MAREHEMU MB.REGIA MTEMA
Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepatwa na majonzi makubwa na
kinasikitika sana kwa kifo cha Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa,
Mheshimiwa Regia Mtema ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum na Waziri
Kivuli wa Kazi na Ajira. Mheshimiwa Regia Mtema amefariki leo tarehe 14
Januari 2011 kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu darajani.
Katika
uhai wake marehemu Regia Mtema amefanya kazi mbalimbali za kisiasa na
kijamii katika taifa. Marehemu Regia Mtema amezaliwa tarehe 21 mwezi
Aprili mwaka 1980 na kusoma shule za sekondari kidato cha kwanza mpaka
cha sita katika shule ya sekondari ya Forodhani na Shule ya Wasichana ya
Sekondari ya Machame. Marehemu Regia Mtema alipata shahada yake ya
kwanza (Bsc Home Economics and Human Nutrition) katika Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine.
Mara
baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia Mtema alifanya kazi katika
taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Afisa
Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na baadaye kuteuliwa
kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA nafasi
ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti
maalum.
Viongozi
wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye pia ni
kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Katibu Mkuu Dr. Wilbroad
Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa chama makao makuu na
wabunge wamejumuika hivi sasa na familia ya marehemu katika kipindi hiki
kigumu.
CHADEMA
inatoa pole kwa familia ya marehemu Regia Mtema, wanachama wote na
wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wa Jimbo la Kilombero kutokana na
msiba huu wa ghafla katika wakati ambapo mchango wake ukihitajika kwa
chama na kwa taifa.
Taarifa
zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha
majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mipango
ya mazishi ya marehemu inapangwa nyumbani kwa Baba wa Marehemu Regia
Mtema, Ndugu Estelatus Mtema, Tabata Chang'ombe. Ratiba ya maziko
itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazopangwa na familia ya
marehemu, Ofisi ya Bunge na chama.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia Mtema, mahali pema peponi. Amina.
Imetolewa na:
John Mnyika(Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment