Wednesday, 18 January 2012

MSIBA WA REGIA WAIBUA MAZITO

CHADEMA NUSURA WAZICHAPE MSIBANI IFAKARA, MBOWE AIPIGA SERIKALI KIJEMBE, MAKANI AANGUKA AKIAGA MWILI, KAFULILA AWA KIVUTIO  Send to a friend
0digg
Askari wa Bunge wakiwa wamebeba jeneza la aliyekuwa mbunge wa viti maalum (Chadema), Regia Mtema, wakati wa salamu na rambirambi za kumuaga rasmi kiserikali zilizofanyika viwanja vya karimjee jijini Dar es Salaam jana.Mbunge huyo anatarajiwa kuzikwa leo alasiri nyumbani kwao Ifakara mkoani Morogoro.Picha na Silvan Kiwale


MAKUNDI mawili yanayopinga ya wanachama wa Chadema jana nusura yazichape kavukavu yalipokuwa katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema huko Ifakara, kutokana na chuki na makovu ya uchaguzi wa wa ndani wa chama hicho wa mwaka 2010.

Wakati hayo yakitokea huko Ifakara, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitumia fursa aliyopewa wakati wa kuaga mwili wa mbunge huyo kuipiga vijembe Serikali huku Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, Bob Makani akianguka ghafla.

Marehemu Regia ambaye alifariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ajali ya gari iliyotokea Ruvu, Pwani, unatarajiwa kuzikwa leo Ifakara.

Katika tukio la Ifakara, mgogoro baina ya kambi mbili zilizotokana na makovu ya uchaguzi huo wa ndani kati ya wafuasi wa marehemu na ya Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Kiwanga ulisababisha kutimuliwa msibani hapo kwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kilombero, Salum Ngozi.

Ilielezwa kwamba baada ya Ngozi kufika msibani hapo juzi majira ya saa moja usiku na kusalimiana na viongozi wa Serikali, alifuatwa na baadhi ya makada wa chama hicho wakimtaka aondoke eneo hilo jambo ambalo aliligomea. Wafuasi hao wa Chadema waliamua kutumia nguvu kumwondoa hali iliyowalazimu polisi waliokuwa eneo hilo kuingilia kati. Askari walimtoa mwenyekiti huyo na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Wilaya.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Ngozi kutimuliwa katika msiba huo. Mara ya kwanza ilikuwa juzi na kumlazimu Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Francis Miti kuingilia kati.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ngozi alikiri kutokea vurugu hizo msibani na kudai kwamba, alifanyiwa fujo na kikundi cha watu aliowaita wahuni na kwamba amefungua kesi ya kufanyiwa vurugu katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Kilombero na kwamba baada ya kumalizika kwa mazishi atasimamia suala hilo ili haki itendeke.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe mbali na kukiri kuufahamu mgogoro huo, alisema asingependa kuzungumzia suala hilo sasa wakati watu bado wanaendelea na msiba.

Mbowe aipiga vijembe Serikali

Jijini Dar es Salaam, tukio la kuaga mwili wa marehemu Regia liligeuka jukwaa la siasa baada ya Mbowe na Makinda kupiga siasa.Mbowe alitumia msiba huo kutoa dukuduku lake juu ya shughuli za chama chake kisiasa na kiutendaji wakati akitoa salaam za rambirambi kwa marehemu.Mbowe aliirushia kombora Serikali na vyama vingine vya upinzani kuhusu mwenendo wa Chadema kuendesha siasa katika vyuo vya elimu ya juu akisema ni mpango maalumu kuwanoa wanasiasa mahiri.

Aliishauri Serikali na vyama vingine vya siasa kuiga utaratibu huo wa Chadema akisema unasaidia kukuza vipaji na kuwaandaa viongozi makini kwa kuwapa nafasi vijana kushiriki katika uongozi.

“Kuna jambo moja ambalo ningependa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine walitafakari na wasilibeze hili. Viongozi huandaliwa na viongozi makini hawazuki tu,” alisema  na kuongeza;

“Naeleza hivyo maana mara nyingi tumekuwa hatueleweki na tumekuwa tukibezwa. Sisi tunatambua viongozi wa baadaye  kisha tunakuza vipaji na kutoa fursa za nafasi za uongozi kwa vijana.”

“Vijana lazima waandaliwe kimaadili na ndiyo maana tuliingia vyuo vikuu lakini tukatafsiriwa kuwa ni wakorofi na wachochezi wa vurugu. Lakini leo tumepata viongozi wazuri vijana kwa njia hiyo kutoka vyuoni kama vile Mheshimiwa Zitto (Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini), Mnyika (John Mbunge wa Ubungo, Mdee (Halima-Mbunge wa Kawe), Silinde (David Mbunge wa Mbozi) na Mtema (Regia Marehemu).

“Hawa tuliwaandaa, hawakuzuka. Rai yangu kwa Serikali na kwa wazazi ni kwamba vijana hawa wakifanya siasa tusiwakwaze na kuwafukuza, bali tuwalee.”

Spika Makinda katika kile kilichoonekana kama ni kumjibu Mbowe, alitumia fursa hiyo kufafanua uendeshaji wa shughuli za Bunge akisisitiza kwamba linaendeshwa kwa kanuni na wala si kufurahisha watu.
Alimsifia marehemu Mtema kwamba alikuwa akizijua vyema kanuni za Bunge: “Bunge huendeshwa kwa kanuni na si kwa matakwa tu ya kufurahisha watu. Yeye marehemu alizijua kanuni ndiyo maana hata wakati alipokuwa akikosea alikuwa tayari kuomba radhi.”

Mzee Makani aanguka
Hata hivyo hafla hiyo iliingia dosari baada ya Makani kuanguka muda mfupi baada ya kuuaga mwili wa marehemu. Baada ya tukio hilo, alibebwa na kupelekwa pembeni ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha kurejea katika hali yake ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake.

Baadaye Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia ambaye alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakimpatia Mzee Makani huduma ya kwanza aliwaambia waandishi wa habari kuwa alianguka baada ya kuishiwa nguvu ghafla.

“Sasa anaendelea vizuri na amerudi kushiriki kumuaga mpendwa wetu katika safari yake hii ya mwisho,” alisema Mbatia.

Kafulila ashangiliwa

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila jana alishangiliwa kwa makofi baada ya kutangazwa kuwa mmoja wa wabunge walioteuliwa na Ofisi ya Bunge kuwamo katika msafara kusindikiza msiba huo akiwakilisha chama chake.
Baada ya kiongozi wa shughuli hiyo, Ofisa Mwandamizi wa Ofisi ya Bunge, Saidi Yakub kumtaja Kafulila baadhi ya waombolezaji walishangilia kwa makofi, vicheko vya chini kwa chini na minong’ono ya hapa na pale.

Hatua hiyo ya waombolezaji inatokana na hali ya kisiasa ilivyo kati ya Kafulila na chama chake hicho ambacho mwishoni mwa mwaka jana kilitangaza kumvua uanachama hatua ambayo ameipinga mahakamani. Kama ikitekelezwa, itamvua ubunge.

mwananchi

No comments:

Post a Comment