Saturday, 14 January 2012

Kupanda umeme: Vilio kila mahali

 Send to a friend
0digg
Waandishi Wetu
KUPANDA kwa bei ya umeme kumepokewa kwa mshtuko na wananchi wa kada mbalimbali wengi wao wakisema hicho ni kitanzi kingine kwao wakati huu ambao gharama za maisha zimepanda, thamani ya shilingi imeshuka huku mfumuko wa bei ukiongezeka.

Wananchi wengi waliohojiwa na waandishi wa habari wa gazeti hili jana wameelezea kushangazwa kwao na kauli iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kwamba kupanda huko kwa bei ya umeme hakutawagusa watumiaji wadogo huku wakibainisha kwamba hawawezi kukwepa athari zitakazosababishwa na ongezeko hilo.

Wakazi wa mikoa mbalimbali nchini wakiwamo wasomi, wafanyabiashara, wafanyakazi na watu wa kawaida, wamesema Serikali isingepandisha gharama hizo kwa wakati huu na badala yake ingewaonea huruma kwa kutafuta namna nyingine ya kutatua tatizo hilo.

Juzi, Ewura iliidhinisha kupanda kwa bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kuanzia keshokutwa, Januari 15 mwaka huu huku Mkurugenzi wake, Haruna Masebu akisema ongezeko hilo halitawahusu wateja wa hali ya chini, wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco).

Kauli yake imepingwa na wananchi wengi ambao walisema gharama kubwa za umeme zitakuwa na athari kubwa kila mwananchi kwani zitasabisha ongezeko la bei za bidhaa na huduma.

Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Siena Italia, Emmanueli Maliti alisema: “Kila mwananchi atakutana na makali ya gharama hizi nje ya makazi yake, hakuna jinsi ya kukwepa. Kwanza hakuna utafiti wowote wa kitaalamu ambao umefanywa na kuthibitisha kwamba hata hao wanaoitwa walalahoi kama wanaweza kugharimia hiyo uniti moja ya umeme kwa Sh60, lakini pia hata kama wangewapa umeme bure, lazima wakutane na makali ya gharama hizo kwenye bidhaa na huduma.”

Alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa hata wasio walalahoi ni watumiaji wakubwa wa mkaa na kwamba kupanda kwa bei kutasababisha matumizi makubwa zaidi ya mkaa hivyo kuathiri mazingira.

“Hapa ndipo unaona mgongano kati ya sera ya kuhifadhi mazingira na sera ya nishati. Kupandisha bei ya umeme siyo suluhisho la matatizo ya Tanesco. Hatujaambiwa Tanesco inashughulikia vipi gharama zake za uendeshaji kwa sababu unaweza ukashusha gharama na kubaki na mapato makubwa bila kuongeza bei,” alisema.
Mhadhidi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bwete Gabriel alisema gharama za umeme zitamwelemea mwanchi wa kawaida na akisema matokeo yake ni kukua kwa umasikini.

Dk Gabriel alisema kupandisha bei kwa watu wa juu na kusema suala hili halimgusi mlalahoi ni utapeli kwani vitu vyote kutoka katika gharama hizo vitamrudia huyohuyo mlalahoi kwa gharama kubwa zaidi.
Umeme wapandisha bei ya maji Dar
Makali ya kupanda kwa bei ya umeme yameanza baada Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), kueleza azma yake ya kupandisha bei ya maji kutokana ongezeko hilo la gharama za umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa Dawasa, Jackson Midala alisema jana kuwa kutokana na bei mpya ya umeme, shirika lake litalazimika kulipa umeme Sh820 milioni kwa mwezi badala ya Sh580 za sasa.

“Mitambo inahitaji umeme mwingi na siyo jenereta. Kutokana na kupanda kwa gharama za umeme tunalazimika kuongeza zaidi ya Sh240 milioni katika fedha hizo ili tuweze kuzalisha. Tupo kwenye mchakato wa kupandisha bili ya maji,” alisema Midala.

Alisema mpaka sasa lita 1,000 za maji zinauzwa kwa Sh850 na ndoo moja ni Sh17 na kwamba fedha hizo ni ndogo zisizoweza kukidhi mahitaji ya uendeshaji kutokana na ongezeko la gharama za umeme.

Alisema tayari Dawasa wamewasilisha maombi Ewura kwa ajili ya kupandisha gharama hizo, lakini kwa sasa watalazimika kupitia upya mchanganuo wa gharama walizoainisha kwenye maombi hayo ili ziendane na gharama za sasa.

Gharama za tiba juu
Mkurugenzi wa Hospitali ya Shree Hindu Mandal, Kaushiki Ramaiya alisema hatua ya kuongeza bei ya umeme itaathiri gharama za uendeshaji katika sekta ya afya na kwamba wananchi wajiandae kukabiliana na ongezeko la gharama za dawa na baadhi ya huduma za hospitali.

Alisema ongezeko hilo litaonekana zaidi kwenye hospitali binafsi hivyo akaonya: “Hawakuangalia anayeumia ni nani.”

Alisema atakayeubeba mzigo wote wa gharama ni mwananchi kwa sababu wamiliki wakati wote wanahakikisha gharama za uendeshaji hazizidi mapato katika kutengeneza faida.

Kilio cha wakazi wa Dar
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam walisema kupandishwa kwa gharama hizo kunaashiria wazi kuwa hakuna mipango madhubuti ya kuwasaidia walalahoi.

Mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Zainabu Ally alisema hivi sasa taifa linaelekea kubaya kwani imefikia mahali viongozi wanatoa uamuzi kwa manufaa binafsi… “Kama tusipokuwa makini na uamuzi wa mambo mbalimbali hasa yenye maslahi kwa taifa letu, tutafika mahali kila kitu kitatisha.

Mkazi wa Buguruni, Jaremiah Agustino alisema wananchi wengi wanaishi chini ya kipato cha Sh1,600 (dola moja) kwa siku na kwamba bei mpya za umeme zitaendelea kuwadidimiza kiuchumi.

Kwa upande wake, Fatuma Suleimani, mkazi wa Kinondoni anayejishughulisha na saluni alisema: “Kweli Serikali inaonyesha kila dalili za kutudidimiza badala ya kutuimarisha kiuchumi. Katika maisha ya mwanadamu kwa sasa umeme una asilimia 70 ya kipato chake, sasa kama ndiyo hivi gharama imeongezeka na mgawo usiokuwa na ratiba tunakokwenda ni wapi?"

Arusha wapinga
Baadhi ya wakazi wa Arusha wamepinga uamuzi huo kupandisha bei ya umeme wakisema utasababisha kupanda kwa bei ya bidhaa mbalimbali na hivyo kuongeza gharama za maisha.

Mmoja wa wakazi hao, Joram Manga alisema umefika wakati kwa Serikali kuisaidia Tanesco ili iweze kujiendesha kwa kulipa ruzuku na madeni mengine badala ya mzigo wote kuachiwa wananchi.

Mkazi mwingine, Jenifer Minja aliwalaumu watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini akisema ndiyo tatizo kwani wamekosa ubunifu wa kupatikana umeme wa gharama nafuu badala yake wamejikita katika umeme wa mafuta wa kukodisha.

Kwa upande wake, mkazi wa jiji hilo, Ismail Mohamed aliitaka Serikali kuwa makini akisema kuendelea kupitisha mipango inayoongeza ugumu wa maisha kwa wananchi kunaweza kusababisha machafuko.

Mkazi wa Arusha, Yesaya Bayo alishauri wanaharakati na wabunge wazalendo kushirikiana kupinga ongezeko la gharama za umeme akisema ni hatari kwa usalama wa nchi kutokana na idadi kubwa ya watu kuendelea kuwa masikini.

Morogoro wahofia maendeleo
Mkoani Morogoro, baadhi ya wananchi wamesema kupanda kwa umeme kutarudisha nyuma maendeleo ya nchi na kuathiri uchumi wao na nchi kwa ujumla.

Mmoja wa wakazi hao, Amani Kasanga alisema nishati ya umeme na mafuta ndiyo mihimili ya maendeleo ya mtu na taifa lolote lile duniani hivyo kutetereka kwa nishati hizo kutavuruga mikakati mingi ya kujiimarisha kiuchumi.

“Hivi sasa umeme umepanda na mafuta yamekuwa yakipanda kila uchao, wananchi watarajia kupanda kwa gharama za maji, chakula na gharama za maisha kwa ujumla,” alisema Kashanaga.

Mkazi mwingine Amani Mwaipaja alisema: “Japokuwa tunaambiwa kuwa gharama hizi haziwahusu watumiaji wadogo lakini kimsingi watakaoathirika na ongezeko hilo ni watu wa kipato cha chini.”

Alisema Serikali inapaswa kutambua kuwa Tanesco, ni shirika la umma hivyo halipaswa kufanya biashara badala yake litoe huduma.

Mratibu wa Mradi wa Umoja wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali Morogoro (Ungo), Venance Mlali alisema madeni makubwa ambayo Tanesco inazidai taasisi za umma ndicho chanzo cha mzigo mzito wa gharama kubebeshwa wananchi wa kawaida.

Mlally alisema Serikali ina uwezo wa kukabiliana na makali ya umeme kwa kusaka vyanzo vingine vya mapato ili kukidhi gharama za umeme zinazoongezeka kila kukicha

Mwanza walia
Huko Mwanza, baadhi ya wakazi wa jiji hilo na wanaharakati wamesema kupanda kwa bei ya umeme ni mwiba kwa wote kwa sababu wazalishaji wataongeza gharama za bidhaa zao sokoni ili kufidia gharama hizo.

Meneja Utetezi wa Sera wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake Kivulini, Celestina Nyenga alisema kupanda kwa gharama hizo za umeme kutawaathiri zaidi wanawake kwa vile ndiyo wazalishaji wakubwa wa familia na ndiyo wanaobeba mzigo pindi gharama za maisha zinapopanda.

Kwa upande wake, mmiliki wa karakana ya uchongaji wa vyuma vya mapambo ya nyumbani, Emmaunul Goodluck alisema Serikali imekuwa ikilazimisha mambo kwa mujibu wa matakwa yake na siyo kwa maslahi ya wananchi.

“Najua kabisa utendaji wangu wa kazi ambao unategemea umeme utanilazimu kupandisha bei kufidia gharama za umeme. Nitaongeza bei kwa mteja na karakana yangu itaendelea na kazi,” alisema Goodluck.

Dodoma wapinga
Baadhi ya wakazi wa mjini Dodoma wamesema hawakubaliani na sababu iliyotolewa na Tanesco ya kupandisha gharama za umeme.

Mmoja wa wafanyabiashara wa mjini Dodoma, Josephat Kishobera alisema sababu zilizotolewa hazimwingii akilini akisema hivi sasa maji ni mengi… “Huu ni ujanja wa Serikali wa kutaka sisi watumiaji wa umeme tuilipie deni la Dowans. Sababu walizozitaja Tanesco hazina msingi wowote na sisi wafanyabiashara tutapandisha bei ya bidhaa zetu,” alisema.

Mwananchi mwingine, Josephat Nyaindi ambaye ni fundi wa kushona nguo alisema kupanda huko kwa bei, kutawagusa zaidi wananchi wa hali ya chini ambao ndiyo watumiaji wa mwisho wa bidhaa ambazo kwa kiasi kikubwa zinazalishwa kwa umeme.

“Kupanda huko lazima kutamgusa mwananchi wa hali ya chini kutokana na wao kutumia bidhaa zinazotokana na umeme kwa mfano, mimi nashona suruali kwa Sh16,000 ni lazima nitapandisha mpaka Sh20,000 ili kulipia ongezeka hilo,” alisema Nyaindi.

Kwa upande wake, Naye Neema James ambaye ni mama wa nyumbani alisema imefika wakati sasa wa kutumia nishati mbadala wa umeme kwani kiasi kilichopanda ni kikubwa ikilinganishwa na kipato cha mwananchi wa kawaida.

“Tunatumia umeme kwa shughuli nyingi, nadhani imefika wakati wa kutumia nishati mbadala wa umeme kama kuni na sola ambazo zina gharama nafuu kuliko huo umeme wa Tanesco” alisema.

Songea waishangaa Tanesco
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea, Ruvuma wameshangazwa na kitendo cha kupandishewa kwa gharama za umeme wakati mgawo wa nishati hiyo ukiendelea.

Mfanyabishara ya mashine ya kukoboa nafaka, Victor Ngongi alisema inashangaza Tanesco kupandisha bei ya umeme ilhali nishati hiyo haipatikani kutokana na mgawo.

Alisema kupanda kwa bei ya umeme kutachangia kupanda kwa ongezeko la bei ya vyakula kwani nao watapandisha bei ya ukoboa kwa asilimia 50 ili kufidia ongezeko hilo na gharama nyingine.

Mkazi wa Bombambili mjini Songea, Meriana Mapunda alisema hatua hiyo ina lengo la kumuumiza mlaji… “Kwa kweli hali ya umeme bado ni mbaya hasa hapa kwetu, umeme ni tatizo vitu vimepanda bei na tunawashangaa kwa kupandisha tena gharama za maisha wakati umeme wenyewe ni tatizo.”

Mbeya walia
Huko Mbeya, baadhi ya wananchi wamesema kitendo cha Ewura kuidhinisha kupanda kwa bei ya umeme kwa asilimia 40.29 ni mbinu za Serikali kutaka kulipa deni la Dowans… “Wameamua kutangaza gharama kubwa ili kupata unafuu wa kulipa deni hilo,” alisema mkazi wa Mwanjelwa, Ngussa Edward.

Mwananchi mwingine, Isaac Samson alisema si kweli kwamba wananchi wanaotumia chini ya uniti 50 hawataguswa akisema  maisha yataendelea kuwa magumu kutokana na bidhaa za viwandani kupanda na mtumiaji akiwa huyohuyo mwananchi wa chini.

Mkazi wa Uwanja wa Ndege, Ulimboka Benjamin alisema kitendo hicho kitaendeleza umasikini kwa wananchi na kwamba ni ndoto kwa wasio na huduma hiyo kuipata sasa.

“Je, kwa kuongeza gharama hizo tutaweza kuwafikia wananchi wote kupata huduma ya umeme? Huu ni unyonyaji kwa manufaa ya watu wachache na kutaka kulipa deni la Dowans,” alisema Ulimboka.

Habari hii imeandaliwa na Ellen Manyangu, Ibrahim Yamola, Fidelis Butahe na Shakila Nyerere - Dar, Patricia Kimelemeta -Ruvu, Joyce Joliga - Songea, Brandy Nelson - Mbeya, Venance George - Morogoro, Mussa Juma- Arusha, Frederick Katulanda - Mwanza, Masoud Masasi na Hamisi Mwesi - Dodoma.


mwananchi

No comments:

Post a Comment