Tuesday, 3 January 2012

WABUNGE DAR WAMTAKA MAGUFULI AOMBE RADHI KWA KAULI CHAFU

 

KAULI ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kwamba watakaoshindwa kulipa nauli mpya ya Sh200 kuvuka Kigamboni ni vyema wakapiga mbizi kuvuka bahari, imewakera wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao sasa wanamtaka aombe radhi.

Juzi, Dk Magufuli akiwa katika ziara eneo la Kivukoni alijaribu kuzungumza na wananchi wa Kigamboni kuhusu ongezeko hilo la nauli lakini badala ya wananchi hao kumsikiliza, walizomea ndipo alipowaambia kuwa watakaoshindwa ni vyema wakapiga mbizi baharini, kuzunguka Kongowe kuingia katikati ya jiji au warudi kijijini wakalime.jana, wabunge hao licha ya kumtaka Dk Magufuli aombe radhi, wameitaka Serikali kusitisha mara moja amri ya ongezeko hilo la nauli katika kivuko hicho kutokana na uamuzi huo kufikiwa bila ya kuwashirikisha wananchi.

Akitoa tamko kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu alisema tatizo lililopo katika kivuko hicho ni ubadhirifu mkubwa ambao umekuwa ukijitokeza na si nauli ndogo.Alisema ubadhirifu huo umesababisha makusanyo ya ushuru kuwa Sh9 milioni badala ya Sh18 milioni kwa mwezi na kuhoji fedha nyingine zinakokwenda.
Alisema  kitendo kilichofanywa na Waziri Magufuli ni cha kuidhalilisha Serikali kutokana na kutokuwa na ushirikiano na viongozi wengine na kufanya kazi kwa hasira.“Kwa hakika, Magufuli ametutukana kutokana na tabia yake ya kufanya kazi kwa hasira.

Tunamtahadharisha sisi ni wazaliwa wa Dar es salaam na ndiyo tunaujua huu mji. Hatutaki kuongea tu kama yeye, kinachotakiwa ni kusitisha ubabe wake maana  hapa siyo Chato (Jimbo ambalo Dk Magufuli ni mbunge wake),” alisema Mtevu.Mtevu alisema lazima Magufuli ajue nauli hizo hazikufuata sheria ya upandishaji kwa maana hata Sumatra (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nchi Kavu na Majini), haijui kinachoendelea huku akisema kauli yake kwamba kupandisha nauli kunatokana na vituo vingine kupandisha ni ya kukurupuka inayotaka kuichonganisha Serikali na wananchi.

Alisema  jiji la Dar es Salaam linachukua watu wengi kutoka Kigamboni  hivyo, kupandisha nauli ni kuwaonea wananchi wanaoishi huko na ikifanya hivyo, Serikali itakuwa haijadhamiria kuwasaidia wananchi, bali kuwakomoa.Mtevu alisema kinachofanywa na Waziri Magufuli ni hasira na si uongozi bora akidai kwamba kila kitu anachoibua kinaleta mgongano katika Serikali huku akimsihi kuacha kukurupuka katika kutekeleza Ilani ya CCM.“Kitendo cha kuongeza nauli ni kuwaongezea neema watu wachache. Zoezi hilo lisitishwe mara moja na kuleta amani.
Alisema kama Serikali imeshindwa kusimamia mapato ya vivuko viwili vya Mv Kigamboni na Mv Alina, vikabidhiwe kwa wabunge kwa wiki mbili ili kukusanya mapato.
Alisema Serikali inapaswa kujua kwamba, CCM ndicho kilichopandisha nauli kutokana na jimbo hilo kusimamiwa na chama hicho na kuongeza kwamba hatua hiyo itawaathiri zaidi ya watu milioni 2.5.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria mkutano huo mbali na Mtemvu ni pamoja na John Mnyika (Ubungo), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk Faustine Ndugulile (Kigamboni, Zarina Madabida, Angela Kairuki na Philipa Mtulano (Viti Maalumu).
Akizungumzia madai ya wabunge hao, Msemaji Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo alisema msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo ni ule uliotolewa na Serikali kupitia kwa Dk Magufuli wa kupandisha nauli tofauti na madai kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kutoa agizo la kusitishwa kwa ongezeko hilo... “Hadi sasa kauli inayosimama ni ya Waziri (Magufuli).”
Kilio cha Dk NdugulileDk Ndugulile alisema hali ya hewa imechafuka katika jimbo lake kutokana na kuwatangazia wananchi kuwa Waziri Mkuu  amesitisha ongezeko hilo baada ya kupigiwa simu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik.Hata hivyo, Sadik alikaririwa na vyombo vya habari jana akikanusha kupokea maagizo hayo na kwamba alichoagiza ni kumtaka katibu mkuu katika ofisi yake kuwasiliana na mwenzake wa Ujenzi juu ya suala hilo kwa manufaa ya wananchi wa Kigamboni.
Dk Ndungulile alisema ongezeko hilo linagusa watu wanyonge   kwa zaidi ya asilimia 800 akiwataja kuwa ni  waendesha baiskeli za miguu mitatu (Maguta), baiskeli za kawaida, pikipiki na Bajaji  wakati wenye magari ya kifahari  hawajapandishiwa kiasi kikubwa cha nauli.Alisema haiingii akilini kuona guta likipaswa kulipiwa Sh1,800 kutoka Sh200 wakati gari dogo litalipa Sh1,300 kutoka Sh800... “Bei hizo ni za kumkomoa nani?”
Alisema tangu achaguliwe kuwa ubunge, amekuwa akimwandikia barua Waziri wa Ujenzi kuhusu kero mbalimbali za kivuko hicho lakini hakuna alichojibu zaidi ya kujitokeza jana (juzi) na kutangaza nauli mpya.“Wakati naingia katika nafasi ya uongozi wa ubunge Jimbo la Kigamboni nilitaka kupata taarifa ya mapato ya uendeshaji wa  kivuko ambapo nilipata taarifa ya makusanyo ya Sh8 milioni hadi 13milioni.

Baada ya kupokea taarifa hizo nilifanya uchunguzi wangu ambao baadaye nilibaini kuwa Serikali inapata kiasi cha Sh5 milioni kama mapato ya kivuko hicho huku kiasi cha Sh3 milioni kikiwa hakijulikani kinakwenda wapi,” alisema. Dk Ndugulile alisema kama Serikali ingeweza kudhibiti hali hiyo, leo hii kusingekuwa na ongezeko hilo la nauli kutoka Sh100 hadi 200 kwa waenda kwa miguu huku magari yenye ujazo tofauti wakitakiwa kulipa kiasi cha Sh1,300 hadi 1,500.Zungu: Kilio cha wajasiriamali
Kwa upande wake, Zungu alisema gharama hizo zimewaathiri kwa kiasi kikubwa wajasiriamali kuliko wenye fedha. Alisema nauli zilizowekwa hazikufuata sheria kutokana na kutoshirikisha wananchi wala kiongozi yoyote na kuhoji ulizi gani shirikishi unaohubiriwa.“Naomba tujiulize kikao cha kuongeza nauli kilifanyika wapi,  maana huu ni mzigo ambao wananchi hawatakiwi kubebeshwa,” alisema.Madabida kwa upande wake alisema ongezeko hilo litawaathiri zaidi kina mama wanaofanya biashara ndogondogo kwa kutumia kivuko hicho.Alisema Magufuli anataka kuwachonganisha wananchi na wabunge kutokana kauli zake

Chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment