Thursday, 21 July 2011

PINDA ASEMA HATIMA YA JAIRO IKO KWA RAIS

Rais Jakaya Kikwete.
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameyaweka hadharani maagizo aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete kuhusu tuhuma za rushwa zinazomkabili Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo akisema amemwambia kwamba atashughulikia suala hilo yeye mwenyewe atakapotoka ziarani Afrika Kusini.

Juzi, Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za kila siku za Serikali bungeni, aliliambia gazeti hili kwamba alipewa maagizo na Rais juu ya kushughulikia tuhuma za kutenga zaidi ya Sh moja bilioni, kwa ajili ya kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara yake.

Hata hivyo, jana alipoulizwa nje ya ukumbi wa Bunge kuhusu maelekezo hayo ya Rais, Pinda, alijibu: "Mheshimiwa Rais amesema atakuja kulishughulikia akirudi."

Pinda ambaye siku ya tukio hilo alionekana kuhamaki bungeni na kusema kwamba kama angekuwa na mamlaka angemfukuza kazi Jairo, jana alionekana mwenye subira huku akisisitiza kuwa: "suala hilo halina uharaka."

Tuhuma dhidi ya Jairo ziliibuliwa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo ambaye alisema mtendaji huyo mkuu wa wizara alitoa dokezo kwa taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo kutoa Sh50 milioni ili kufanikisha bajeti kupita bungeni hatua ambayo iliibua hasira miongoni mwa wabunge hasa ikizingatiwa hali ya nishati ya umeme ilivyo kwa sasa nchini.

Shellukindo katika tuhuma zake alisema, Jairo aliziandikia barua idara na taasisi hizo akiziagiza ziweke fedha hizo kwenye akaunti namba 5051000068 inayomilikiwa na Geological Survey of Tanzania (GST) kwenye Benki ya NMB, Tawi la Dodoma.

Kabla ya ufafanuzi huo wa Pinda, jana mchana kulikuwa na tetesi zilizozagaa katika jiji la Dar es Salaam na baadhi ya mitandao ya intaneti zikidai kwamba Jairo ameandika barua ya kuomba kujiuzulu. Akizungumzia tetesi hizo Pinda alisema: "Sina taarifa hizo," na kuongeza Pinda na kukiri kwamba hata yeye amezipata lakini haelewi chochote kuhusiana na hilo.

Jumatatu wiki hii, baada ya Shellukindo kuibua tuhuma hizo bungeni, Pinda aliahidi kuwa angewasiliana na Rais siku hiyo baada ya kutua kutoka kwenye ndege kwa ajili ya kumchukulia hatua za kinidhamu... "Kwa jinsi jambo hili lilivyokaa, hakuna jinsi mtu unavyoweza kulitetea hata kidogo, nilitamani sana kwamba nije hapa niseme kwamba uamuzi wangu mimi ni huu, lakini haikuwezekana.

Kwa dhati kabisa naomba wabunge tuwe na subira, mara tu mheshimiwa Rais atakapotua South Africa (Afrika Kusini) jioni ya leo (juzi), nitamwarifu na ninaamini tutaelewana kuhusu hatua za kuchukua.

Hata hivyo, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema haijui chochote kuhusu mawasiliano hayo ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda, kuhusu hatua za kushughulikia jambo hilo. Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga alisema hadi jana mchana, kurugenzi hiyo haikuwa na taarifa yoyote juu ya tuhuma zinazomhusu Jairo wala mawasiliano baina ya Waziri Mkuu na Rais.“Kama (Waziri Mkuu Pinda kumpigia Rais Kikwete), atakuwa amempigia siyo lazima sisi tujue,” alifafanua  Kibanga.

Chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment