Monday, 16 January 2012

Mwenyekiti Wenu Nimevamiwa Na Kushambuliwa Porini Madibira


 
Ndugu zangu,
Hizi si habari njema. Juzi alhamisi kunako saa kumi na mbili na nusu asubuhi nilipatwa na balaa la barabarani.
Ilikuwaje? Niliondoka Iringa Jumatano jioni kuelekea kijijini kwetu Nyeregete. Nilifika Madibira, Mbeya jioni ya saa kumi na mbili na nusu. Kwa vile giza lilikaribia, nikaamua kulala kijijini Mahango, nyumbani kwa ndugu yangu aitwaye Salim Raphael Mjengwa.
Alfajiri tukaondoka pamoja maana naye alitamani kufika kijijini Nyeregete kumsalimu baba yake mzazi. Tukiwa katikati ya pori eneo la Ikoga kuelekea mji wa Rujewa nikabaini gari iliyokuwa ikija nyuma yetu  kwa mwendo wa kasi.
Nikamwambia ndugu yangu Salim juu ya uwepo wa gari nyuma yetu. Akaniambia kuwa ni basi dogo la abiria. Kupitia sight mirror nikamwona dereva wa nyuma yangu akijaribu kunipita mahali pasipostahili na kwa mwendo wa kasi. Kwa vile barabara ilikuwa ni nyembamba sana , basi, akalazimika kukatisha jaribio la kunipita.
Baada ya mwendo wa nusu kilomita hivi nikapaona mahali muafaka pa kuegesha gari yangu pembeni kumruhusu apite. Nikawasha indiketa, nikaweka gari yangu pembeni.
Dereva yule akapita na kusimamisha gari yake katikati ya barabara. Akatoka kunifuata. Nami nikaanza kujiandaa kufungua mlango na mkanda wangu ili nitoke tuongee.
Kabla hata sijafungua mlango, yeye akauvuta mlango wangu na kunishambilia kwa ngumi usoni. Nikainamisha uso wangu kwenye usukani. Nikasikia pia ndugu yangu Salim akitamka; " Seme unafanya nini?" Salim alimfahamu kwa jina dereva huyo, anaitwa Seme.

Mara, dereva mwenzangu akaacha kunishambulia na kunitukana. Nikainua kichwa. Nikamwona akiondoka huku kundi la vijana waliokuwa abiria wake nao wakirudi kwenye gari lao. Walikuja kushiriki shambulizi dhidi yangu.

Walikuwa na dhamira mbaya sana. Kama si uwepo wa ndugu yangu Salim ambaye wote walimtambua hadithi ingekuwa nyingine.

Tulipofika Rujewa nikaripoti tukio hilo kituo cha Polisi Mbarali. Dereva mwenzangu naye akafika kituoni. Afande Mwamakula, ambaye ni mkuu wa kituo aliweka wazi kuwa alichofanya dereva yule ilikuwa ni jinai.

Kwa vile nilihitajika kufika kijijini kumwona mgonjwa aliye taabani. Na kwa vile nilihitajika kurudi Iringa kupokea ugeni kutoka Ubalozi wa Sweden. Na kwa vile dereva yule alikiri kosa lake na kuniomba radhi. Na kwa vile dereva yule aliweka wazi kuwa ni msomaji wa makala zangu, basi, nikaamua kutoendelea na shauri lile. Nilimsamehe kwa kumwambia; hupaswi kufanya tendo kama lile kwa mtu yeyote yule. Ule haukuwa uungwana.

Wenu,
Maggid Mjengwa,
Iringa.

No comments:

Post a Comment