Frederick Katulanda, Mwanza
ABIRIA 16 wamefariki dunia na wengine 120 wamenusurika baada ya mabasi mawili kugongana mkoani Shinyanga.Mabasi hayo yaligongana jana asubuhi katika Kijiji cha Kibingo, Kata ya Nyamigota wilayani Geita, moja likitokea Musoma kwenda Bukoba na jingine Mwanza likielekea Biharamulo. Kati ya abiria hao 120 walionusurika, zaidi ya 60 walipata majeraha. Taarifa zilizopatikana kutoka wilayani Geita na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Philemon Shelutete na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Abdalah Dihenga zimeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea saa 3:20 asubuhi. Akizungumza kwa simu jana, Shelutete aliyataja mabasi hayo kuwa ni la Kampuni ya Mabasi ya Bunda lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Bukoba na basi la Sheratoni ambalo lilikuwa likitokea Biharamulo kwenda Bukombe.Shelutete alidai kuwa ajali hiyo ilitokea kwa uzembe baada ya dereva wa basi la Sheratoni kulazimisha kulipita roli aina ya Fuso mali ya kampuni ya vinywaji baridi Nyanza Bottling Ltd ya jijini Mwanza, ndipo likagongana na basi la kampuni ya Bunda. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Nonosius Komba alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kwamba wakati huo alikuwa akielekea eneo la tukio. Dk Dihenga alisema awali walipokea maiti za watu wanane na kwamba hadi kufikia saa 7:00 mchana walikuwa na maiti 16. "Mpaka sasa tuna idadi kubwa ya majeruhi wa ajali hiyo, wanaendelea kutibiwa na madaktari wetu, lakini kati yao majeruhi sita hali zao ni mbaya hivyo tumelazimika kuwakimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi na wengine tumewahamishia Hospitali Teule ya Sengerema kwa matibabu," alisema Dk Dihenga. mwananchi |
Wednesday, 18 May 2011
16 WAMEKUFA KATIKA AJALI NYINGINE GEITA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment