Wednesday, 4 May 2011

TALIBAN WASEMA OSAMA BADO YUKO HAI

KIONGOZI wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda,  Osama bin Laden bado yupo hai na mzima wa afya.Washirika wa karibu wa al-Qaeda wa mtandao wa Taliban, umeeleza jana kuwa taarifa za kifo cha Osama hazina ukweli na ni za uzushi na hazina msingi.

Kituo cha televisheni cha GEO mjini Karachi nchini Pakistan limekariri taarifa za kundi la Taliban kwamba Osama yupo hai mafichoni na kusisitiza kwamba mwanzilishi huyo wa mtandao huo yupo salama.

Bin Laden, anayedaiwa kuhusika na mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 katika kituo cha kimataifa na Pentagon nchini Marerkani ameripotiwa kuuawa nchini Pakistan na majeshi ya Marekani mapema juzi katika nyumba alikokuwa amejificha.

Rais Barrack Obama wa Marekani alisema mjini Washington kuwa mashambulizi yaliyomua Osama yalitokana na kazi nzuri ya kitengo cha upelelezi cha Marekani.Kwa mujibu wa Marekani, Bin Laden aliishi katika nyumba moja katika mji wa  Abbottabad nchini Pakistan na Obama alisema kuwa nyumba hiyo ilikuwa ikifuatiliwa tangu Septemba mwaka jana.

Televisheni ya Dunya nchini Pakistani imeripoti kuwa katika mashambulizi hayo yaliyomuua Osama na mtoto wake wa kiume huku wake zake wawili na watoto wake sita wakiwa wamewekwa chini ya ulinzi.


Katika hatua nyingine, kundi lingine la Tehrik-e  Taliban la nchini Pakistan limetangaza kulipiza kisasi kwa Marekani kufuatia hatua yake ya kutekeleza operesheni ya kumsaka na kumuua Osama."Tulijivunia uwepo na uwezo wa Osama. Ni lazima tutalipiza kisasi kwa Marekani,"alisema  Ahsan Ullah Ahsan, msemaji wa kundi hilo jana.

Alipoulizwa namna atakavyotekeleza azma hiyo Ahsan alisema:"Tayari tuna watu wetu ndani ya Marekani na tunawatuma wengine zaidi."Osama anatuhumiwa kuhusika na mashambulizi katika balozi za Marekani Dar es Salaam,Tanzania na Nairobi nchini Kenya yaliyotokea na kuua mamia ya watu huku wengine wakijeruhiwa Agosti, 1998.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam Rais Kikwete alikumbusha mashambulizi hayo ya mtandao wa Osama wa Al Qaida nchini na watu 11 kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.

Alisema katika shambulio pacha ililotokea ofisi za Ubalozi wa Marekani nchini Kenya zaidi ya watu 200 waliuawa.

Rais alisema baada ya mashambulizi hayo uchunguzi ulifanyika na kuonyesha Osama na mtandao wake walihusika na mmoja wa watuhumiwa ambaye ni mtanzania alikamatwa Pakistan na sasa amefungwa gereza la Guantanamo Bay nchini Cuba.

chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment