Friday, 4 July 2014

Mbasha amshitaki Gwajima

stori: Waandishi Wetu
Mambo juu ya mambo! mvumo mkali wenye kuogofya unaendelea kutamalaki katika ndoa ya wanamuziki zao la upako wa Injili Bongo, Emmanuel na Flora Mbasha, safari hii ‘topiki’ siyo zile tuhuma za ubakaji zilizopo mahakamani.
Wanamuziki zao la upako wa Injili Bongo, Emmanuel na Flora Mbasha,

Mbeba ‘niuzi’ wa awamu hii ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, baada ya Mbasha kuona isiwe tabu, hivyo kuamua kupambana na mtumishi huyo wa Mungu kwa njia ya kiroho zaidi. 
Mbasha baada ya kulieleza gazeti mama la hili, Uwazi lililoandika habari yenye kichwa “Mbasha: Gwajima Niachie Mke Wangu”, akiidadavua dhana yake kwamba hapendi ufadhili wa Gwajima kwa mkewe, yaani Flora sasa ameamua kwenda mbele zaidi.
Habari zinadai kuwa, mbele ya Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Mkoa wa Dar es Salaam, Bruno Mwakibolwa ambalo Gwajima ni memba hai, ameshapokea mashitaka kuhusu mchungaji huyo kuhusika kuitikisa ndoa ya waimbaji hao wa Neno la Mungu na mlalamikaji ni Mbasha mwenyewe.
Wikiendi iliyopita, Mbasha aliketi na kiongozi huyo na kushusha tuhuma zake dhidi ya Gwajima kama zilivyothibitishwa na mlalamikaji mwenyewe, nazo ni hizi zifuatazo;
MOSI; Gwajima ni kiongozi wa kiimani wa Mbasha na Flora lakini tangu matatizo ya ndoa yao yalipojitokeza, mchunga kondoo huyo wa Bwana hajawahi kufanya lolote kunusuru muunganiko huo uliohalalishwa kwa jina la aliye juu.
Emmanuel Mbasha
PILI; Gwajima anajua kila kitu kuhusu mgogoro wa Mbasha na mkewe lakini kipindi chote cha matatizo, Kanisa la Ufufuo na Uzima limekuwa mfadhili wa Flora kwa sehemu kubwa. Hapa anauliza, huu ufadhili una kipi nyuma yake?
TATU; Gwajima anatambua kuwa Flora ni mke wa mtu, mwenye mali ameshaomba aachiwe mwandani wake bila mafanikio. King’ang’anizi kina msukumo upi?
NNE; Gwajima amekuwa akimuumiza Mbasha kihisia, kiakili na kiroho kwa sababu yeye anagombana na mkewe lakini mchungaji huyo bila kufikiria maumivu aliyonayo, humwita Flora madhabahuni katika ibada na kumpa nafasi ya kuimba.
TANO; Flora anaishi hotelini na yeye mwenyewe alishakiri kuwa fedha za kulipia hoteli alizipata kutokana na michango ya waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima. Hapa Mbasha analalamika, inakuwaje kanisa limfadhili mke wa mtu kuishi hotelini ikiwa mumewe hajui?
SITA; Katika hoja zote hizo, Mbasha amelieleza Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste kuwa hana imani na Gwajima kwa vile kama ni busara baada ya kuona ndoa hiyo imetikisika yeye (Gwajima) angekaa pembeni kwa namna yoyote ile, hivyo Mbasha akaiomba menejimenti ya baraza hilo kumpa adhabu kali mwenzao.
Mbasha alipozungumza na Amani, Jumanne iliyopita, alisema baraza hilo liliahidi kushughulikia shauri lake na uamuzi utachukuliwa baada ya kumwita Gwajima na kumsikiliza kwa upande wake.
WENYE KWENU KWAHERI!
Kesi ya Mbasha kudaiwa kumbaka shemeji yake ilipoanza, mume huyo wa Flora alikimbilia mafichoni, kwa hiyo swali kwamba anaabudu kwenye kanisa gani halikuwa na mashiko kwa sababu mhusika mwenyewe hakuwa akionekana.
Baada ya Mbasha kujitokeza na kufikishwa mahakamani, kupelekwa mahabusu kwenye Gereza la Keko kabla ya kuachiwa kwa dhamana, ndipo swali kuwa anaabudu kanisa gani lilipoanza kutokana na ukweli kuwa yupo uraiani kwa ‘bondi’.
Swali hilo lilitokana na hoja kwamba kabla ya mgogoro na mkewe walikuwa wakisali kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Gwajima ambaye alishamtuhumu kumfadhili Flora na akamtaka amwachie ‘waubani’ wake huyo ili maisha yaendelee.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,

Jawabu la swali hilo, lilijibiwa Jumapili iliyopita baada ya Mbasha kutinga Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), maarufu kama Mito ya Baraka, linaloongozwa na Mchungaji Bruno Mwakibolwa, na kukamilisha haja zake za kuabudu pale.
Mbasha alipozungumza na Amani kuhusu kusali kwa Mchungaji Mwakibolwa badala ya kwa Gwajima, alijibu: “Nimehama Kanisa la Ufufuo na Uzima, sisali tena kule. Kuanzia sasa shughuli zangu za kuabudu nitazifanyia Mito ya Baraka kwa Mchungaji Mwakibolwa.
“Siwezi kwenda kwa Gwajima kwa sababu simuelewi na ndiyo maana nimeamua kumshtaki kwa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste. Roho yangu ya kuabudu isingekuwa timilifu, ingejaa mashaka kwenda sehemu ambayo imenijeruhi na nisiyoiamini.
“Kwa kifupi si kwamba nimeanza kuabudu Mito ya Baraka hili ndilo kanisa letu tangu zamani, mimi na mke wangu. Tulihamia Kanisa la Ufufuo na Uzima baada ya Gwajima kutushawishi, kwa hiyo nimerejea kundini.
MCHUNGAJI MWAKIBOLWA
Juzi, Amani lilimsaka Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Mkoa wa Dar es Salaam, Mchungaji Mwakibolwa lakini simu yake ilipokelewa na kusikika sauti za watu wakiwa kwenye maombi kama si ibada.
GWAJIMA
Baada ya hapo, Amani lilimsaka Mchungaji Gwajima kwa njia ya simu yake ya mkononi lakini yeye hakupokea hata pale alipopigiwa kwa kurudiarudia.
KESI YA MBASHA
Kesi ya Mbasha kudaiwa kubaka itatajwa tena Julai 17, mwaka huu kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
VIPI KUHUSU KUPATANA?
Wiki iliyopita katika Gazeti la Risasi Jumamosi kuliandikwa habari yenye kichwa; MBASHA, FLORA WAPATANA. Katika habari hiyo ilidaiwa wawili hao walipatana lakini walibakiza kikao kimoja cha kumalizia taratibu zote.
Habari zinasema, taratibu hizo zinandelea licha ya Mbasha kumshitaki Gwajima kwenye Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Mkoa wa Dar es Salaam.    

No comments:

Post a Comment