Monday, 30 May 2011

DK SLAA ACHAFUA HEWA UCHAGUZI CHADEMA


BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha), limepata viongozi wapya katika uchaguzi uliotawaliwa na mizengwe na vurugu zilizotishia usalama wa wapigakura.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa, vurugu hizo zilichochewa na kitendo cha Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa (pichani) kuonyesha visu alivyodai kuwa vilikamatwa na walinzi wa chama hicho jana asubuhi.

Mbali na kuonyesha visu kadhaa, Dk Slaa alitangaza kuenguliwa kwa wagombea watatu wa nafasi ya uenyekiti; Bernard Saanane, Greyson Nyakarungu na Mtela Mwampamba kwa madai ya ukiukaji wa maadili.

Dk Slaa aliwaeleza wapigakura kuwa kamati ya ulinzi ya chama hicho pia ilibaini kuwapo kwa mabaunsa waliodaiwa kupandikizwa katika mkutano huo kwa lengo la kuuvuruga.Alisema watu hao waliletwa na baadhi ya wagombea wa nafasi za uongozi ambao kimsingi chama hicho kilikuwa kimebaini kuwa ni mamluki waliopandikizwa kwa lengo la kuvuruga uchaguzi huo. Kuhusu wagombea walioenguliwa, Dk Slaa alidai kuwa kuondolewa kwao kumetokana na kukiuka maadili.

Baadhi yao ndani ya mkutano huo walionyesha huzuni kutokana na uamuzi huo uliodaiwa kuwa ni mgumu kuwahi kufanyika katika vyama vya siasa.“Ingawa chama kinasema kimechukua hatua hiyo kwa malengo mahususi, mimi bado ninapata shaka kama kweli hakuna mgombea ambaye hajafanya kampeni kabla ya wakati,” alisema mjumbe mmoja kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Hata hivyo, matokea ya uchaguzi huo yaliyotangazwa saa 12 asubuhi jana na Dk Slaa baada ya kukamilika kwa shughuli ya kuhesabu kura iliyofanyika usiku kucha. Akitangaza uamuzi huo uliochafua hali ya hewa ndani ya ukumbi wa mkutano saa tano usiku juzi, Dk Slaa alisema uamuzi huo ulifikiwa na kamati ya uchaguzi iliyoundwa na watu sita  ikiongozwa na yeye.Akifafanua sababu za kuenguliwa kwa wagombea hao, Dk Slaa alisema inatokana na wao kujihusisha na vitendo vya ukiukaji wa maadili ya chama hicho kwa kupiga kampeni kabla ya muda uliopangwa.

“Nafasi mnayowania ni kubwa na ina umuhimu wake kwa taifa. Kwa kuwa sisi sera yetu kubwa ni kupinga vitendo vya ufisadi na kusimamia maadili hatuwezi hata siku moja kuruhusu vitendo vya ukiukwaji wa maadili kufanyika ndani ya chama chetu,”alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Tulikubaliana kuwa kampeni zitapigwa ndani ya ukumbi wa mkutano, lakini wapo wagombea wamekiuka agizo hilo na kupiga kampeni kabla ya muda. Tunao ushahidi kuwa wapo waliofanya hivyo katika maeneo ya Kinondoni, Manzese na hata jana (juzi) makao makuu,”alisema Dk Slaa.

Chadema imara
Alisema Chadema siyo chama cha makundi bali ni cha watu wote chenye dhamira ya kulikomboa taifa na kusisitiza kuwa kitaendelea kuchukua hatua kila kinapobaini kuna sababu za kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa Dk, Saanane alitajwa na wajumbe wanane wa mkutano huo kuhusika na vikao vya siri, mara nane katika kukigawa chama kimakundi na mara tatu alitajwa kutaka kujitoa baada ya kuingia ukumbini. Mgombea mwingine aliyekuwa na tuhuma kama hizo ni Nyakarungu ambaye naye alitajwa na wajumbe wanane akidaiwa kufanya vikao vya siri mara nane, kukigawa chama katika makundi na mara tatu kuhusika na vitendo vya rushwa.

Kuhusu Mwampamba alisema yeye alikataa tuhuma zote zilizokuwa zimeelekezwa kwake, lakini baadaye alikiri jambo lililofanya kamati hiyo kuona kuwa ni mwongo na hafai kuwa kiongozi. Katibu huyo mkuu alisema Chadema inachukua hatua hizo kwa vitendo ili kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo suala la maadili ya viongozi na kupinga kwa nguvu zote vita dhidi ya ufisadi.

“Sisi (Chadema) tunajinadi kupambana na vitendo vya ufisadi, sera yetu tunayosimamia ni maadili, katika kutekeleza hilo kwa vitendo ni lazima tuanzie ndani na ndipo tutoke nje,”alisema Dk Slaa.
Baada ya maelezo hayo, Dk Slaa alimtangaza John Heche kuwa mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa Bavicha baada ya kuwabwaga wapinzani wake watano.

Alisema Heche aliibuka mshindi kwa kura 143 sawa na asilimia 53.6 kati ya kura zote 239 zilizopigwa. Heche alishinda nafasi hiyo ya uenyekiti ambayo ataishika kwa miaka miwili.Awali, ilikuwa ikiongozwa na kamati ya muda chini ya mbunge wa Ubungo, John Mnyika kufuatia kuvunjika kwa mkutano mkuu wa uchaguzi mwaka 2009.

Wagombea wengine wa nafasi ya mwenyekiti waliopambana na Heche ni Aidan Sadick, Bernard Mao, Deogratius Kisandu, Edwin Soko na Masoud Suleman.

Dk Slaa pia aliwatangaza Juliana Shonza kuwa mshindi wa nafasi ya makamu  mwenyekiti (Bara) na Sharifa Suleiman Hamisi kwa nafasi hiyo Zanzibar.Walioshinda ujumbe wa baraza kuu ni Edward Kinabo, Frank Fumpa, Zainab Mussa Bakari na Alex Mushi. Uchaguzi huo wa Bavicha umefanyika baada ya kushindikana Septemba mwaka 2010, kufuatia vurugu ambapo uongozi wa Chadema ulilazimika kuusimamisha.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment