Wednesday, 17 July 2013

Miili ya askari JWTZ kuletwa Jumamosi


Dar/mikoani. Wakati miili ya askari wa Tanzania waliokufa Darfur ikitarajiwa kuletwa keshokutwa, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wameanza kuwasili Dar es Salaam kwa ajili ya kuipokea.
Msemaji wa Mpango wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa na Afrika (UNAMID), kwenye Mji wa Darfur, Chris Cycmakick alisema jana kuwa miili hiyo ilikuwa ikiendelea kufanyiwa uchunguzi ambao unatarajiwa kukamilika leo.
“Hata kama uchunguzi ukikamilika kesho (leo), hatuwezi kusafirisha keshokutwa (kesho Ijumaa) kwa kuwa hapa Sudan ni kama siku ya mapumziko. Sasa utaratibu unafanyika kuisafirisha Jumamosi kwa ndege ya Umoja wa Mataifa,” alisema Cycmakick.
Wapiganaji hao saba waliuawa na moja ya vikundi vya waasi walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kulinda amani kupitia UNAMID huko Darfur.
Uchunguzi wa gazeti hili, ulibaini kuwa wanajeshi hao wanatoka vikosi vya 42KJ Chabruma, Songea, 44KJ Mbeya, 36KJ Msangani, 92KJ Ngerengere, 94KJ Mwenge, Dar es Salaam, 41KJ Nachingwea na Makao Makuu ya Jeshi- Upanga, Dar es Salaam.
Familia zawasili Dar
Wakati miili ya wapiganaji hao ikiletwa, tayari familia zao zimeshawasili Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapokea marehemu hao kwa maziko katika maeneo yaliyopangwa na wengine wakisubiri katika mikoa yao.
Akizungumza na mwandishi wetu jana eneo la Mji Mpya, Songea, Mama wa marehemu, Rodney Ndunguru, Lucy alisema wanachosubiri ni kupokea mwili wa marehemu watakapoletewa na jeshi kutoka Dar es Salaam.
Alisema mwili wa mtoto wake huyo aliyekuwa Kambi ya 92KJ, Ngerengere mkoani Morogoro utasindikizwa na mke wa marehemu, Fatma Hajj Ammen anayetokea Zanzibar alikokwenda kujifungua mtoto ambaye sasa ana miezi minne.Mama huyo alisema kuwa mwanawe huyo kifungua mimba na aliyekuwa katika kikosi cha makomandoo, atazikwa alikolala baba yake, eneo la Myangayanga, Songea.
Naye Maria Chaula, mke wa Koplo Oswald Chaula aliyekuwa Kikosi cha Mizinga katika Kambi ya Chabruma, aliondoka jana alfajiri kwenda Dar es Salaam kupokea mwili wa marehemu mume wake wakati watoto wake wanne wakitangulia Kijiji cha Mtitu Wilaya Kilolo, Iringa kwa taratibu nyingine za mazishi.
Mama wa marehemu Chaula, Zaina Mpagama, akiwa kijijini Mtitu, alisema askari huyo ambaye ni mtoto wake wa sita na ni pekee wa kiume, ameacha pengo lisilozibika... “Baba, nimepata pigo, mwanangu pekee wa kiume jamani...,” alisema huku akilia kwa uchungu.
Mjini Mbeya, huzuni na simanzi zimetawaka katika Kambi ya 44KJ Mbalizi baada ya taarifa za kifo cha askari wa miguu, Peter Werema.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment