Tuesday, 31 May 2011

MCHAKATO MWINGINE HUU

 Mchakato wa kununua meli mpya umeanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mchakato wa kununua meli mpya kwa ajili ya kusafirisha abiria katika Ziwa Victoria umeanza kwa ajili ya ununuzi wa meli hiyo.

Rais Kikwete amesema kuwa kwa sasa wataalamu washauri wa kupatikana kwa meli hiyo, yaani Kampuni ya OSK-Ship Tech ya Denmark, tayari wamekamilisha upembuzi yakinifu juu ya aina ya meli inayofaa kwa matumizi katika Ziwa Victoria.

Rais Kikwete amesema kuwa fedha za ununuzi wa meli hiyo zitatengwa katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/2013 baada ya kuwa maandalizi yote ya ununuzi wa meli hiyo kuwa yamekamilika.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa kazi ya tathmini ya kuzikarabati meli za Mv Victoria, Mv Umoja na Mv Sengerema ambazo zote zinatoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria umefanywa na sasa fedha zinatafutwa kwa ajili ya kuanza kazi yenyewe ya ukarabati.

Rais Kikwete ametangaza hayo leo, Jumatatu, Mei 30, 2011, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa eneo la Usagara, Bukumbi, Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, kabla ya kuzindua rasmi barabara ya lami ya kilomita 90 kutoka Usagara hadi Geita.


Amewaambia wananchi hao, “Kwa upande wa usafiri katika Ziwa Victoria, ninafurahi kuwafahamisha kwamba mchakato wa kununua meli mpya umeanza. Hivi sasa wataalam washauri, yaani Kampuni ya OSK-Ship Tech ya Denmark, wamekwishakamilisha upembuzi yakinifu juu ya aina ya meli itakayofaa katika Ziwa Victoria.”

Ununuzi wa meli hiyo utakuwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mheshimiwa Rais Kikwete wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana wakati alipowaahidi wananchi wa mikoa ya Ziwa kuwa Serikali yake ingenunua meli ya kusafirisha abiria ndani ya Ziwa hilo kuchukua nafasi ya Mv Bukoba iliyozama miaka 1996.

Tokea kuzama meli hiyo miaka 15 iliyopita ambako watu wanaokadiriwa kufikia 1,000 pia walipoteza maisha, Serikali haijapata kununua meli nyingine kwa ajili ya usafiri wa abiria katika Ziwa hilo na wasafiri wameendelea kutumia meli ndogo zaidi.

Mbali na Ziwa Victoria, Rais Kikwete pia aliahidi kununua meli ya abiria katika Ziwa Nyasa kuchukua nafasi ya Mv Mbeya iliyozama katika Ziwa hilo. Aidha, aliahidi kununua meli kwa ajili ya usafiri wa abiria katika Ziwa Tanganyika ambako meli inayosafirisha abiria ya Mv Liemba imekuwa inatumika kwa miaka 100 na imechoka na kuchakaa.


Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

30 Mei, 2011

NI VIZURI RAIS ANAPOKUMBUKA AHADI ZAKE NA KUZITIMIZA,LAKINI HAPO NILI-BOLD KIDOGO NNA MASHAKA.HATA HIVYO TUFANYE SUBRA.

No comments:

Post a Comment