Monday, 16 May 2011

Ufisadi wa Sh48 bilioni waitikisa nchi

UFISADI unaoonyesha kuwa zaidi ya Sh48 bilioni zimetafunwa na wajanja umeendelea kulitikisa taifa baada ya kampuni za kigeni kufungua kesi zikidai fidia ya Sh3 trilioni za fidia kutoka kwa wanunuzi wa pamba kwa kushindwa kutimiza masharti ya mkataba.Madai hayo mapya yanakuja wakati serikali ilitoa fedha katika utaratibu wa mpango wa kuhuisha uchumi (stimulus package) na Bunge lilipitisha bajeti ya dharura ya Sh1.7 trilioni.

Akizungumza kutoka Mbinga jana, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha alisema kuwapo kwa kesi hiyo kunadhihirisha kwamba taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwamba kuna zaidi ya Sh48 bilioni ambazo ameshindwa kuzithibitisha kama zilitoka kwa taratibu zinazotakiwa ni sahihi.

Kabwe alitoa kauli hiyo akirejea habari iliyotolewa jana na gazeti dada la Mwananchi, The Sunday Citizen kuwa sekta ya pamba nchini inaweza kuanguka baada ya wanunuzi wa nje kudai fidia ya dola 2 bilioni sawa na Sh3 trilioni kutokana na kuvunjwa kwa mkataba.

Aprili 15 mwaka huu, Zitto aliibua madai hayo ya ufisadi huo wa zaidi ya Sh 48 bilioni alipombana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika kipindi cha maswali na majibu bungeni. Alisema kwa mujibu wa taarifa ya CAG, fedha hizo zilipotea katika utaratibu wa mpango wa kuhuisha uchumi (stimulus package).

Kutokana na ushuhuda huo, Kabwe aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na CAG kufanya uchunguzi wa kina kwenye matumizi ya fedha za mpango wa kuhuisha uchumi.“Tunataka majibu kabla ya kikao cha bajeti kwa sababu kama nilivyosema awali, hizi ni fedha nyingi,” alisema Kabwe.

Zitto alisema kwamba serikali ilimnyima taarifa muhimu ikiwamo orodha ya watu na kampuni ambazo zilifaidika na mpango huo wa matumizi ya Sh48 bilioni na kwamba kesi iliyofunguliwa sasa ni uthibitisho kwamba wafanyabiashara wa pamba walikuwa hawapaswi kufidiwa kwa sababu hawakupata hasara yoyote kama inavyodaiwa.

Alisema kesi hiyo inaonyesha kwamba wafanyabiashara wanauza bidhaa zao katika masoko ambayo yana faida kubwa.Gazeti la Sunday Citizen, jana liliripoti kuwa wasindikaji na wauzaji waliingia mkataba wa kusafirisha tani 260,000 za pamba lakini walisafirisha tani 162,000 tu ikiwa ni sawa ni asilimia 62 ya kiasi walichokubaliana.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mutunga alisema baadhi ya kampuni za kigeni zilifungua kesi kwa Liverpool Cotton Association (LCA) ambalo ni Shirikisho mama zikidai fidia kwa kushindwa kutimiziwa mkataba kama ilivyokubaliwa.

Mutunga alisema kushindwa kwa wanunuzi hao wa pamba kutimiza masharti ya mkataba, kulisababishwa na sababu zilizo nje ya uwezo wa wasafirishaji pamba wa ndani na wa nje kama vile hali mbaya ya hewa, usimamizi mbovu wa mfumo wa vocha za malipo kwa wakulima na hali mbaya ya uchumi ulimwenguni mwaka 2008 ambayo ilisabaisha bei ya pamba duniani kuwa chini pamoja na kuvurugika kwa uzalishaji wa ndani.

Wakili wa kampuni ya uwakili ya Matata ya Mwanza, Chama Matata anayewatetea baadhi ya wanunuzi wanaosafirisha pamba nje alisema suala hilo lilifikishwa LCA sababu mamlaka yake na hukumu ndiyo pekee zinazotambuliwa na mikataba hiyo.

Ingawa Sheria Nambari 225 ya LCA haitambui kushindwa kutekelezwa kwa mkataba kwa visingizio mbalimbali vikiwamo majanga ya asili, hiyo ina maana kuwa mzigo wote wa lawama unawaangukia wanunuzi suala lililowaingiza wanunuzi hao katika matata.

Mbowe ajibu tuhuma za ukabila
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kuwa hakuna chama cha siasa kinachoweza kutawala kwa dini moja Tanzania hivyo CCM kiache kuwadanganya wananchi kuwa viko vyama vya udini na ukabila nchini.

Akihutubia wananchi wa Tunduru katika Uwanja wa Baraza la Iddi, Mbowe alisema kuwa CCM na CUF vimekuwa vikihubiri kuwa Chadema ni chama cha kidini na kikabila kitu ambacho hakimo na wabunge wa chama hicho wanadhihirisha hilo.

Mbowe alisema kuwa vyama hivyo vinataka kuwagawa wananchi kwa udini na ukabila wakati wananchi wote ni wamoja na wanachohitaji ni maendeleo.

"Msidanganywe ndugu zangu. Tunachotaka ni maendeleo, inashangaza kiongozi mkubwa anatoka na kusema kuwa Chadema ni chama cha Wachaga, hakuna kitu kama hicho kwa kuwa haitatokea nchi ikatawalika kwa kabila moja na dini moja," alisema Mbowe.

Alisema kuwa inashangaza kuona kuwa wananchi wanalishwa sumu ya udini na ukabila na kusahau matatizo yao wakati hao wanaotoa sumu hiyo maisha yao ni bora na watoto wao wanakula vizuri na kusoma kwa raha.

Mbowe alisema Mkoa wa Ruvuma ambao Tunduru imo, wanawachelewesha Watanzania kwenye maendeleo kwa kuendekeza ushabiki wa kisiasa, udini na ukabila kitu ambacho kinahatarisha maendeleo yao na Watanzania kwa ujumla.

"Leo nitawaambia na muachane na tabia hiyo. Asilimia 86 ya wakazi wa Ruvuma hawajawahi kutumia umeme, amkeni mnawachelewesha wenzenu katika maendeleo ambayo yako mbele yenu," alisema Mbowe.

Alisema Chadema kitapambana kwa kuwa CCM kimewanyima umeme, barabara, maji na maendeleo mengine kwa kufanyia kazi matumbo yao na ndugu zao."Wana-Tunduru mna shida sana. Hata watoto wenu wana hali ngumu hasa kwenye elimu, barabara na tutawasaidia kwa kupambana ndani na nje ya bunge," alisema.

Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere aliwaambia wananchi wa Tunduru kuwa udini ambao wamekuwa wakidanganywa nao, utawasababishia umaskini kadri siku zinavyozidi kwenda."Mimi nashangaa kwa nini mnadanganyika kiasi hiki, tuungane tupambane pamoja kufikia maendeleo kama nchi za wenzetu," alisema Nyerere.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha aliwalaani viongozi wa dini wanaohubiri udini na ukabila wa vyama: "Udini, ukabila wa nini jamani? Sisi ni maskini halafu bado tunasikiliza ya hao!"

mwananchi

No comments:

Post a Comment