Thursday, 7 March 2013

Kibanda ateswa kama Ulimboka•  AVAMIWA, APIGWA, ATOBOLEWA JICHO, ANG’OLEWA KUCHA NA MENO


MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Rai, Mtanzania, Dimba na Bingwa, Absalom Kibanda, amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya.
Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) alipigwa na kitu kizito chenye ncha kali kichwani, kutobolewa jicho la kushoto, kung’olewa ukucha wa kidole cha mkono na meno.
Tukio hilo linakuja ikiwa ni miezi takriban tisa tangu kutekwa, kuteswa, kuumizwa vibaya, kung’olewa meno na kucha na kisha kutelekezwa msituni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, usiku wa Juni 26, mwaka jana.
Tangu kutokea kwa tukio la Dk. Ulimboka ambalo linafanana kabisa na hili la Kibanda, Jeshi la Polisi nchini limekuwa likitupiana mpira katika kueleza hatua zilizofikiwa kuwasaka watuhumiwa waliohusika.
Pamoja na mtuhumiwa mmoja anayedaiwa kuwa raia wa Kenya, Joshua Mulundi, kufikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika na tukio hilo, bado Jeshi la Polisi halijawahi kumhoji Dk. Ulimboka wala watuhumiwa aliowataja kwa majina kuwa walihusika kumteka na kumtesa.
Katika tukio la Kibanda, inaelezwa kuwa watuhumiwa hao ambao hawajakamatwa walimtendea unyama huo akiwa nyumbani kwake eneo la Mbezi Beach usiku wa saa sita akiwa ndani ya gari akingojea kufunguliwa lango.
Tukio hili pia limetokea wakati Kibanda akikabiliwa na kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo anashitakiwa na Jamhuri akidaiwa kuchapisha makala katika gazeti la Tanzania Daima ambalo alikuwa Mhariri Mtendaji wake.
Kesi hiyo ambayo ilikuwa imepangwa kuendelea kusikilizwa jana, iliahirishwa baada ya mawakili wake kuwasilisha ombi mahakamani kueleza tatizo alilolipata mteja wao.
Kibanda anena
Akielezea tukio hilo kwa taabu kutokana na maumivu makali aliyoyapata, Kibanda alisema kuwa akiwa amesimama langoni ghafla alishtukia gari lake likivunjwa kioo, na katika harakati za kutaka kutambua nini kinaendelea, alivamiwa na watu hao.
“Baada ya kuona hali hiyo nilitaka kujiokoa kwa kukimbia lakini nilianguka, hivyo wakaanza kunishambulia kwa kunipiga nondo kichwani na sehemu mbalimbali za mwili, wakanikata kidole kwa kuing’oa kucha na kunitoboa jicho la kushoto,” alisema.
Kibanda aliongeza kuwa baada ya kumtendea unyama huo, alimsikia mmoja wao aliyekuwa na silaha ya moto akiikoki risasi na kisha kumuuliza mkuu wao, “afande tummalizie?”
Bashe atoa kauli
Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd Hussein Bashe, alimkariri Kibanda akisema kuwa alivamiwa na watu watatu waliokuwa wamejihami kwa silaha za moto na jadi.
Bashe alisema kuwa alikaa ofisini na Kibanda hadi usiku wa saa tano na kumtangulia kidogo kwenda nyumbani, lakini baadaye akapigiwa simu na kuelezwa kuwa amevamiwa akiwa nyumbani kwake na kujeruhiwa.
Alisema tukio hilo ni la kusikitisha na linapaswa kulaaniwa na kila mpenda uhuru wa kupata habari, kwa kile alichoeleza hakuna mtu mwenye haki ya kumhukumu mwenzie kwa mtindo walioufanya kwa Kibanda.
Bashe alisema pamoja na jitihada za madaktari wa Kitengo cha Mifupa cha Muhimbili (MOI) bado wameshauriwa kumpeleka Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika jicho lake ambalo linaonekana kupata athari zaidi kuliko sehemu nyingine.
“Madaktari wametuhakikishia katika vipimo walivyomfanyia kuwa hakuna madhara yoyote makubwa bali yuko salama, hivyo na hawa ni wataalamu wetu ambao tunawashukuru kwa juhudi zao,” alisema.
TEF waonya
Akizungumza kwa niaba ya waandishi na wahariri wa habari waliofurika kwa wingi hospitalini hapo, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga, alisema tukio hilo limefanywa na watu waoga ambao wanadhani kwa kufanya hivyo wataweza kuwanyamazisha waandishi.
Alisema tukio hilo halina uhusiano wowote na ujambazi, bali ni dhamira ya watu waliokuwa wakitaka roho ya mhusika kwa kuwa hawakuchukua vitu vilivyomo ndani ya gari lake.
“Hatuwezi kutenganisha tukio hili na kazi yake hata kama wahusika hawakuonesha dalili ya kuchukua vitendea kazi vya kuwasaidia. Tunachoweza kuamini ni kuwa hili ni tukio la kutaka kuvinyamazisha na kuviogopesha vyombo vya habari,” alisema.
Makunga alisema jukwaa litafanya uchunguzi wa kina ili kubaini matukio mbalimbali ya kushambuliwa waandishi wa habari yanayoshika kasi kila kukicha.
“Nawaomba waandishi tuwe na moyo wa subira wakati uchunguzi wa kutekwa na kuteswa kwa mwenyekiti huyu ukiendelea kujua ukweli,” aliongeza.
Mbowe: Watuhumiwa wasakwe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alikuwa miongoni mwa viongozi wachache wa kitaifa waliofika Moi kumjulia hali Kibanda na kisha kulifananisha tukio hilo kama uharamia.
Mbowe alisema kuwa vyombo vya dola vinatakiwa kuchukua hatua za haraka ili kulinda uhuru wa habari na wanahabari nchini, huku akisisitiza umoja wa kushikamana kwa kipindi chote.
“Tunaitaka serikali kuchunguza kwa kina suala hili la Kibanda, kwani ni la kiharamia, si mara ya kwanza watu kufanyiwa kama hivi hapa nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa wanahabari wanatakiwa kuendeleza mshikamano muda wote pasipo kurudi nyuma.
Mengi: Wahusika watajwe
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), Reginald Mengi, alisema suala hilo wamelipokea kwa masikitiko na hawakutegemea litokee.
“Tukio hili ni kubwa na kwa sasa MOAT tunataka kuhakikisha tunaokoa maisha ya mwenzetu na baadaye tutakaa kuamua cha kufanya,” alisisitiza.
Mengi ambaye alifika hospitalini hapo mapema na kuungana na wanahabari pamoja na ndugu zake Kibanda, mara kwa mara alirejea kauli ya kuwataka wanahabari kutumia taaluma yao vizuri na kufanya kazi bila woga.
“Naomba mzingatie maadili na taaluma, sote tuwe kitu kimoja juu ya hili na zaidi tufanye uchunguzi wa kutosha ili kuweza kuripoti bila kuingiliana na wengine,” alisema.
Alisema waandishi wanapaswa kutambua kuwa kuna mikakati ya kuwagawa inayofanywa na watu wasiotaka kuguswa masilahi yao, kwamba matukio kama hayo ni njia moja ya kuwatisha na kuwakatisha tamaa.
“Haya ni mambo ya kusikitisha, wapo waliokuwa wanauliza kwanini Kubenea (Saed) alitibiwa au kwanini kulifanyika jitihada za kumsaidia Dk. Ulimboka. Sasa majina ya wahusika wa uharamia huu yanapaswa kutajwa hadharani,” alisema Mengi.
Mengi aliongeza kuwa walijadiliana na kuamua kuteua watu wawili watakaokwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kushughulikia matibabu ya Kibanda. Waliokwenda ni mke wa Kibanda na mwandishi wa habari, Erick Kabendera.
Zanzibar watoa pole
Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza), nayo ilieleza kupokea kwa mshituko na masikitiko makubwa habari za kuvamia na kumjeruhi vibaya Kibanda.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, walisema kuwa wanaungana na wengine katika tasnia ya habari na watetezi wa haki za binadamu kulaani kitendo hicho cha kumjeruhi Kibanda.
“Tunatoa pole kwa Kibanda, familia yake, Jukwaa la wahariri, pamoja na ofisi yake kutokana na tukio hilo, na kumuomba Mwenyeji Mungu ampe afya kwa haraka.
Katibu wa Wahamaza, Salma Said, alisema kuwa viongozi wa serikali na polisi wanapaswa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha kuwa watu waliohusika na tukio hilo wanakamatwa kwani limekuja muda mfupi wakati wananchi wakiwa na hofu ya matukio ya kushambuliwa kwa viongozi wa dini visiwani Zanzibar.
Nao waandishi, wanaharakati na wadau mbalimbali wa habari mkoani Arusha walieleza kusikitishwa na tukio hilo na hivyo kuwatahadharisha waandishi nchini kuwa makini.
Katibu wa klabu ya waandishi wa habari mkoani, Arusha Eliya Mbonea, aliwataka wanahabari kulichukulia tukio hilo kama somo kwao na kuongeza tahadhari.
Polisi yaanza uchunguzi
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka waandishi wa habari kushirikiana katika kutoa taarifa ya uchunguzi ya wahalifu waliomteka na kumjeruhi, Kibanda.
Akizungumza jana Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema kuwa ni mapema juu ya uchunguzi wa kuwabaini waliohusika katika tukio hilo.
Kova alisema Kibanda ndiye anafaa kuwa shahidi wa kwanza katika tukio hilo, wa kusema kilichotokea lakini kutokana na hali yake hawezi kuhojiwa hadi apate ahueni.
Kova alisema tukio hilo ni kubwa na Jeshi la Polisi Makao Makuu limetoa askari wanne ambao wataungana pamoja na wale wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ambao wamebobea katika uchunguzi.
Wanaharakati wazungumza
Naye mwanaharakati Onesmo ole Ngurumwa, alisema matukio haya yanajirudia na kwamba walikwishatoa tahadhari hivi karibuni kuwa hali si nzuri kiusalama hususan kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014.
Ole Ngurumwa alisema kuna tatizo katika vyombo vinavyosimamia usalama kwani vimekuwa vikifanya kazi kwa ubaguzi.
Alitolea mfano tukio la Dk. Ulimboka na mwanaharakati mmoja aliyeuawa mkoani Mara kwamba hadi leo polisi matukio yote hayo na mengine haijayatolea taarifa za kukamatwa waliohusika.
“Kuna taarifa nyingi tu za vitisho kwa wanaharakati, waandishi wa habari na watu wengine lakini bado havifanyiwi uchunguzi, hali ambayo ni ya hatari,”alisema.
Alisema ni lazima waandishi wenyewe wakajiimarishia ulinzi wao kwa kujenga ushirikiano bila kajali tofauti zao.
Ole Ngulumwa alisema matukio hayo yanatokana na waandishi kuibua uozo wa baadhi ya watendaji wasiopenda kutenda haki sasa wanapoguswa huamua kuwadhuru waandishi.
Naye mwandishi mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, alisema kwa sasa wananchi wanapaswa kusubiri ripoti ya Jeshi la Polisi watasema nini juu ya tukio hilo.
Alisema ni wazi watu waliomdhuru Kibanda walikuwa na dhamira ya kumuondolea uhai wake, kwa kuwa kama wangekuwa ni wezi wangeweza kuchukua vitu vilivyokuwa katika gari lake.
“Hawa ni watu wasiompenda Kibanda, naipa pole familia yake, watu wa tasnia ya habari juu ya ukatili huu uliofanywa kwa mwenzetu. Cha msingi tutoe nafasi kwanza kwa ajili ya uchunguzi alisema,” Ulimwengu.
Tukio la kuvamiwa na kuumizwa kwa waandishi wa habari si geni nchini kwani katika miaka ya karibuni Mhariri Mtendaji wa gazeti la MwahaHalisi, Saed Kubenea, alivamiwa ofisini na kumwagiwa tindikali usoni huku mwandishi mwenzake, Ndimara Tegambwage, akikatwa mapanga kichwani.
Pia Septemba 2, mwaka jana, mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kulipuliwa na bomu akiwa kazini kijijini Nyololo.

chanzo:tanzaniadaima

No comments:

Post a Comment