukuru, wakipeleka huko mimi si nitaitwa? Wapeleke tu nyaraka zao. Maana mimi napenda watu wenye uwezo wa kuthubutu..., hilo jambo limekwishaelezwa jana (juzi) na Waziri Chikawe, sasa hizo nyaraka mpya sijaziona na kama zipo wazipelekea mamlaka husika," alisisitiza.

Akionyesha msisitizo, Chenge alisema kama nyaraka hizo zinazoonyeshwa sasa ni zile za mwaka 2007, itakuwa sawa na kuwafanya Watanzania watu wasiojua kufikiri vema kwani nyaraka hizo ndizo zilizochunguzwa na kubainika hakuna kitu chochote kuhusu yeye.

"Tujielekeze katika mambo ya msingi tuache kuwahadaa Watanzania. Kama nyaraka zenyewe unazosema wanazo hao waliozitoa ni za mwaka 2007, basi huko ni kuhadaa Watanzania," alisema Chenge na kuongeza:

Uchunguzi una msingi wake, na ukishafanyika majibu yake huambatana na msingi wa jambo lenyewe..., nasema tena, hili jambo limekwishachunguzwa na hao SFO."

chanzo.mwananchi

No comments:

Post a Comment