Friday, 20 May 2011

ZITO ATAKA NGELEJA AACHIE NGAZI

 Send to a friend
Thursday, 19 May 2011 22:39

NAIBU Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kuachia ngazi kwa kuwa tangu amekaa kwenye wizara hiyo, mgao wa umeme umekuwa kitu cha kawaida na kusababisha uchumi wa taifa kuporopoka kwa kasi.
Alisema kuwa waziri huyo amekuwa sasa ni waziri wa mgawo badala ya kuwa waziri ambaye angewasaidia wananchi kuondokana na adha ya umeme unaowawezesha vijana na watu wote kufanya kazi.
"Huyu si waziri na hafai kwa kuwa mgawo kila siku saa 16 kukosa umeme ni hatari kwa makampuni, wafanyabiashara na wananchi kwa jumla,"alisema Zitto na kuongeza:
"Umeme wa mwaka huu kutoka Januari hadi Mei, umeikosesha Serikali kiasi cha Sh850 bilioni. Mwaka 2006 mgawo uliozaa Richmond ulisababisha uchumi kushuka kwa asilimia moja, kitu ambacho ni hatari,"alisema.
Kauli ya Zitto imekuja wakati Tanesco ikiwa umetangaza kuanza kwa mgawo wa umeme ambao ulianza jana na utaendelea kwa wiki kadhaa zijazo. Mgawo huo wa umeme unaelezwa kwamba utakuwa unadumu kwa saa 16 kwa siku na hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi.
Alisema kuwa aliposema kuwa Serikali haina fedha hivi karibuni alishambuliwa na viongozi wa Serikali, lakini taarifa yake imewaamsha kwani Serikali na kutaka mishahara iwe inalipwa tarehe 25 ya kila mwezi.
"Nimeambiwa Wizara ya Fedha na Uchumi imewaagiza wakuu wote wa Serikali kuwa ikifika kila tarehe 25 ya mwezi lazima wafanyakazi wawe wamelipwa la sivyo watawajibishwa,"
"Tumekwenda vijijini kabisa ambapo raia wa nchi hii wanaishi pamoja na wakulima ambao ni uti wa mgongo wa taifa, lakini hali zao ni mbaya na Serikali inaendelea kuwakandamiza wananchi hao na hawana pa kusemea,"alisema Zitto.
Mbowe na mauaji Tarime
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitoa tamko la chama kuhusu mauaji ya Tarime akieleza kuwa haiwezekani polisi wakaendelea kuua raia hivyo wanahamia Tarime mpaka kieleweke.
"Tutahamia Tarime kwa kuwa kwa mujibu wa taarifa ya awali hakuna raia ambaye alipigwa risasi kwa mbele hivyo inaonekana walikuwa wakikimbia hata kama wana makosa wameuawa kikatili,"alisema Mbowe.
Mbowe alisema kuwa hawaendi Tarime kuwatetea wahalifu bali wanakwenda kuwahakikishia haki inatendeka.
Dk Slaa amkaba Membe
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amemshangaa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe kwa kueleza kuwa Tanzania ni nchi inayojitegemea na yenye Rais, lakini walipoletewa barua kutoka SFO kuhusu Andrew Chenge, hawakuchukua hatua.
Dk Slaa alisema ni bora hizo fedha ambazo Serikali ya Uingereza inataka kuzitoa kwenye NGO ziende huko kuliko kuzipeleka serikalini kwa kuwa Serikali iliyopo madarakani ni ya kifisadi.
"Ni bora hizo fedha ziende kwa NGO ambayo inaaminika na kuweza kuwasaidia wanyonge,"alisema Dk Slaa.
Alitumia wakati huo kumtaka Ridhiwani Kikwete kwenda mahakamani kwa siku zake alizotoa kwani hana cha kuweza kumsumbua kwa kuwa ni mtoto mdogo.
Alisema kuwa maisha ya wananchi yameendelea kuwa magumu hivyo ni bora Rais Kikwete akae chonjo kutokana na hali hiyo."Juzi nimejiwa na askari polisi wameniambia kuwa usione tunawapiga mabomu, maisha yetu ni magumu,"alisema Dk Slaa.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa aliwaambia wananchi wa jimbo hilo kuwa CCM ni meli inayozama, hivyo wawahi mitumbwi Chadema ili waweze kuokoka."CCM njooni Chadema tuwaokoe kutoka katika meli inayozama na msihangaike kupanga viti katika meli inayozama,"alisema Msingwa.Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, alisema kuwa ata
pambana katika bajeti yake ili kuhakikisha maliasili zinawanufaisha wananchi maskini na si viongozi wa CCM waliokalia ufisadi."Nimeagizwa na chama changu kuhakikisha bajeti ijayo tunabanana na Serikali ya CCM ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao,"alisema Msigwa.

Chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment