Tuesday 6 August 2013

Mtanzania mwingine adakwa na madawa Thailand

SIKU chache baada ya serikali za Tanzania na Thailand kutiliana saini mkataba wa kubadilishana wafungwa na kutekeleza sheria ya vifungo, raia wa Tanzania amebambwa na dawa za kulevya nchini humo.

Mtanzania huyo aliyefahamika kwa jina moja la Kileo, alikamatwa Jumanne wiki iliyopita katika kisiwa cha Macau akiwa amemeza dawa hizo aina ya cocaine akielekea China.

Kwa mujibu wa maofisa wa polisi wa Thailand, dawa hizo zinakadiriwa kufikia kilogram 1.091, zikiwa na thamani ya dola za HongKong 900,000.

Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra, akiwa ziarani nchini alitiliana saini na serikali kubadilishana wafungwa, jambo ambalo baadhi ya wadadisi wa mambo walidai ni hatua ya kuwanusuru vigogo waliofungwa huko kwa makosa ya kujihusisha na biashara hiyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi wiki hii kwenye makao makuu ya polisi, msemaji wa polisi nchini Thailand alisema wanamshikilia Kileo (37) aliyekamatwa Jumanne 5:30 asubuhi kwenye eneo la kukagua mizigo katika uwanja wa ndege.

“Polisi walimsimamisha baada ya kumtilia shaka na kumweka katika kamera za X-ray ndipo wakabaini kuna kitu tumboni.

Alisema kuwa baada ya kubaini kuwa ana kitu kisicho cha kawaida tumboni alichukuliwa na kupelekwa kwenye hospitali ya Conde de Sao Januario kwa uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa gazeti la ‘The Macau Post Daily’ la nchini humo lililochapisha habari hiyo, polisi walisema kuwa mshukiwa huyo aliwaambia kuwa alichukuliwa ili kusafirisha dawa hizo kutoka mji mmojawapo ulioko Tanzania mapema mwezi huu.

Taarifa zaidi zilisema kuwa mtuhumiwa huyo awali alipanda ndege kwenda Ethiopia kisha akaenda Thailand mahali alipomeza dawa hizo na baadaye akapanda ndege hadi kisiwa cha Macau ili kuelekea Guangzhou mahali ambapo alitarajiwa kuonana na mchora mpango wa sakata hilo.

Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.

Polisi walisema kuwa Kileo aliwaeleza kwamba alilipwa dola za Marekani 7,000 kukubali kumeza na kusafirisha dawa hizo.

Hii ni mara ya pili ndani ya wiki mbili kwa raia wa Tanzania kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumeza na kusafirisha dawa za kulevya.

Mtuhumiwa mwingine alitokea kusini mashariki mwa Afrika na kisha kukamatwa na polisi baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Thailand Julai 10 mwaka huu.

Mtuhumiwa huyo pia aliwaeleza polisi hao kuwa alipita akiwa amemeza dawa za kulevya na kuzisafirisha kupitia njia ile ile.

Polisi bado wanachunguza kama watuhumiwa hao walichukuliwa na kundi lilelile linalosafirisha dawa ya kulevya.

Tanzania Daima - 06, July 2013

No comments:

Post a Comment