Tuesday, 3 January 2012

TAARIFA YA MBUNGE WA KIGAMBONI KUHUSU SAKATA LA KUPANDA KWA NAULI

BUNGE LA TANZANIA

OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA KIGAMBONI


Kumb na: KIG/KVK/VOL.1/6               

                                                 03 Januari 2012

Mhe. Mizengo Peter Pinda (MB)


Waziri Mkuu


DAR ES SALAAM


YAH: ONGEZEKO LA VIWANGO VYA NAULI KATIKA KIVUKO CHA MAGOGONI Kichwa cha habari hapo juu chahusika. Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni Serikali imetangaza nauli mpya katika kivuko cha Magogoni ambazo zimeanza kutumika tarehe 01.01.2012. Wananchi wa Jimbo la Kigamboni wanapinga ongezeko hili kwa sababu zifuatazo:


1. Vivuko na nauli zake zinatawaliwa na sheria ya SUMATRA CAP 314. Masuala ya nauli (tariffs) yanatawaliwa na kanuni ambazo zilichapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 92 la tarehe 26 Februari 2010.


a. Kifungu 4.1 kinasema “No service provider shall be allowed to set up and charge tariff which is not approved by the authority (SUMATRA).


b. Kifungu 6.2 kinasema “No service provider shall effect changes in tariff without notification of intended changes to the Authority for determination and approval.


c. Kifungu 10.3 kinasema The Authority shall notify the public of the application through a daily circulated newspaper and call for:


i. Stakeholders’ written submissions within 14 days from the date of publication


ii. Stakeholders’ meeting


Mheshimiwa Waziri Mkuu, WanaKigamboni wangependa kujua yafuatayo:


a. Je nauli hizi mpya zimepitishwa na SUMATRA? Kama ni ndiyo. Lini?


b. Ni lini mapendekezo ya nauli mpya yalitolewa kwa umma? Serikali ilitumia magazeti gani? Matangazo yalitoka tarehe zipi?


c. Ni lini na wapi mikutano ya wadau kuchangia kuhusu nauli mpya ilifanyika?


d. Mheshimiwa Waziri Mkuu, WanaKigamboni pamoja na mimi kama Mbunge sijapata kuona tangazo lolote na wala kushirikishwa katika kujadili bei mpya. Katika barua yangu ya tarehe 19 Januari 2011 yenye kumbukumbu namba KIG/KVK/VOL.1/1 kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TEMESA (nakala imeambatanishwa) niliomba na kusisitiza kuwa Wanakigamboni tuhusishwe na kushirikishwa katika mchakato wowote wa kuongeza nauli. Bahati mbaya sana, hili halikufanyika.


2. Mheshimiwa Waziri Mkuu, vilevile wanaKigamboni wanahoji vigezo vilivyotumika kufikia bei mpya za kivuko. Mheshimiwa Waziri Mkuu unatambua idadi ya vijana katika nchi yetu ni takribani asilimia 60-70%. Vijana wengi kwa sasa wanajiajiri kwa kuendesha maguta, pikipiki, Bajaj na kusukuma mikokoteni. Mheshimiwa Waziri Mkuu wanakigamboni wangependa vigezo vilivyotumika nauli ya vyombo vifuatavyo:


a. Guta toka Tsh 200 hadi Tsh 1800 (Asilimia 800); bei ambayo ni kubwa kuliko ya gari ndogo.


b. Bajaj zimepanda toka Tsh 300 hadi Tsh 1300 (asilimia 333).


c. Mikokoteni imeongezeka toka Tsh 200 hadi Tsh 1500 (Asilimia 650). Isitoshe mizigo inayopakiwa nayo inatozwa nauli.


Wafanyabiashara wengi wa Kigamboni wanatumia maguta, Bajaj na mikokoteni kusafirisha bidhaa. Kutokana na ongezeko la nauli ya kivuko bei ya bidhaa zimepanda maradufu. Hali ambayo inazidi kuwatia umaskini wananchi wa eneo hili.


3. Mheshimiwa Waziri Mkuu Wananchi wa Kigamboni wanaamini kuwa hakuna haja ya kuongeza nauli ikiwa mapato yatadhibitiwa vizuri. Kivuko hiki kinakusanya kiasi wastani wa Tsh 8 milioni kila siku. Makusanyo maalumu yakifanyika mapato hufika hadi Tsh 13 milioni. Mheshimiwa Waziri Mkuu upotevu wa Tsh 5 milioni kila siku ni nyingi. Wananchi hawaoni kwa nini wabebeshwe mzigo wa Serikali kushindwa kusimamia na kudhibiti mapato.


Mheshimiwa Waziri Mkuu ningependa kutoa mapendekezo yafuatayo:


1. Nauli hizi mpya zisitishwe ili tuweze kubaini uhalali wake kisheria na vigezo vilivyotumika.


2. Utaratibu ufanyike kuhakiki mapato na matumizi ikiwa ni pamoja na kuangalia maeneo ya kupunguza gharama. Kuna maeneo mengi yanayoweza kutumika katika kupunguza gharama.


3. Mchakato uanze upya ukishirikisha wadau wa huduma hizi.


Aidha, wananchi wa Kigamboni wametiwa simanzi na kuongezewa machungu na kitendo cha tarehe 01.01.2012 kilichofanywa na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli (MB) cha kuwatukana na kuwadhalilisha. Wananchi wa Kigamboni wanamtaka Waziri huyu awaombe radhi. Naomba umshauri Waziri Magufuli afanye hivyo. Ni jambo la kiustaarabu na kiungwana na litalinda heshima ya Serikali.


Mwisho, Mheshimiwa Waziri Mkuu nashauri kuwa suala hili lipewe umuhimu wa pekee kutokana na hali iliyopo Kigamboni sasa hivi. Kumekuwepo na utulivu wa muda kwa kuwa niliwaomba Wanakigamboni wanipe Mbunge wao nafasi ya kulifanyia kazi suala hili. Kwa kuchelewa kutoa maamuzi Serikali inajiweka katika mazingira magumu. Wako katika ujenzi wa Taifa


Mhe. Dkt Faustine Ndugulile (MB)


MBUNGE


Nakala:


1. Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


2. Mhe. Mecky Sadick-Mkuu wa Mkoa Dar Es Salaam


3. Mhe. Wilson Mukama-Katibu Mkuu wa CCM Taifa


4. Kamati ya Wabunge wa Dar Es Salaam


5. Waheshimiwa Madiwani wote-Jimbo la Kigamboni

No comments:

Post a Comment